Tarryn Allarakhia apewa mitano tena Taifa Stars
UAMUZI wa kocha wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania maarufu kama Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ kumwingiza dimbani winga Tarryn Allarakhia unaweza kuwa bora zaidi kwenye mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya majirani zetu Zambia huenda ukawa ndiyo bora zaidi kwenye mchezo huo. Uamuzi wa pili ulikuwa kumwingiza dimbani kiungo mkabaji Novatus Miroshi ambao waliinua kiwango cha Taifa Stars kwenye mchezo huo. Winga Tarryn Allarakhia anachezea katika kloabu ya Rochdale AFC ya hapa Uingereza. TANZANIASPORTS inachambua kwa kina juu ya uchezaji wa kiungo huyo ambaye amekuwa kivutio katika mchezo dhidi ya Zambia.
Stamina za kiafrika
Akizungumzia ubora wa winga Tarryn Allarakhia, mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Athuman Machupa alisema nyota huyo anahitaji nguvu na kutengenezwa zaidi kwa utimamu wa mwili. “Ni mchezaji mzuri sana ambaye anahitaji stamina ya kiafrika, akifanikiwa hilo ni mali nzuri kwa nchi,” amesema Athuman Machupa.
Moja ya mambo yaliyompa sifa winga huyo ni kutambulika kuwa anao uwezo mzuri wa kucheza soka na miguu yake pamoja na akili viliongea kwa vitendo. Clacence Kunambi, mwandishi wa habari za michezo na mhariri mwandamizi ameonga mkono hoja ya Athuman Machupa kwamba kitaalamu winga Tarryn ameonesha ubora ambao unahitaji kuimarishwa kwa kiasi kidogo ili aongezeke uwezo. Winga huyo amezungumziwa vyema na wataalamu hawa wawili na kuamsha mjadala zaidi kuhusiana na uwezo wake.
Mfumo unaomfaa
Katika mfumo wa 4-4-2 unaopendwa na kocha Hemed Suleiman unalazimika mawinga kurudi eneo la mabeki wa pembeni kusaidia ulinzi, lakini wanakosa uhuru pale timu inapotaka kumiliki mpira zaidi. Katika mfumo wa 5-3-2 unampa nafasi winga huyu pale ambapo anakuwa na viungo wenzake wawili ili kuipeleka moto kwa timu pinzani. Kwenye mfumo huu anaonekana kucheza kwa malekezo zaidi na anakosa ule uhuru ambao anaweza kusababisha madhara zaidi. Kwa kutumia mfumo huo huo 5-3-2 anaweza kucheza kama mshambuliaji wa pili yaani nambari 10 (akiwa nyuma ya namba 9). Winga huyu anaonekana akipata ujuzi kidogo anaweza kusimama vema katika nafasi ya 10 kwa sababu ya kasi na wepesi wake kukimbia kuelekea lango la adui. Si kukimbia tu, bali kushambulia na kuleta madhara. Majaribio yake mara kadhaa yalisababisha faulo nyingi kufanywa na mabeki wa Zambia. Bahati mbaya nyuma yake (kiungo cha ulinzi) hakukuwa na uhakika wa kulindwa sababu viungo wwote muhimu Novatus Miroshi na Yusuf Kagoma hawakuwa dimbani.
Wepesi na kasi
Tarryn Allarakhia anaonekana kuwa mwepesi na kucheza kwa kasi kila wakati alipopata pasi. Ni winga ambaye anaingia eneo la hatari pasipo kuhofia wala kutegemea kupiga krosi. Huyu ni winga ambaye anatumia kasi yake na wepesi kuliandamana lango la adui akiwa na lengo la kujipatia faulo au kusababisha madhara kwa timu pinzani.
Mpira wa malengo
Sifa nyingine ambayo imeonekana kwa winga huyo ni kucheza kwa malengo. Kila alipokea pasi akiwa nje kidogo ya eneo la katikati ya uwanja kwenda kushoto kisha ndani alikuwa na jukumu la kutafuta matokeo. Kumiliki mpira pekee hakutoshi badala yake alikuwa naonekana bayana kucheza tofauti na sehemu kubwa ya kikosi cha Taifa Stars, kwani malengo yalionesha shauku yake ya kushinda. Akiwa mmoja wa viungo watatu waliotakiwa kusimama kwenye mstari wa katikati ya dimba-kushoto alikuwa na jukumua la kuzuia na kuwasukuma wapinzani kurudi katika eneo lao. Mpira wa malengo una maana kubwa katika mchezo, mchezaji anategemewa kuwa na uamuzi unaolenga kuifanya timu icheze kwa kufanya kitu cha ziada ili kuibuka na ushindi. Tarryn ameonesha anataka kuingiza malengo na mkakati maalumu wa mchezaji binafsi katika kusaidia timu. Katika eneo hili winga huyu kwenye mchezo huo hakuwa na mpinzani.
Utunzaji wa mali
Kwenye mchezo wa soka kuna msemo wa ‘kutunza mali’. Msemo huo unamaanisha uwezo wa mchezaji kumiliki mpira au kutunza mpira pale ambapo inahitajika. Kwenye eneo hili Tarryn Allarakhia alikuwa bora zaidi kwenye utunzaji wa mpira na kuipa uhai safu ya ushambuliaji a Taifa Stars. Tangu kuingia nyota huyu alionekana kutamani kufanya vitu adimu lakini sifa ya kuwa na uwezo wa kumiliki mpira na kuisaidia timu kusonga mbele ni sifa inayompa nafasi ya mitano tena.
Kukubalika kwa mashabiki
Tarryn amekuwa gumzo kwa mashabiki wa mpira nchini Tanzania. Wengi wanaona winga huyu ndiye aliamsha uhai wa Taifa Stars katika mchezo huo. Wakizungumza na TANZANIASPORTS wamesema Tarryn ni nyota ambaye anatakiwa kupangwa mara kwa mara, ili kuelewana na wenzake kwa sababu anao uwezo mzuri. “Huyu mzungu Tarryn anawe anapangwa mara kwa mara. Ana kitu kizuri. Ni mtu na nusu, zile gusa achia, kimbio, chenga na kasi ni nzuri sana.” amesema shabiki mmoja. Mwingine naye ameongeza kwa kusema, “Huyu mzungu anaitwa nani, awe anaitwa mara kwa mara. Anacheza mpira wa maana sana na hesabu zake unaziona kabisa, anafaa sana,”
Matakwa ya kocha
Baada ya kuachwa mara kwa mara, lakini benchi la ufundi kwa sasa liliamua kumwita kwa ajili ya michezo ya kufuzu. Ni dhahiri baada ya kuona uwezo wake unavyoongezeka ni wazi anatakiwa kuwa sehemu ya kikosi hicho kwa mechi nyingi. Ni jukumu la kocha Hemed Suleiman kuamua mwelekeo, lakini Tarryn ni miongoni mwa wachezaji wazuri wenye kuongeza maarifa katika kikosi cha Taifa Stars pale kinapohitaji maarifa ya ziada binafsi na kiufundi.


Comments
Loading…