Baada ya kuwa na msimu wa kwanza mbaya Chelsea, winga Juan Cuadrado, 27, anatarajiwa kuhamia Inter Milan nchini Italia.
Milan wanasema wapo tayari kufanya mazungumzo na Chelsea ili mchezaji huyo wa Colombia arejee katika Serie A.
Wawakilishi wa Liverpool wamekutana na Mkurugenzi wa Michezo wa Inter, Piero Ausilio kujadiliana uwezekano wa kumchukua kiungo wa Croatia, Mateo Kovacic, 21.
Juventus wa Italia wanawasiliana na Chelsea kwa ajili ya kumsajili kiungo mshambuliaji, Oscar, 23.
Santos wa Brazil wanafikiria kufungua mashitaka dhidi ya Barcelona, katikati ya sakata la kutofuatwa taratibu husika wakati wa kumsajili mshambuliaji wao, Neymar, mwaka 2013.
Mmiliki mwenza wa West Ham, David Sullivan anasema kwamba hawatafanya papara kuajiri kocha mya baada ya kuondoka kwa Sam Allardyce lakini wanaanza mchakato wa usajili wa wachezaji, wakiwa wametenga pauni milioni 25.
West Ham wanadaiwa kwamba wamepeleka maombi kwa mara ya pili kwa Frank de Boer wa Ajax ili ajiunge nao kama kocha kuanzia kiangazi hiki.
Washabiki wa Arsenal wamepata matumaini baada ya kiungo wao, Theo Walcott ambaye bado hajakubali kusaini mkataba mpya kusema kikosi cha Arsenal cha sasa ndicho kizuri zaidi alichopata kuwamo.
Walcott aneywindwa na Chelsea alifunga mabao matatu kwenye mechi ya mwisho wa ligi kuu dhidi ya West Bromwich Albion, alipochezeshwa nafasi ya ushambuliaji wa kati, baada ya kuwa majeruhi kwa muda na kisha kusugua benchi.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amesema kwamba Jack Wilshere ana majukumu makubwa ya kufanya katika timu yake na kupuuza madai ya kutakiwa kwake Manchester City.
Wenger amesema alifurahia soka yake tangu akiwa na umri wa miaka 17 hivyo hawezi kuonesha zaidi kwamba anamhitaji na kwamba wamekuwa wavumilivu sana pia juu ya majeraha yake ya mara kwa mara.
Newcastle wanafikiria kumchukua Patrick Vieira ambaye ni kocha wa vijana wa Manchester City ili afundishe kikosi chao msimu ujao.
Newcastle wapo chini ya kocha wa muda, John Carver, baada ya kuondoka kwa Alan Pardew aliyejiunga na Crystal Palace. Newcastle wamenusurika kushuka daraja siku ya mwisho wa msimu uliomalizika majuzi.