in , , , ,

TATHMINI YA MICHEZO YA JUMUIYA YA MADOLA ILIYOFANYIKA GLASGOW, SCOTLAND 2014. ​

Timu ya Tanzania

UTANGULIZI

Kuwa na Dira, Malengo, Mipango kuwekeza katika Kuibua vipaji, Kuviendeleza vipaji hivyo na kuvipatia Mashindano yalio muwafaka na kwa wakati muwafaka ni sehemu ya Majukumu makubwa na ya msingi kwa kila Chama na Shirikisho la Michezo la nchi yoyote duniani.

Mbali na Majukumu hayo, lakini pia ni wajibu kutekeleza, kufuatilia utekelezaji huo na kutathmini kwa lengo kujikosoa, kujirekebisha, kutengeneza na kuimarisha kwa lengo la kuleta Ufanisi na Maendeleo zaidi.

Jamii ya Wanamichezo na wale wote wenye kufuatilia kwa karibu shughuli na kalenda za michezo duniani, wanakumbuka kuwa mwaka 2014, Tanzania ilishiriki katika Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika mjini Glasgow, Scotland kuanzia tarehe 23 July hadi tarehe 3 August 2014. Kwa kweli lilikuwa ni Tamasha la kimichezo la aina yake ambalo lilikutanisha Wanamichezo mahiri kutoka nchi mbalimbali ambazo zilizowahi kutawaliwa na Dola ya Kingereza.

Tanzania imekuwa na historia ya kujivunia katika Michezo ya Jumuiya ya Madola. Ushiriki wa Tanzania katika Michuano ya Jumuiya ya Madola ulianza tangu mwaka 1962 katika Michezo iliyofanyika mji wa Perth, Australia.

Katika Michezoya Jumuiya ya Madola iliyofanyika mwaka 1970 mjini Edinburg, Scotland, bondia Titus Simba aliipatia Tanzania medali ya kwanza (fedha) kwenye mchezo wa ngumi wa uzito wa juu(Heavy weight).

Sote tunaelewa na sio rahisi kuisahau Michezo iliyofanyika mwaka 1974 huko Christchurch, New Zealand; katika Michezo hio kijana wa miaka 21 kwa jina la Filbert Bayi Sanka aliishangaza Dunia, mbali ya kushinda Medali ya Dhahabu, lakini pia alivunja Rekodi ya Dunia ya mbio za mita 1,500 kwa muda wa 3.32.2.

Mtanzania mwengine kwa jina la Gidamis Shahanga aliionyesha Dunia uwezo wa Wanariadha wa Tanzania pale aliposhinda Medali za Dhahabu katika mbio za masafa marefu (Marathon) huko Edmonton, Canada mwaka 1978. Shahanga aliweka historia ya kuwa mwanariadha wa pekee Tanzania kushinda Medali nyIngine ya Dhahabu katika mbio ya mita 10,000 miaka minne baadaye, katika Michezo iliyofanyika huko Brisbane, Australia mwaka 1982.

Hali kadhalika, katika Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika mjini Kuala Lumpar, Malaysia mwaka 1998, mwanariadha wa mbio za masafa marefu (Marathon) Simon Mrashani alishinda Medali ya Fedha na Gewey Suja Medali ya Shaba. Bondia Michael Yombayomba alipata Medali ya Dhahabu katika uzito wa juu.

Mwaka 2002 katika Mashindano ya Jumuiya ya Madola yaliyofanyioka Manchester, Uingereza Francis Robert Naali na John Yuda waliipatia Tanzania Medali ya Dhahabu na Shaba katika mbio za masafa Marefu (Marathon) na Mita 10000.

Historia yetu ya mwisho ya kujivunia ilikuwa ni mwaka 2006, wakati kijana Samson Ramadhan aliposhinda Medali ya Dhahabu katika Michezo iliyofanyika huko Melbourne, Australia na Fabian Joseph Naasi kupata medali ya Shaba katika mbio za Mita 10000.

