in , ,

Taifa Stars, Je ni Umimi dhidi ya Uzalendo…..

Taifa Stars

BAADA ya Tanzania kufungwa nyumbani 0-1 na Uganda katika mechi ya kwanza ya kuwania nafasi ya kushiriki fainali za mashindano ya Afrika ya wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani (CHAN) nchini Afrika Kusini mwakani, mijadala mingi mirefu imekuwa ikijitokeza kwenye mitandao ya kijamii ambapo Watanzania wameandika mengi kuhusu kipigo hicho. Kuna la viongozi wa TFF kutoipa uzito mechi hiyo, kuna hoja za kujiamini kupita kiasi na kuidharau Uganda baada ya Tanzania kujiona sasa ni ya hadhi ya kupambana na kina Cameroon, Ivory Coast, Morocco na wengine wa hadhi hizo na lipo la kucheza chini ya kiwango. Kuna wataalam wa soka wameeleza kwamba Tanzania ilikuwa ikielekea lango la Uganda bila malengo rasmi ya tunakusudia kufanya nini kivipi wakati Uganda walikuwa na mpango huo ambapo licha ya kutushambulia mara chache wangeweza kutufunga hata 3-0.

Ukikusanya maoni yote hayo utapata jibu moja kwamba Watanzania tuliathirika na kukosa uzalendo. Kama kweli TFF waliipuuza mechi hiyo tafsiri yake ni kukosa uzalendo. Unaidharau, timu fulani na kucheza bila kujituma kwa sababu hujali kufungwa na hujali kufungwa kwa sababu huna upendo mkubwa wa nchi yako. Ukweli ni kwamba wachezaji wetu wengi wa timu ya taifa wanazipenda mno Yanga na Simba– bila kujali wanachezea timu gani nchini- kuliko wanavyoipenda timu ya taifa. Wa Yanga na Simba huonesha majonzi makubwa wanapofungwa wakichezea timu za klabu zao lakini wachezaji hao hao huwa hawaoneshi majonzi yoyote wanapofungwa wakiwa timu ya taifa.

Watafungwa na Uganda kwenye fainali za Challenge Cup jijini Dar es Salaam, kwao sawa tu kwa sababu iliyofungwa si Yanga wala Simba! Watafungwa na Uganda kwenye fainali za Challenge Cup Uganda, sawa tu, ili mradi ushindi kwa Yanga au Simba baadaye utakuwepo. Wafungwe na yeyote na wapoteze nafasi muhimu ya kuendelea na mashindano, humuoni mchezaji wa timu ya taifa kalala uwanjani, hana nguvu kwa majonzi kama tunavyowaona wa nchi nyingine wenye uzalendo kwa nchi zao.

Enzi tulipokuwa na uzalendo, walilia kina Kitwana Manara kule Zambia kwenye Challenge Cup mwaka 1975 si tu kwa Kitwana kupigwa akichangiwa na wachezaji wa Kenya enzi zile za maisha ya kishenzi mpirani bali walilia kutolewa na Kenya mashindanoni.Walilia sana kina Mohammed Kajole aliyeanzia kuchezea timu ya taifa kwa mara ya kwanza kwenye mashindano hayo akiitwa kujiunga na wenzake waliotangulia Zambia. Walilia sana kwa sababu walilipenda sana taifa lao.

Mwaka huo huo wachezaji wetu wa timu ya taifa walilia sana jijini Khartoum Sudan baada ya Sunday Manara kuoneshwa kadi nyekundu ya maonezi dakika za mwanzo mwanzo za mchezo kwa sababu Wasudan walimuogopa kutokana na alivyowafanya vibaya kwenye mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam. Walilia sana kwa uchungu wa nchi yao. Miaka miwili kabla, yaani 1973, kina Zimbwe, Haidar Abeid Muchacho na wengine walilia mno nchini Mauritius walipotolewa kwa penalti tano tano.Walilipenda taifa lao kwa dhati na kwa hiyo walilililia. Leo hii kila kitu ni sawa tu. Ushinde, utoe sare, ufungwe poa tu.

Tatizo linalotukabili Tanzania baada ya uzalendo kupotea ni tatizo la umimi. Utalijuaje? Muulize mchezaji wa nchi yenye uzalendo kuhusu mechi ya timu yake ya taifa na timu nyingine atakwambia; “tutapambana kwa nguvu zote kuipatia ushindi timu yetu ili kuipa sifa nchi yetu na kuwapa furaha wananchi wenzetu. Hatutaki kuiangusha nchi yetu”. Swali hilo hilo mchezaji wetu atajibu; “nitapambana kwa nguvu zote kuipa ushindi timu yetu kwa sababu naona hii ndiyo nafasi yangu ya kujitangaza kimataifa ili nipate soko la nje”. Unaona hapo tofauti ya uzalendo na umimi?

Ukishakuwa na timu za mitazamo hiyo miwili tofauti, tegemea timu moja itakuwa ya wachezaji watakaocheza kwa lengo moja la kuibeba nchi yao wakati wale wa timu nyingine watacheza soka ya kuonesha wanaweza mmoja mmoja kutafuta sifa binafsi na soko la kimataifa! Hiyo ndiyo hali iliyoikuta timu yetu.

Lakini tatizo la uzalendo duni si la Taifa Stars tu bali utalikuta kwenye nyanja zote za kimaisha na ndiyo maana shule zinakosa watoto wa kidato cha tano bila mtu yeyote kujali, wizi wa mali ya umma na rushwa iliyotamalaki vinashamiri kwa sababu hatuna uzalendo. Vitendo vya kigaidi vimejitokeza mara mbili kwa bomu kurushwa kati kati ya watanzania lakini mamlaka zinazohusika wala hazihangaiki kuufichua mtandao wa kigaidi na kuutokomeza, hatuna uzalendo. Kwa hiyo hili ni tatizo la kila eneo la utendaji Tanzania na si la uchezaji wa timu ya taifa tu.

Wakati mikakati mingine ya kufufua uzalendo ikipangwa, ni vizuri tuwe na mkakati maalum wa kuwapa darasa la kupenda nchi wachezaji wetu wa michezo yote wanapokuwa kwenye maandalizi ya kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa ili wajue kwamba wakati huo wao ni wawakilishi wa taifa na wala si wawakilishi wa matashi na malengo yao binafsi. Ni vizuri darasa hilo likianza tukijiandaa kurudiana na Uganda tunakohitaji ushindi wa 2-0 au ushindi wowote wa magoli ya kuwazidi tofauti ya goli angalau moja kama 2-1 ,3-2 ,4-3 na kadhalika.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Wenger kuongeza mkataba Arsenal

Usain Bolt atasalimika kashfa hizi?