KIJANA Mtanzania mwenye ulemavu wa miguu, Zaharan Mwenemti ni mmoja wa Watanzania watano watakoiwakilisha nchi katika michuano ya Olimpiki itakayofanyika nchini Uingereza mwishoni mwa Julai , mwaka huu.
Mwenemti ambaye kwa sasa anajifua kwa udi atacheza michezo mitatu ambayo ni kurusha tufe, kurusha kisahani na kutupa mkuki.
Mbali ya mchezaji huyo mahiri, pia wapo vijana wapya wane wanaotegemewa kupata medali kwa masuala ya riadha na kuogelea.
Mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi ameviambia vyombo vya habari kwamba ana uhakika vijana wa riadha watatwaa medali kwenye michuano hiyo itakayotimua vumbi nchini Uingereza.
Matumaini ni makubwa, vijana wanaendelea kujifua vizuri hususan wa riadha’’ alisema alipowazungumzia wanariadha waliopiga kambi katika Mji wa Kibaha kilometa karibu 50 kutoka Jiji la Dar es Salaam.
Wanariadha tegemeo ni Samson Ramadhani ambaye anajifua kwa kufukuza upepo katika umbali wa mita 5,000 pamoja na Fustine Mussa na Musendeki Mohamed anayetarajiwa kupata medali ya kuongelea.
Bayi ambaye aling’ara katika riadha mwaka 1980 kwa mbio za mita 3,000 aliwahakikishia waandishi kwamba anayo imani kubwa na wanamichezo wake wanaokwenda kwenye olimpiki.
Kwa upande wa ngumi kijana pekee ni Seleman Kindunda ambaye anajifua usiku na mchana kujiandaa na michuano hiyo.
Comments
Loading…