Kwa masikitiko makubwa tangu wakati huo, Tanzania hatujaweza kufanya tena vizuri katika Michezo ya Jumuiya ya Madola si mwaka 2010 huko New Delhi, India na wala si mwaka 2014 huko Glasgow, Scotland.

KIKAO CHA TATHMINI
Kikawaida Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), hufanya tathmini ya kila jambo au shughuli inayoitekeleza. Mara nyingi sana TOC imekuwa ikijipangia kufanya tathmini ya kila Michezo inayoiratibu kama vile; Michezo ya Afrika, Michezo ya Jumuiya ya Madola na Michezo ya Olimpiki. Jambo hili, hupendeza pale linapojumuisha wahusika (stakeholders) wote yaani, Vyama vya Michezo, TOC, Wanamichezo walioshiriki na Serikali kupitia Wizara inayohusika na Michezo. Tathmini zimekuwa zikikwama kufanyika kutokana na ukosefu wa fedha. Pamoja na mipango mizuri ya kuandaa tathmini husika, juhudi za kuishirikisha Serikali kupitia Wizara husika (HVUM) angalau kusaidia kuchangia tathmini limekuwa likikwama.

Mwaka huu, tunashukuru utashi, upenzi na juhudi binafsi zilizofanywa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Bernard Membe (Mbunge) kwa kuwezesha Tathmini hii kufanyika.

Tathmini hiyo, ilifanyika tarehe 01 October 2014, katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Filbert Bayi iliyoko Mkuza Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Mgeni Rasmi, katika Kikao hicho cha Tathmini ambacho kilikuwa chini ya Uenyekiti wa Rais wa TOC Ndugu Gulam Rashid, alikuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Bernard Membe (Mbunge) ambapo mbali ya kukifungua Kikao hicho pia alikuwa msikilizaji aliyekuwa akijifunza kutoka kwa Viongozi wa Serikali, TOC, Vyama vya Michezo na Wanamichezo washiriki kuhusu maandalizi na ushiriki wetu Glasgow 2014.

Katika Risala yake ya Ufunguzi, Mheshimiwa Membe aliwapongeza Wanamichezo kwa juhudi zao na kuwataka kutokata tamaa na hadi kufikia kuwapa hadithi ya mwindaji, aliyekwenda kuwinda kwa mara ya kwanza na kurudi nyumbani mikono mitupu. Lakini baada ya kujiandaa vyema, mwindaji alipokwenda tena porini alifanikiwa kurudi na nyama nyingi.

Mheshimiwa Membe alivitaka Vyama vya Michezo na Wanamichezo kujiaandaa mapema na kurudia wito wa Mheshimiwa Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania kuwa, kumalizika kwa Michezo ndio mwanzo wa maandalizi ya kujiaandaa na michezo ijayo.

MAONI YA WALIMU WALIOANDAMANA NA TIMU, VYAMA NA WANAMICHEZO

Walimu, Viongozi wa Vyama/Mashirikisho ya Michezo na Wachezaji walioshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola, Glasgow 2014 walichangia ni kwanini timu zetu hazikurudi na Medali katika michezo hiyo.

Kwa ujumla waliishukuru Serikali (Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni/Michezo na Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa) hasa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Camillius Membe kwa ubunifu wake wa Mpango wa Diplomasia ya Michezo. Mpango huo uliwawezesha wanamichezo wetu kwenda katika nchi zifuatazo:- China (Riadha, Ngumi na Table Tennis), Ethiopia (Riadha), New Zealand ( Kuogelea na Riadha) na Uturuki (Judo na Ngumi).

Pamoja na mazoezi waliyoyapata katika nchi zilizotajwa kuwa ya muda mfupi, lakini baadhi ya wachezaji waliokuwa na maandalizi ya awali waliweza kufanya vizuri katika michezo yao waliyoshiriki huko Glasgow.

Waliiomba Serikali isaidie maandalizi vyama/mashirikisho wanaojiandaa kwa michezo ya Kimataifa kwa asilimia mia moja (100%). Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa ushiriki wa Michezo ya Kimataifa iongezwe na timu zetu kuandaliwa kama kweli tunataka medali, kwa kifupi Taifa liwekeze kwenye Michezo.

