in , , ,

TUKITOKA BOTSWANA NA MISRI TUNATAKIWA KUFANYA YAFUATAYO

Hadithi imejirudia ile ile, hatujawahi kuwa na hadithi mpya tena
yenye kufurahisha kwenye michuano ya kimataifa iwe katika ngazi ya
vilabu au timu ya Taifa.

Hii ni kwa sababu hatuna misingi imara ambayo tumeijenga sisi kama
sisi ya kutuwezesha tufanye vizuri kwenye michuano hii ya kimataifa.

Misingi hii haipo kwenye ligi zetu, shirikisho la mpira wa miguu
Tanzania mpaka kwenye vilabu vyetu

Ligi zetu zimekuwa dhaifu sana kuanzia ligi za ngazi za chini mpaka
ngaji ya juu (ligi kuu).

Tumetengeneza mazingira ambayo tunatoa timu ambazo siyo shindani kwa
sababu ya mazingira mbalimbali kama waamuzi, uwezo wa kuibua vipaji
ambavyo vitaleta msaada mkubwa kwenye timu husika.

Ndiyo maana hata timu ambazo zinapanda madaraja mbalimbali zinakuwa
timu ambazo ni dhaifu.

Mfano mzuri ligi daraja la kwanza imekuwa ligi yenye kulalamikiwa sana
kila siku na hii ni kwa sababu aina ya uendeshwaji wake.

Timu nyingi zimekuwa zikiandaliwa mazingira ya uonevu zinappkuwa
katika viwanja vya ugenini, na kuna wakati mwingine waamuzi uhusika
moja kwa moja kuharibu mazingira ya mchezo.

Kitu hiki hupelekea kupandisha timu ambazo ni dhaifu katika ligi kuu,
ligi ambayo inatoa mwakilishi wa Tanzania katika michuano ya
kimataifa.

Yanga

Ni ngumu kupata mwakilishi dhabiti wa kuiwakilisha nchi kama una ligi
ambayo ina idadi kubwa ya timu ambazo ni dhaifu.

Bingwa wa ligi atapata jaribio ambalo jepesi ambalo litamfumba macho
nakujiona yeye ni bora.

TFF wanatakiwa kusimamia ligi daraja la kwanza iwe ligi ambayo
inachezwa kwa haki ili tupate timu imara katika ligi kuu.

Kuna kanuni inayo zitaka kila timu za ligi kuu kuwa na timu za vijana,
na timu hizo za vijana zinatakiwa zicheze mechi ya utangaluzi kabla ya
mechi ya wakubwa.

Hii kanuni usimamizi wake hauwekewi mkazo na TFF, na vilabu
vinachukulia kitu cha kawaida.

Maendeleo halisi ya mpira wa miguu yanaanzia chini, hayaanzi kwa mtu
mwenye umri wa miaka mingi.

Hatuna muendelezo wa kupata vipaji bora kwa sababu hatuna mazingira
mazuri ambayo yanawezesha vilabu kuibua , kulea na kuvikuza vipaji
mbalimbali.

Vilabu vyetu vimekuwa vikiegemea katika kusajili wachezaji kwa kutumia
pesa nyingi kitu ambacho kuna wakati wanapata wachezaji ambao hawana
viwango vikubwa.

Kitu ambacho kama wangeamua kugeuka na kuanza kuibua, kulea na
kuvikuza vipaji mbalimbali vya watoto wangepata urithi mkubwa wa
vipaji ndani ya timu ya wakubwa na kuwafanya wao waendelee kuwa
washindani kwa muda mrefu.

Tunatakiwa tusijilaumu kwanini tumetoka kwenye mashindano, tunatakiwa
kujiuliza kwanini tumeshindwa kufanya vizuri kwenye mashindano haya.

Kuna umuhimu kwetu sisi kuumizwa na matokeo tunayoyapata katika
mashindano ya kimataifa.

Yanga na Simba

Tunaamua kushindana kimataifa huku tunasura ya kitaifa, hatuna sura ya
kimataifa ndani yetu?

Uliiona jezi ya Al-Masry? ina chapa za wadhamini kuanzia kuanzia nguo
ya juu mpaka bukta yao.

Hii inawafanya kuendesha timu katika mazingira rafiki, mazingira
ambayo yanatia motisha kwa wachezaji wetu lakini kwetu sisi ni tofauti
sana

Mfano wadhamini wa Township Rollers waliokuwa wanacheza na Yanga ni
wadhamini nane (8), wakati Yanga ina mdhamini mmoja tu msimu huu
ukiachana na macron ambaye mkataba wake unaanza msimu kesho

Hii inaonesha tofauti ya uendeshwaji wa timu za wenzetu na timu zetu,
hakuna misingi mikubwa ya kibiashara inayohusika kuendesha timu zetu.

Hivo wakati tunatoka Botswana na Misri tunatakiwa turudi na somo kubwa
ambalo tunatakiwa kulifanya kwa vitendo

Somo la kujiendesha kibiashara kwa timu zetu ili kupunguza gharama za
uendeshaji na kuongeza morali kwa wachezaji

Hata somo la kurudi katika misingi ya kuibua vipaji tunatakiwa
tusilipuuzie, wakati tunaiendesha timu kibiashara ndiyo wakati huo huo
tunaotakiwa kufikiria kuanzisha timu za vijana ambazo zitakuwa chachu
kwenye maendeleo yetu.

Maendeleo ambayo yatachagizwa kwa kiasi kikubwa na TFF kuamua
kusimamia ligi ziwe na ushindani mkubwa ili tupate wawakilishi imara.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

TIMU ZIPI ZINA NAFASI KUBWA YA KUTINGA NUSU FAINALI YA LIGI YA MABINGWA?

Tanzania Sports

VIATU VYA SCOTT VIMEFICHA PESA ZA POGBA