in , ,

Tulitamani Singida Iwe Azam Fc, Azam Fc inatamani iwe Singida United

Heka heka uwanjani

Tumaini lilianza kujengeka mioyoni mwetu kwa sababu tuliona kuna kitu
kinachoitwa “mbadala” katika mpira wetu.

Wengi wetu tumechoka na tunataka kuona mabadiliko makubwa yenye mwanga
wa mafanikio katika mpira.

Ndiyo maana tunapoona mtu anakuja kama “mbadala” wa maendeleo ya mpira
wetu humpenda na kumpa ushirikiano mkubwa huku tukimtia moyo aweze
kufikia tunapopatamani.

Tunatamani sana tufike mbali kwenye mchezo huu tunaoupenda sana,
tunatamani kuona timu kubwa za Taifa zikija hapa na kuondoka zikiwa na
huzuni kutoka kwenye timu yetu ya Taifa.

Tunatamani kuona TP Mazembe mpya katika ardhi yetu, ndiyo maana
tulifurahi sana tulipowaona Azam FC wakija na uwekezaji mkubwa.
Waliwekeza kwa kiasi kikubwa sana katika klabu.

Klabu ya Azam FC ikawa na uwanja wake wa mazoezi pamoja na uwanja wa
kuchezea mechi, hata wachezaji waliishi katika mazingira bora kwa
sababu hosteli nzuri zilijengwa kwa ajili yao.

Waliweka vitu vingi vya muhimu kwenye klabu, tukawa tunasubiri ni lini
Azam FC itakuwa na uwezo wa kumtoa TP Mazembe katika michuano ya
kimataifa.

Subira yetu haikuwa na kikomo, tuliamini ipi siku itatokea hivo
hatukuchoka kusubiri. Wakati tukiwa tunasubiri Singida United masikio
yetu yakasababisha macho yetu yaitazame Singida United kwa shauku.

Tuliona dalili za nafanikio mengine pia sehemu hii, dunia ya sasa
mpira ni biashara. Biashara ambayo unaweza kutangaza bidhaa za
mfanyabiashara na klabu ikanufaika.

Eneo hili halijawahi kutiwa mkazo katika mpira wetu, lakini Singida
United walituonesha kuwa inawezekana kupata wadhamini kwenye mpira
wetu kama utakuwa na uongozi wenye ushawishi nje ya uwanja.

Walionekana kuiendesha kibiashara timu, hawakusita kwenda na barua za
maombi za kutaka udhamini sehemu mbalimbali, uoga wa kuwa ni timu
changa iliyopanda daraja haukuwepo ndani yao.

Mikakati yao dhabiti juu ya uendeshaji wa klabu yao waliianisha kwenye
barua za kuomba udhamini na waliwavutia wengi mpaka wakafanikiwa.

Ile dhana ya kwamba wadhamini hupenda timu kubwa ikaondoka, tukabaki
tukisubiri kipi kitafuata baada ya wadhamini.

Ni mapema sana kutoa hitimisho kwa Singida United kwa sasa lakini
ukweli ni kwamba walipoamua kufanyia ukarabati uwanja wa Namfua
tuliamini wanafuata njia za Azam FC.

Lakini hofu yangu ni moja, wanaweza wakawa wanapitia njia aliyotumia
Azam FC lakini wakashindwa kujua kwanini njia ile haijafanikisha
kuwafikisha Azam FC mbali?

Azam FC wamewekeza sana kwenye klabu na kuisahau timu kitu hiki
kinaonekana kwa Singida United. Mikakati yao mingi ni kuwekeza kwenye
klabu na kuisahau timu.

Unaweza ukawa na kiwanja, Gym, Hostel, bwawa la kuogelea na wadhamani
wengi kwenye timu lakini kama hujawekeza kwenye timu ni ngumu kupata
mafanikio makubwa.

Timu haiishii kuwa na kocha wa kigeni na wachezaji wengi wa kigeni
peke yake. Kuna maeneo mengi ambayo hatutaki kuyafikiria kuyawekeza
kwenye timu.

Hatuna sporting director, director of football, scouts, wachambuzi wa
kwenye timu. Ni watu muhimu kwenye timu lakini hawapewi kipaumbele
kikubwa.

Ndiyo maana ni rahisi kwa timu kusajili mchezaji wa kiwango cha chini
(awe kutoka ndani au nje ya nchi) kwa sababu timu hawana scouts wa
kuwafuatilia wachezaji hawa kabla hawajasajiliwa ili kujua kama ana
kiwango kinachokidhi mahitaji ya timu.

Hata kwenye mechi za kimataifa hatuna wachambuzi ambao hutumwa na timu
kwenda kuangalia timu pinzani na kuja na uchambuzi wa uchezaji wa timu
husika, mpira sasa hivi una uwekezaji mkubwa wa mbinu ndani ya uwanja
unatakiwa uwe na watu wa aina kipindi mechi inapoendelea ili
kusaidizana na benchi la ufundi kuona madhaifu ya timu husika kimbinu
na kimfumo.

Tuliwaona Azam FC wakijenga hostel tukajua ni muda sahihi kwao wao
kuwa na timu za vijana ili kuzalisha wachezaji watakaotumika katika
timu ya wakubwa kwa baadaye au kuwauza kwenye timu zingine, lakini
njia waliyopo Azam Fc inawarudisha kukutana na Singida United
inapokuja sehemu ambayo Azam FC imekwama.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

NATAMANI KUSIKIA LWANDAMINA KARUDI YANGA

Tanzania Sports

JANA MLIMTEGEMEA MANJI, LEO MTENGENEZENI MANJI WENU