Michango binafsi ya kila mwalimu, viongozi wa Vyama/Mashirikisho ya michezo, wachezaji na TOC yalikuwa kama ifuatavyo:

A. WALIMU
1. Mwakipesile-BFT .
a. Kiwango cha Mchezo wa Ngumi Turkey kipo chini kwa hiyo wanamichezo wetu hawakupata mazoezi yaliyostahiki.
b. Mapendekezo – China ingekuwa sehemu nzuri kwa Wanamichezo wetu.
c. Walimu wa Ngumi wapatiwe Mafunzo zaidi.

2. Suleiman Nyambui – RT:
a. Taifa la Tanzania limekosa sifa ya Medali za ushindi kwa muda mrefu.
b. RT haiwezi kuandaa wachezaji bila mazingira mazuri.
c. Kwa Tanzania kupata nafasi ya fainali ni ushindi kwetu, akizungumzia Wanamichezo wetu walioingia fainali mita 10,000.
d. Bajeti ya maandalizi na Michezo kwa jumla bado ni finyu kwa michezo mbalimbali, hivyo ameiomba Serikali ione umuhimu wa kuwa na Bajeti ambayo itakidhi kugharamia Maandalizi ya Timu na ushiriki wa Tanzania katika Michezo ya Kimataifa.
e. Taifa liwe makini (serious) katika kuendeleza Michezo.
f. Kama mipango ya Vyama vya Michezo ni mibovu Wizara husika isaidie katika kuandaa.

3. Ramadhani Namkoveka – KUOGELEA.
a. Matokeo ya Glasgow ni mazuri ukilinganisha na ushiriki wa Tanzania katika Michezo iliyopita.
b. Facilities ni tatizo (mabwawa ya kuogelea) kwa sasa Tanzania haina “Olympic-size swimming pool”. Aliomba Serikali kujenga bwawa la kuogelea la kiwango cha Olimpiki.
c. Aliomba walimu wa mchezo kupatiwa Mafunzo.

4. Jax Mhagama-BAISKELI.
a. Shukrani kwa Mheshimiwa Waziri Membe kwa juhudi zake.
b. Kwa ujumla wahusika hawako makini katika Maandalizi na kushauri kuwepo na mashirikiano ya karibu zaidi
i. Vyama vya Michezo
ii. TOC.
iii. BMT.
iiii. SERIKALI.
c. Fedha za wafadhili ndizo zinazoendesha Vyama vya Michezo.

5. Zaidy Hamisi-JUDO.
a. Kambi zilifanyika Bara/Zanzibar zilikuwa za ushindani zaidi.
b. Kambi ya Uturuki haikusaidia sana kwa vile tulikuta wenzetu wakiandaa
wachezaji wadogo kwa kushiriki Michuano ya Olimpiki ya Tokyo 2020..
c. Tulikosa michezo ya majaribio.
d. Viongozi wa Serikali watembelee wachezaji kambini.
e. Maslahi ya wachezaji bado ni duni (2007- USD 30, 2014 USD 30) Tofauti
kubwa na nchi zingine.

B. VIONGOZI WA VYAMA VYA MICHEZO
1. Makore Mashaga KM-BFT.
a. Ruzuku kutoka Serikali kwa Vyama ni muhimu na lazima.
b. Alishauri Michezo kurudishwa mashuleni, lakini bado haijaratibiwa
vizuri kwa lengo la, kupata wachezaji bora wa baadaye.
c. Makampuni yanayowekeza hapa nchini yapewe majukumu ya kusaidia
Sekta ya Michezo mingine.
d. Viongozi wa Vyama nao washiriki / wahusishwe wakati wa mashindano
nje ya nchi.
e. Fursa zaidi kwa walimu na waamuzi.
f. Usimamizi wa TOC na Serikali ni muhimu.

