Kuna tetesi kwamba Manchester United wanataka kuvamia Goodison Park na
kumchukua mshambuliaji wao, Romelu Lukaku wa Everton kiangazi
kinachokaribia.
Habari zilizovuja ni kwamba United wanataka kuongeza nguvu kwa
kumsajili Mbelgiji huyo mwenye umri wa miaka 22, hata kama kocha Lous
van Gaal hatawafikisha kwenye safari ya kushiriki Ligi ya Mabingwa
Ulaya (UCL).
Wakiwa ndani, Everton wanaelezwa kuhofia uwezekano wa mpachika mabao
huyo wa zamani wa Chelsea kuondoka, lakini wakitoka hadharani
wanatamba kwamba hauzwi kwa bei yoyote ile, kocga Roberto Martinez
amekuwa mwingi wa kusema hayo kwamba haondoki.
United wanaohenya kutafuta walau nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi
Kuu ya England (EPL) wanamenyana na Everton Jumapili hii, wakiwa na
uchu wa kupata pointi nyingi iwezekanavyo, ikizingatiwa kwamba ligi
inaelekea ukingoni.
Kocha wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho alichagizwa kwa kukubali
Lukaku aondoke Stamford Bridge, akaenda kung’ara Everton na hata
kuwatungua timu yake hao wa zamani. Mourinho anatajwa kuwa na nafasi
kubwa ya kushika hatamu Old Trafford msimu ujao, hivyo huenda
akarekebisha makosa yake kwa kumchukua mchezaji huyo wa kimataifa.
Mourinho anadaiwa kwamba yupo tayari kumsajili kiungo wa zamani wa
Arsenal, Lassana Diarra, 31, iwapo ataajiriwa na Manchester United .
Liverpool wanaongoza mbio za kumsajili mshambuliaji wa Dynamo Kiev,
Andriy Yarmolenko, 26, anayedaiwa kwamba anawaniwa pia na Arsenal na
klabu nyingine za ligi kuu.
Liverpool waliamua kuachana na mpango wa kumsajili kiungo Sadio Mane,
23, kabla hajaamua kwenda Southampton, eti kwa sababu program moja ya
kompyuta waliyotumia iliwaonesha kwamba hatawaongezea thamani kwa bei
aliyokuwa akiuzwa.
Chelsea wanapanga kumwaga pauni milioni 52 kwa ajili ya kuwasajili
nyota wawili wa Roma, kiungo Radja Nainggolan, 27 na mlinzi Kostas
Manolas, 24. Wawili hao wanadaiwa kuwa katika mpango mkakati wa kocha
mpya mtarajiwa, Antonio Conte.
Kocha wa West Ham, Slaven Bilic amesema amekuwa akichukuliwa muda wake
mwingi kwa kupigiwa simu na mawakala wa wachezaji wanaotaka kujiunga
na timu yake inayofanya vyema katika ligi.
Kocha wa Man United, Louis van Gaal amesema kwa kusoma alama za
nyakati, anaona wazi kwamba kuna dalili hatakuwa kocha wa Manchester
United msimu ujao. Amelalamikiwa na wadau wengi, wakiwamo wachezaji
wake mwenyewe, wachezaji wa zamani na washabiki kwa mtindo wake ambao
hauvutii wala kuzaa matunda yanayotakiwa.
Matatizo ya Crystal Palace uwanjani yanadaiwa kusababishwa na
wachezaji kutopendezwa na jinsi wanavyopishana kwa pengo kubwa la
mishahara.
Tottenham Hotspur wanamfuatilia mshambuliaji wa Utrecht, Sebastien
Haller, 21, wakati wakiandaa mpango wa usajili kwa ajili ya msimu
ujao. Spurs wamekaa vizuri kwenye msimamo wa ligi, wakiwa wa pili na
wanawakimbiza Leicester.
Barcelona wanajipanga kuwapa Manchester United pauni milioni 12 ili
kumsajili mlinzi Marcos Rojo, 26.
Kipa wa Arsenal aliye kwa mkopo Roma, Wojciech Szczesny, 25, amesema
kwamba angependelea kubaki Italia ili apate muda zaidi wa kucheza,
badala ya kurudi kusugua benchi Emirates.
Kocha wa zamani wa Newcastle, John Carver amebainisha kwamba ametuma
maombi ya kazi ya ukocha Aston Villa, kwa kuwa nafasi hiyo ipo wazi
kutokana na kufukuzwa kwa Remi Garde aliyeenda hapo kwa ushauri wa
Arsene Wenger. Villa wanaelekea kushuka daraja.
Manuel Pellegrini amedai kwamba kutolewa mapema habari kwamba
ataondoka Manchester City mwishoni mwa msimu hakujampunguzi uwezo wa
kufundisha wala kuhamasisha wachezaji wake ili wapate ushindi.