Unapoanza kuelezea mchezo wa kikapu duniani basi mawazo ya wengi yatahamia nchini Marekani katika ligi ya ‘NBA’ hii inatokana na ubora wakiwa wameupa kipaumbele sana mchezo huo.
Kumbe inawezekana endapo ukiweka kipaumbele kile ukipendacho na kinaweza kuwa kikubwa na kila mmoja akaona ukubwa wa mchezo ule nchini humo huku wanamichezo matajiri zaidi wanatoka NBA.
Dunia inaishangaa Marekani kwa mapenzi mazito ya mpira wa kikapu ikiutupa kando mchezo pendwa wa mpira wa miguu, nchi hiyo ndio mchezo unaotazamwa zaidi yaani huwezi kuufanisha mchezo huo na mpira wa miguu kama ulivyo kwa nchi nyingi duniani.
Lakini pia maslahi yake kwa wanaocheza mchezo huo ni makubwa mno ndio maana kila mara inapotangazwa orodha ya wanamichezo tajiri duniani huwezi kukosa kuwaona wachezaji wa NBA, uwekezaji mzuri pamoja na kupenda kile mtu unachoamini.
Hata wewe uliye na ndoto yako ya kufika mahali fulani kwa tasinia au biashara ukichukua mfano huu wa NBA unaweza kufika na ukapata mafanikio kwa unachokiamini.
Hebu geuza shilingi rudi Afrika hasa Tanzania, mchezo wa kikapu hauchukuliwi kama ni moja ya michezo bora kabisa ndio maana zimetoka kauli nyingi baada ya kusimamishwa kwa michezo mbalimbali kupisha janga la Korona na baadae kutolewa kauli za kurejeshwa wakati huo Waziri wa michezo akasema michezo mingine isubiri kila mmoja alikuwa na mawazo yake juu ya hilo.
Tovuti hii imemtafuta Mwalimu wa Mpira wa Kikapu Tanzania Bahati Mgunda kuelezea maendeleo ya mchezo huo ambapo yeye anasimamia watoto walio chini ya miaka 18 katika kituo cha JKM Park jijini Dar es Salaam.
Mgunda ameweka wazi kuwa mchezo huo unaendelea kukua kwa kasi ukilinganisha na hapo zamani ambapo tatizo kubwa linatokana na uongozi pamoja na hamasa mbalimbali maswala hayo yakiwekwa sawa huenda wakafika pale wanapotazamia.
Amefurahishwa na kauli ya Rais Magufuli juu ya kufungua michezo yote na ikiachwa kando kauli za kusubiri kwa michezo mingine.
Alipoulizwa juu ya Kikapu ya Tanzania kutokuwa na mvuto Mgunda amesema kuwa mpira wa miguu una watu wengi kwa hapa Tanzania ila alikuwa na hamu ya kujua kwanini ilitolewa kauli juu ya michezo mingine kuwekwa kando kwanza.
“Ni kweli Mpira wa miguu una watu wengi, viongozi wa serikali pamoja na kundi kubwa kupenda mpira wa miguu ila bado nilikuwa na hamu ya kujua kwanini ilitolewa kauli ile,” alisema.
Alichoshangazwa yeye michezo mingine inakutanisha makundi madogo ya watu kuliko mpira wa miguu ambao una mashabiki wengi sasa kwanini hii mingine iachwe kando mchezo ambao na huu mwingine urudi.
Ili kikapu iweze kupendwa na kuvutia watu Mgunda ameweka wazi kuwa mabadiliko yanaanzia kwao wenyewe viongozi baada ya hapo serikali ndio waweke mpango wao huku wakiangazia macho yao shule za msingi ili waweze kupata watu sahihi.
“Serikali waangalie zaidi sehemu ya uzalishaji wa wawchezaji huko shule za msingi yaani vijana wadogo ili tupate wakiwa katika hali nzuri, iandae mipango yakinifu ya kuwaweka sawa watoto hao wataweza kuleta mabadiliko,”alisema.
Mgunda ambaye ni mlezi wa watoto katika kituo cha JKM Park ana watoto zaidi ya 1300 ambao wanacheza hapo, huku akisema kuwa wanashirikiana na NBA kwa karibu sana katika kuunganisha au kutafuta fursa mbalimbali kwa watoto hao.
Kuthibitisha NBA wanaungana nao Mgunda amesema kuwa huwa wanatoa kozi mbalimbali katika nchi tofauti nchini Afrika ambapo ofisi zao zipo huko Afrika Kusini kwa bara la Afrika.
Muelekeo wa Kikapu wa Tanzania kwa kiasi unasonga mbele kutokana na jitihada za watu wachache wanaojitoa ili kupeperusha vizuri bendera ya nchi kupitia mchezo huo.
Kwa miaka ya hivi karibuni mfano mzuri umeonekana kwa Mtanzania Hasheem Thabeet ambaye alifika kucheza katika ligi ya Marekani ya mpira wa kikapu.
Naungana na Mgunda juu ya maoni yake bado wadau pia wanatakiwa wauangazie mchezo huu kwa namna nyingine kwani faida yake kubwa mno endapo watapatikana watu wengi zaidi wa kuwakilisha taifa.
Mifarakano mbalimbali baina ya viongozi wa vyama husika nayo ni tatizo kubwa, katiba na kanuni za chama cha mpira wa kikapu ziweze kubadilishwa juu ya mtu mmoja kuwa na nafasi nyingi zaidi.
Mfano rais wa Shirikisho la mchezo wa kikapu yeye pia ndio msemaji mkuu nabado kazi nyingine anazifanya yeye badala ya kuwa na wasaidizi ili kufanikisha vizuri.
Kwa Tanzania mchezo huo mtu akiupenda basi itakuwa ameupenda kutoka moyoni tofauti na mingine ambayo mifano yake halisi inaonekana, mfano soka kila mmoja angependa kucheza mpira wa miguu kutokana na mafanikio yaliyo wazi.
Upande mwingine wa waandishi wa habari huku nako tunatakiwa kusimama kibwebwe kutangaza michezo yote kama inavyofanywa katika mpira wa miguu, inaweza ikawa sababu ya wadau wengi kuielewa michezo mingine ambayo ipo na ina watu wanaohitaji kuipeleka mbele.
Kwa wapiga kura na wadau waliona uwezo wa kufanya hivyo inapotokea fursa hizo wajitokeze na kufanya maamuzi yaliyokuwa na faida ndani yake ili kuleta mabadiliko ya kweli, kama alivyosema Mgunda lazima harakati zianzie kwa viongozi kisha serikali ije kuweka misingi imara.
Tanzania imekuwa moja ya nchi zinazoandaa michuano hiyo mara kwa mara huku baadhi ya taasisi zikiwa na mipango mbalimbali, wachukue hii katika kusoma mazingira ili safari ianzie hapo, mwaka 2018 iliandaa michuano ya kanda tano ya Afrika kwa mchezo huo lakini imendelea hivyo kwa miaka kadhaa hii iwe sababu ya kitovu cha kuinua mchezo huo na kupata mafanikio zaidi.
Kazi ya viongozi kutafuta miundombinu itakayoiwezesha kusimamia vizuri ligi pamoja na mambo mengine ya wasimamizi.
Yote haya yakitazamwa kwa jicho la mwewe huenda ufumbuzi ukapatikana wakati mambo mengine ya msingi na utaratibu sahihi wa kuandaa vijana kutoka shue za msingi pamoja na vyuo, huwezi kutenganisah misingi na utaratibu ulio sahihi.
Comments
Loading…