2. Noel Kiunsi – KUOGELEA.
Maandalizi.
a. Ni muhimu nchi kuwa kuwa Bwawa la kuogelea (Olympic size swimming
pool).
b. Aliomba Vifaa vya Michezo visitozwe kodi.
c. Vyama vya Michezo kufanya kazi kwa pamoja.
d. Turudi kwa Vijana – kuibua, kuviendeleza na kuvilea vipaji.
e. Aliwashauri Viongozi wenzake kufanya Mashindano zaidi kwa lengo la
kupata fursa ya nchini Vyama vyetu na Wanamichezo watajifunza.

3. Issa Mtalaso – MPIRA WA MEZA.
a. Tuliridhika na mazoezi China.
b. Tulivimba vichwa vya ushindi.
c. Kuondokana na dhana ya kuachia Vyama pekee katika maandalizi.
d. Hakuna nchi inaendelea bila mkono wa Serikali.
e. Sera ya nchi imeua Michezo.
f. Bajeti kutoka mapema ili Vyama na Wanamichezo wajiaandae.

4. Innocent Mallya-JATA.
a. Mazingira ya kambi kwa maandalizi.
b. Uturuki wanajiandaa na Tokyo 2020 hii inaonyesha jinsi gani wenzetu
walivyo makini.
b. Uwezo wa nchi Ki-Michezo – ingekuwa vyema wachezaji wetu
wangepelekwa Russia, South Africa, Nigeria.
d. Vifaa vya Michezo.
e. Mechi za majaribio kufanyika tu kikanda.
f. Wafadhili; Ugumu wa kupata ufadhili.
g. Serikali kuandaa harambee maalum kwa ajili ya kugharamia Michezo.
h. Kuwe na Vikao vya Tathmini kama hivi siku zijazo.

5. Simon Machemba-BAISKELI.
a. Chuo cha Mallya – kukataa kuendesha programme maalum ambazo
zitasaidia kukidhi mahitaji ya Vyama vya Michezo (tailor-made) ambao wanasema hawawezi kufanya hivyo.
b. Vifaa vya michezo – kodi nk.
c. Sports Marketing-Donation na Sponsorship – vitu tofauti.
d. Mahusiano – CHABAZA NA RAS – Serikali.
e. TOC iheshimu “technical know-how”.

6. Nassor -BAISKELI ZNZ
a. Kuwepo kwa Michezo katika mashule.
b. Ukitoka shule hakuna ajira.
c. Wanamichezo wapewe nafasi ya ajira JWTZ, Polisi, JKT, Magereza nk.

C. WANAMICHEZO
1. Fabian Joseph-RT.
a. Hatuna sehemu ya mazoezi wanariadha wa mbio ndefu.
b. Kenya / Ethiopia wanaendelea na mazoezi sisi tunabangaiza, wenzetu
wana ufadhili wa makampuni ya vifaa kama Adidas, Nike, Puma nk.

2. Abdulrahaman Simai-JUDO.
a. Vyama vya Michezo havina Ofisi.
b. Kila chama cha Michezo kuwa na ofisi.
c. “Motivation”.

3. Alphonce Felix-RT
a. Kuwepo Kambi endelevu.
b. Upimaji wa afya.

4. Neema -MPIRA WA MEZA.
a. Mavazi upande wangu (size) hasa kwa wale wenye maumbile madogo, hatutendewi haki.
b. Kuwepo na Vazi la Taifa – vitenge viko vingi Kariakoo.

5. Yahya-MPIRA WA MEZA.
a. Maandalizi ya wasiwasi.
b. Wachezaji hawana uhakika wa kuwemo katika Timu.
c. Watu wanafanya mazoezi kwa muda mrefu halafu hawaendi safari.

