*Kenya waibana Nigeria, Ivory Coast wapaa
*Bafana, Burkinafaso, Ethiopia nao wachanja
*Cameroon, Malawi, Ghana safi, Zambia mh…
Taifa Stars wameipandisha chati Tanzania, kwa kuwa gumzo baada ya kuwafunga Morocco kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2014.
Wakicheza nyumbani mbele ya maelfu ya washabiki wao, Stars waliwaaibisha Simba wa Milima ya Atlas kwa kuwakandika mabao 3-1.
Morocco wanapigania kufuzu kucheza kombe hilo mwakani nchini Brazil kwa mara ya kwanza tangu 1998, lakini ndoto zao zilitibuliwa na wanandinga wanaopiga soka ya kulipwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
AlikuwaThomas Ulimwengu aliyefunga bao la kwanza muda mfupi kabla ya mapumziko, kisha Mbwana Samatta wa TP Mazembe pia akafunga mabao mawili dakika ya 67 na 80 ya mchezo uliopigwa Dar es Salaam.
Morocco hawakuamini matokeo hayo, kwani yamefifisha ndoto zao kurejea kilinge cha dunia, ambapo mshambuliaji wao anayekipiga Granada ya Hispania, Youssef El-Arabi alifunga bao la kufutia machozi dakika za majeruhi.
Kwa ushindi huo, Tanzania wanapanda hadi nafasi ya pili ya kundi ‘C’ wakiwa na pointi sita, wakati Morocco ni wa tatu kwa pointi zao mbili, huku wakibakisha mechi tatu.
Ivory Coast ndio wanaoongoza kundi hilo, na hawakujutia kumtosa nahodha wao, Didier Drogba, kwani walipata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Gambia.
Kocha Sabri Lamouchi wa Ivory Coast alitamba kwa kikosi chake, ambapo mabao yalifungwa na Wilfried Bony, Yaya Toure na Salomon Kalou.
Ivory Coast wanaongoza kundi lao la ‘C’ kwa pointi nne, na wanakaribia kabisa moja ya nafasi tano zilizotengwa kwa ajili ya bara la Afrika nchini Brazil mwakani.
Mabingwa wa Afrika, Nigeria wameambulia pointi moja baada ya kutoka sare na Kenya.
Hii ilikuwa mechi ya kwanza ya Nigeria tangu walipotwaa ubingwa kwa kuwafunga Burkina Faso, ambapo hadi dakika ya 93 walishalala kwa bao moja lililofungwa na Francis Kahata, katika mtiti uliopigwa Calabar.
Hata hivyo, alikuwa Nnamdi Oduamadi aliyetokea benchi na kuwafundisha jinsi ya kufunga nyota wengine wa kimataifa ambao hawakung’ara dimbani, Obafemi Martins, Sunday Mba na Victor Moses.
Kwa sare hiyo, Nigeria wamewaacha Malawi waungane nao kuongoza kundi lao, kwani waliwashinda Namibia kwenye mechi nyingine wikiendi hii.
Katika mechi ya Malawi dhidi ya Namibia, Frank Mhango ndiye aliwapatia Wanyasa bao pekee, huku wakiwa bila kocha wao wa muda, aliyelazimika kwenda kumzika mwanawe aliyefariki dunia kwa saratani.
Namibia wana pointi tatu kutokana na mechi tatu kwenye kundi lao la ‘F’ na Kenya wanashika mkia wakiwa na pointi mbili tu.
Nyota mwingine wa soka ya Afrika, Samuel Eto’o alirejea kuwatumikia Cameroon, akafunga mabao mawili walipowashinda Togo 2-1.
Ushindi huo unatoa mwanya kiasi fulani kwa Cameroon kufuzu kushiriki mashindano makubwa kwa mara ya kwanza tangu 2010.
Dove Wome alisawazisha moja ya mabao ya Eto’o, lakini nyota huyo alirejesha tofauti ya bao. Togo haikuwa na nyota wake, Emmanuel Adebayor, golikipa Kossi Agassa na wengine kadhaa wanaoendesha uasi dhidi ya kocha wao, Didier Six, timu yao ikishika mkia kwa pointi moja.
Afrika Kusini waliokuwa wenyeji wa mwisho wa Kombe la Dunia, wamerejesha matumaini ya kushiriki mwakani, baada ya kuwafunga Jamhuri ya Afrika ya Kati 2-0 jijini Cape Town, kwa mabao ya Thabo Matlaba na Bernard Parker. Bafana waliongoza kundi ‘A’ kwa muda kabla ya Ethiopia kuwaondosha hapo Jumapili hii.
Wahabeshi wameonesha dhamira ya kurejea kwenye soka ya kimataifa, baada ya kuwakung’uta Botswana 1-0, wakafikisha pointi saba na kushika usukani wa kundi hilo kwa tofauti ya mbili.
Tunisia walijihakikishia udhibiti wa kundi ‘B’ baada ya kuwafunga wanaoshika nafasi ya pili, Sierra Leone kwa mabao 2-1 mjini Rades.
Burkina Faso waliomaliza nafasi ya pili katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu, waliwananga Niger 4-0 katika mtiti wa kundi ‘E’ uliopigwa jijini Ouagadougou.
Vinara wa kundi hilo, Congo Brazzaville walifikisha ushindi wa tatu katika mechi tatu, baada ya kuwabandua Gabon 1-0 jijini.
Beki wa Queen Park Rangers (QPR), Christopher Samba ndiye alifunga bao hilo, akitafuta sasa kucheza Kombe la Dunia mwakani, hata kama QPR inayoshika mkia Ligi Kuu ya England (EPL) itashuka daraja.
Senegal walitoka sare na Angola, hivyo kuwaweka pointi mbili mbele ya Waangola hao katika kundi ‘J’ jijini Conakry, mechi ilikochezwa kwa vile uwanja wa Leopold Senghor wa Dakar, Senegal umefungiwa kwa mwaka mmoja kutokana na fujo za mwaka jana. Senegal wanaongoza kundi lao kwa pointi tano.
Lesotho waliwashangaza mabingwa wa zamani wa Afrika, Zambia, kwa kutoshana nao nguvu dimbani.
Zambia walicheza kipindi cha pili wakiwa 10, baada ya golikipa wao, Kennedy Mweene kulambwa kadi nyekundu.
Walikuwa wakiongoza hadi dakika ya 89, Lesotho waliposawazisha. Kocha wa Zambia, Herve Renard ameonya kwamba wanaweza kujutia pointi mbili walizopoteza.
Zambia, hata hivyo, wanaongoza kundi ‘D’ kwa tofauti ya pointi moja, baada ya matokeo ya Jumapili hii, ambapo Ghana waliwachapa Sudan 4-0.
Kundi la washindi 10 kutoka makundi haya ya awali, litaingia kwenye raundi ya mwisho kwa kucheza mechi mbili, nyumbani na ugenini ili kupata watakaokwenda Brazil mwakani.
Comments
Loading…