Olympics
Baraza jipya la Michezo la Taifa (BMT)
SERIKALI imetangaza Wajumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambalo ni chombo cha juu cha kuratibu masuala ya michezo nchini.
Uteuzi huo unafanyika wakati Tanzania inaadhimisha miaka 50 tangu kupata uhuru mwaka 1961 ikiwa imewahi kung’ara kimataifa kwa mchezo wa riadha hususan miaka ya 70 ambapo wanariadha kadhaa walifanikiwa kupata medali za dhahabu.
Aidha Serikali inateua wajumbe wakati timu nyingi zilizoshiriki michuano ya kimataifa kwa miaka 50 iliyopita zikiwa zikiambulia vipigo.
Wajumbe wa baraza hilo sasa ni pamoja na Mwenyekiti wake Dionis Malinzi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU) na mfanyabiashara.
Wajumbe wengine ni Jenister Mhagama ambaye ni mbunge wa Jimbo la Peramiho na mmoja wa viongozi wa michezo katika Bunge la Tanzania.
Mjumbe mwingine kutoka Bunge hilo ni Mkiwa Kimwanga ambaye ni wa Viti maalumu wa Chama cha CUF ambacho kinashirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Chama cha Mapinduzi kwenye utawala wa Zanzibar.
Wengine ni Jamal Rwambow ambaye ni polisi mwandamizi Dar es Salaam, Venance Mwamoto ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Kilolo na pia mchezaji wa soka, Juma Pinto ambaye ni Katibu mkuu wa chama cha waandishi wa habari za michezo(Taswa) na Mkurugenzi wa gazeti la Jambo Leo.
Wengine ni Dk Cyprian Maro, Kanali Eliot Makafu, Jeniffer Mmasi, Ramadhan Dau ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Alex Mgongolwa ambaye ni wakili pamoja na Maulid Kitenge ambaye ni mtangazaji wa Kituo cha Radio One na Kituo cha Televisheni cha ITV.
Wajumbe wengine ambao ni wajumbe kwa nyadhifa zao ni Mkurugenzi Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, Kamishna wa Elimu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwakilishi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Mkurugenzi wa Michezo kutoka Wizara ya Habari, Vijana , Utamaduni na michezo na Mwakilishi kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa ujumla Baraza hilo ni chombo kikubwa ambacho kinatakiwa kuwa na wajumbe wanayoielewa vema michezo nchini.
Mbali ya kuielewe pia ipo haja ya kuwa na wajumbe waliobobea kwa kushiriki na kuipatia sida timu yoyote waliyoshiriki ama Tanzania kwa ujumla.
Dunia ina aina nyingi za michezo na Tanzania hali kadhalika ina michezo ya aina nyingi.
Tanzania kwa miaka mingi imekuwa ikishiriki michezo mbalimbali ya kimataifa, lakini asilimia 99 timu zinazoshiriki zinarudi mikono mitupu.
Hivyo uteuzi wa wajumbe hao umeanza kuibua hoja za je walioteuliwa watasaidia kuimarisha michezo nchini?
Baadhi ya wadau wa michezo jijini Dar es Salaam wanahoji vigezo vilivyotumika kuwateua huku wakisema baadhi yao hawana sifa hata za kuongoza michezo katika ngazi ya kata.
“Walioteuliwa wengi ni wapenzi wa soka kuliko michezo mingine mingi, je kweli watasaidia maendeleo ya michezo Tanzania?”, anahoji mwanamichezo kutoka wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam.
Wanadai michezo nchini ipo ya aina nyingi tofauti ya baadhi ya wajumbe wanavyoujua mpira wa miguu peke yake.
Wadau wanasisitiza kwamba Tanzania ina michezo mingi na ndio maana wameunda vyama vingi vya michezo na mashirikisho ya vyama hivyo nayo mengi pia.
Lakini Mwenyekiti wa BMT Dionis Malinzi aliwaambia waandishi wa habari kwamba vyama vingine ni vya mfukoni na kwamba vikae chonjo kufutwa.
Wapenzi wa michezo pia wanatilia shaka utendaji wa baraza hilo kwani wanasema ofisi zake zilizopo karibu na Uwanja wa Uhuru ni chafu mithili ya magofu.
Wanatilia shaka pia uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Dau anayefanya kazi kwenye jengo refu kuliko yote nchini Tanzania kwamba unalenga kumwomba ufadhili zaidi badala ya kusaka maendeleo ya michezo Tanzania.
Lakini baadhi ya wajumbe walisisitiza kwamba watafanya kazi zao kwa kufuata sheria taratibu na kanuni za miochezo nchini.
Wanasema watavitambua vyama vyote na mashirikisho yake na kuendeleza michezo bila kupendelea aina moja ya mchezo.
Swali ni je, medali za dhahabu zitaonekana nchini au Tanzania itaendelea kuwa kichwa cha mwenda wazimu?
.
Baadhi ya vyama hivyo ni Tanzania Olympic Committee (TOC), Tanzania Basketball Federation (TBF), Tanzania Swimming Association (TSA), Tanzania Paralympic Committee (TPC), Tanzania Amateur Netball Association (TANA), Tanzania Cricket Association (TCA), Tanzania Football Federation (TFF), na Automobile Assocatioan of Tanzania (AAT).
Vyama vingine ni Chama cha Netiboli Tanzania(Cheneta), Tanzania Amateur Handball Association (TAHA), Tanzania Table Tennis Association (TTTA), Tanzania Volleyball Association (TAVA),
Boxing Federation of Tanzania (BFT), Tanzania Golf Union (TGU), Tanzania Amatuer Darts Association (TADA), Football Referees Association of Tanzania (FRAT), Tanzania Football Coaches Association (TAFCA) na Soccer Players Union of Tanzania (SPUTANZA).
Kama haitoshi pia vipo vyama vya Tanzania Tennis Association (TTA), Cycling Association of Tanzania(CAT), Judo Association of Tanzania (JATA), Tanzania Association of Youth Soccer Academics (TAYSA), Tanzania Badminton Association (TBA), Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara (SHIMIWI),
Shirikisho la Michezo Mashirika ya Umma Tanzania (SHIMMUTA), Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA),
Tanzania Shooting Association (TSA), Tanzania Scrabble Prayers Association (TSPA), Tanzania Sailing Association,
Shirikisho la Michezo la Vyuo Mchanganyiko, Tanzania (SHIMIVUTA),
Umoja wa Michezo Shule za Msingi, (UMITASHUMTA).
Tanzania Rugby Union (TRU), Tanzania Athletics Coaches Association (TACA), Amateur Wrestilling Association of Tanzania (AWATA), The Union of Taekwondo Tanzania (UTT), Tanzania Weightlifting Federation (TWF), Tanzania Shotkan Karate (TASHOKA), Tanzania Special Olympic (SOT),
Tanzania Hockey Association (THA), Athletic Tanzania (AT), Tanzania Deaf Sports Association (TDSA), Tanzania Sports Medecine (TASMA) na
Chama cha Michezo ya Jadi (CHAMIJATA).