D. VIONGOZI WA TOC
1. Suleiman Jabir-TOC.
a. Taifa lazima litambue kuwa Maendeleo ya Michezo hayaji kiurahisi na ni gharama.
b. Mawasiliano kati ya TOC na Vyama vya Michezo imekuwa tatizo kubwa. Kamati ya Olimpiki Tanzania kama mratibu wa Michezo ya Afrika, Jumuiya ya Madola na Olimpiki imekuwa na ushirikiano duni wa mawasiliano hasa pale inapohitaji taarifa muhimu za wachezaji kutoka Vyama vya Michezo.
c. Maendeleo hayo ni katika maeneo matatu:- i) Michezo ngazi ya chini (Grassroots Development, ii) Michezo kwa Wote(Sport for All) na
iii) Michezo kiwango cha juu cha ushindani (High Performance Elite Sport).
d. Ni lazima kuwe na Sera na Program zinazotambulika na kupewa nafasi maalum kwa upande wa Serikali, Vyama vya Michezo, TOC na wahusika wote.
e. OS/TOC -“High Performance Centers”; alizungumzia na kuvitaarifu Vyama vya Michezo juu ya “Olympic Solidarity Scholarship Programs”.
f. Kuwepo kwa ushirikiano mzuri na wenye kuleta ufanisi baina Wizara inayoshughulikia Michezo na Wizara inayoshughulikia Elimu kwa lengo la kuinuwa Michezo na kuibuwa vipaji mashuleni.
g. Wakati umefika kwa Tanzania kutambua kuwa, kuna haja kubwa sana ya kuweka mbele utaalamu na kutekeleza mambo vile inavyotakiwa ambapo kila muhusika na kila mtu kwa nafasi yake na uwezo wake, atekeleze jukumu lake ipasavyo.
h. Ni muda mrefu tumekuwa tukielezwa kuwa Wizara inayoshughulikia Michezo Bara imekuwa inaandaa “National Sports Policy”, Jee imefikia wapi?

HITIMISHO
Baada ya kusikiliza na kujifunza kutoka kwa Wanamichezo, Mheshimiwa Membe aliwahakikishia Wanamichezo na Vyama vyao kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga vyema kuwaendeleza Wanamichezo kwa kutumia nyezo ilizonazo. Vilevile, Serikali itaangalia uwezakano wa kuzungumza na Watanzania wenye Vituo vya kuendeleza Michezo kama kile cha “Filbert Bayi Sports Complex” na vIngine kwa kuwaandaa wanamichezo kwa Kambi za muda mrefu hasa kwa Matayarisho ya ndani na baadaye ndio kuwapeleka nje ya nchi kwa Matayarisho ya muda mfupi kwa nia ya kupata uzoefu halisi wa kimashindano “Competition exposure”.
Lengo ni kupata Wanamichezo wa kuiwakilisha nchi katika Michuano ya Kimataifa na kuieletea sifa na Medali za ushindi nchi yetu.

Naye Rais wa TOC Ndugu Gulam Rashid, alisisitiza umuhimu wa Wanamichezo kufikia viwango vilivyowekwa ili waweze kuteuliwa na kujumuishwa katika Timu ya Tanzania. Viwango ndio hutupa dira ya uwezo wa Wanamichezo na kuweza kukadiria matokeo hata kabla ya Mashindano yenyewe. Kambi ya TOC sio ya Maandalizi na wala si ya Kujiandaa bali ni Wachezaji na Viongozi wa Timu ya Tanzania kuwa pamoja, kuelewana, kuzoeana na kujitayarisha pamoja kama nchi.

Hali kadhalika, alivikumbusha Vyama kuwa wao ndio wenye jukumu la kuendeleza michezo kwa kuweka Malengo, Mipango, Mipango Mikakati. Vile vile alisisitiza kuwa Vyama vina jukumu la kuandaa mashindano yao katika ngazi mbalimbali kwa lengo la kuibua, kuviendeleza na kuvilea vipaji na kuwaendeleza Wanamichezo hao. Mwisho, alivishauri vyama kushiriki Michuano mbalimbali ya Kimataifa kwa lengo la wanamichezo hao kuonekana na hata kuweza kujumuishwa katika Mipango ya Olimpiki Solidariti badala ya kusubiria kushiriki katika Michezo inayoratibiwa na TOC tu.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

72 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Wachezaji Ivory Coast wapata mamilioni, nyumba

Sherwood bosi mpya Aston Villa