Italia wamtaka Radamel Falcao
*Man United kutumia pauni milioni 150
*Mirallas atafuta timu kubwa za Ulaya
PILIKA za usajili bado hazijazaa matunda makubwa kivitendo, lakini makocha, mawakala na wachezaji wanahangaika kuhakikisha wanakuwa pazuri mwishoni mwa mwezi huu.
Miamba wa Italia, Juventus na Roma wapo tayari kuzungumza na Manchester United kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wao aliyetoka Monaco kwa mkopo, Radamel Falcao, anayeelekea kutokuwa na furaha Old Trafford kwa kutopewa muda wa kutosha wa kucheza.
Wataliano hao wanataka kujiimarisha kwa ajili ya awamu ya pili ya Serie A, huku Manchester United wakiwa wamepata kunukuliwa wakisema kupitia kwa kocha wao, Louis van Gaal kwamba mchezaji huyo anaweza kucheza dakika 20 tu kwa mechi.
Katika hatua nyingine, mabosi wa United wanadaiwa kumpa fursa Van Gaal kusajili zaidi kuimarisha kikosi chao kinachoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, ikidaiwa zitamwagwa pauni milioni 150.
Kipaumbele cha United kwa sasa ni kuimarisha sehemu ya ulinzi na kiungo, ikidaiwa kwamba kusudio la kwanza ni kumnasa mlinzi wa Borussia Dortmund, Mats Hummels anayewaniwa pia na Arsenal.
Roma kwa upande wao, wapo tayari kusikiliza ofa ya Manchester United kwa kiungo wao Kevin Strootman (24), lakini Rais James Pallotta amebashiri kwamba itakuwa ofa ya kipuuzi ambayo haiwezi kukubaliwa.
Kiungo wa Everton, Kevin Mirallas (27) amezionesha klabu kubwa za England na Ulaya kwa ujumla kwamba anaweza akajiunga nazo, baada ya kukataa kusonga mbele na majadiliano juu ya mkataba wake unaoelekea ukingoni hapo Goodison Park.
Liverpool wamepata pigo baada ya kaka wa mshambuliaji Gonzalo Higuain ambaye pia ni wakala wake kusema kwamba mchezaji huyo wa Argentina hatarajii kuondoka Napoli, licha ya kuwapo habari kwamba anawaniwa na Liverpool.
Kocha David Moyes wa Real Sociedad anataka kumsajili mshambuliaji wa Burnley, Danny Ings (22), Mwingereza anayewania pia na klabu nyingine kadhaa za Ligi Kuu ya England.
Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers amesema kwamba mchezaji wake, Lukas Leiva haendi popote, huku yule wa Crystal Palace, Alan Pardew akisema huenda wakatoa dau kumsajili mshambuliaji wa Swansea, Bafetimbi Gomis (29) na beki Jose Enrique (28) wa Liverpool.
Aston Villa wamekuwa katika wakati mgumu kumpata kiungo Scott Sinclair (25) wa Manchester City, kutokana na klabu hiyo kutaka walipwe pauni milioni tatu ambazo Villa wanaona ni nyingi mno.
Mlinzi wa Celtic, Virgil van Dijk (23) amepokea kwa furaha taarifa kwamba Arsenal wanamhitaji. Huko huko Arsenal, mshambuliaji Alexis Sanchez (26) amemwambia bosi wake, Arsene Wenger asahau suala la kumpumzisha msimu huu.