Droo ya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa iliyochezeshwa jana Ijumaa imewapanga wawakilishi pekee wa Ligi Kuu ya England kukutana. Vita ya Jurgen Klopp dhidi ya Pep Guardiola ndiyo vita inayosubiriwa kwa hamu zaidi kuliko nyingine yoyote katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu huu.
Mabingwa watetezi Real Madrid wao wamepangwa kukutana na wahanga wao wa mchezo wa fainali wa msimu uliopita, Juventus. Vinara wa La Liga FC Barcelona safari hii watakutana na AS Roma wakati wababe wa Manchester United, Sevilla FC watakuwa na kibarua kigumu cha kujaribu kufanya miujiza dhidi ya wababe wa Ujerumani, Bayern Munich. Nani ana nafasi gani ya kutinga nusu fainali?
Liverpool v Manchester City (Aprili 4 na Aprili 10)
Liverpool ndiyo timu pekee iliyofanikiwa kuwafunga Manchester City kwenye mchezo wa EPL msimu huu. Wanaungana na Wigan Athletic kufanya timu mbili pekee ambazo zimewafunga vinara hao wa EPL kwenye michezo muhimu. Liverpool na Manchester City ni timu zenye aina inayofanana ya mchezo. Zote hizi hukabia juu zaidi na hujikita zaidi kwenye mashambulizi.
Tatizo lililopo kwa kila upande ni kwamba timu pinzani inapofanikiwa kuwapenya wakabaji waliopanda juu zaidi ya uwanja, timu hiyo hupata urahisi wa kutengeneza nafasi za kufunga mabao. Matokeo ya 4-3 kwenye mchezo wa EPL uliopigwa Januari baina yao yalitoa taswira ya uimara na udhaifu wa pande hizi mbili. Tutarajie mchezo wa kuvutia na mvua ya magoli kwenye michezo baina ya wawakilishi hawa pekee wa Ligi Kuu ya England.
Klopp ana rekodi nzuri zaidi dhidi ya Pep Guardiola kuliko mpinzani wake huyo. Katika michezo 12 dhidi yake ameshinda 6 na kutoa sare 1. Hata hivyo Pep ana kikosi kizuri zaidi cha wachezaji na pengine ni fundi zaidi kimikakati. Manchester City wana nafasi kubwa zaidi ya kuingia nusu fainali kwa mara ya pili kwenye historia yao baada ya ile ya 2015/16 chini ya Manuel Pellegrini.
Juventus v Real Madrid (Aprili 3 na Aprili 11)
Ni marudio ya mchezo wa fainali wa msimu uliopita ambayo Real Madrid waliibuka washindi kwa 4-1 ndani ya dimba la Millenium jijini Cardiff. Pia ni marudio ya nusu fainali ya 2014/15 ambayo Juventus walifanikiwa kuwaondosha miamba hawa wa Hispania kwa jumla ya mabao 3-2 na kutinga fainali ambayo walikwenda kupoteza kwa 3-1 dhidi ya FC Barcelona ya Luis Enrique.
Juventus walionesha morali ya maana upiganani walipowaondosha Tottenham kwenye hatua ya 16 bora kwa jumla ya mabao 4-3. Cristiano Ronaldo na wenzake kwa upande wao walivuka kirahisi katika hatua ya 16 bora dhidi ya PSG waliopewa nafasi kubwa ya kuwafungisha virago mabingwa hao watetezi. Kikosi kizuri zaidi cha Real Madrid na rekodi yao ya maana kwenye michuano hii kinawapa nafasi kubwa ya kuibuka wababe na kutinga nusu fainali.
FC Barcelona v as Roma (Aprili 4 na Aprili 10)
Ushindi wa jumla wa 4-1 wa vinara hawa wa La Liga dhidi ya Chelsea katika hatua ya 16 bora umewatambulisha rasmi kama timu yenye nafasi kubwa ya kuibuka mabingwa wa mashindano haya msimu huu. Lionel Messi alifunga matatu kati ya mabao yao manne kwenye hatua hiyo na kufikisha mabao 100 kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa.
Roma wao walivuka kwa sheria ya bao la ugenini wakipoteza kwa 2-1 ugenini na kushinda 1-0 nyumbani dhidi ya mabingwa wa Ukraine, Shakhtar Donetsk. Wana kibarua kigumu cha kuwazuia FC Barcelona kutinga nusu fainali. Barcelona ndiyo timu yenye rekodi ya kuruhusu mabao machache zaidi msimu huu wa Ligi ya Mabingwa wakiwa wameruhusu mawili pekee. Lionel Messi na nyota wao wengine mahiri wanawapa nafasi kubwa ya kuvuka.
Sevilla v Bayern Munich (Aprili 3 na Aprili 11)
Kwa mara ya kwanza timu hizi mbili zinakutana. Wakati Bayern Munich wakipita kwa urahisi na kishindo kwa ushindi wa jumla wa 8-1 dhidi ya Besiktas ya Uturuki, Sevilla ya mwalimu Vincenzo Montella ambayo inakamata nafasi ya tano kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Hispania walipigana na kuonesha soka safi dhidi ya Manchester United na kuvuka kwa ushindi wa jumla wa 2-1.
Sevilla ni moja kati ya timu za wastani zenye uthubutu na morali kubwa ya upiganaji. Sare mbili za mabao dhidi ya Liverpool kwenye hatua ya makundi na ushindi wa 2-1 ndani ya Old Trafford msimu huu zinaunga mkono hoja hiyo. Hata hivyo wana udhaifu mkubwa kwenye ulinzi na kikosi chao hakina wachezaji wenye viwango vya juu unapowalinganisha na Bayern Munich. Inatarajiwa Bayern chini ya Jupp Heynckes watacheza nusu fainali.