Wakati natazama mechi ya Simba SC na Azam FC kitu pekee kilichokuwa kinazunguka kichwani kwangu ni ule muunganiko uliowahi kutokea Simba SC katika eneo la kiungo cha kati , muunganiko uliokuwa uunaundwa na James Kotei pamoja na Jonas Mkude.
Muunganiko huu ulikuwa kipindi cha kocha Patrick Aussems. Kwenye muunganiko huu wa James Kotei na Jonas Mkude kuna kitu kimoja ambacho kilikuwa kinawabeba sana Simba SC, kitu gani hicho?
James Kotei alikuwa na uwezo wa kukaba vizuri, kutibua mipango ya wapinzani wakati wanashambulia na kupokonya mipira kazi ambazo Jonas Mkude alikuwa anazifanya lakini siyo kwa ubora ambao James Kotei alikuwa anafanya.
Wakati James Kotei alivyokuwa anapokonya mipira mtu aliyekuwa anachukua jukumu la kuisambaza mipira kwenda mbele ni Jonas Mkude. James Kotei alikuwa na uwezo wa kusambaza mipira kwenda mbele lakini siyo kwa kiwango alichokuwa anakifanya Jonas Mkude.
Kwa hiyo viungo hawa wawili walikuwa wanajua kufichiana madhaifu yao. James Kotei alikuwa ni mzuri sana kwenye kupokonya mipira kuzidi Jonas Mkude. Jonas Mkude alikuwa mzuri sana kwenye kusambaza mipira kuzidi James Kotei.
Kitu cha pili ambacho Simba SC walikuwa wananufaika na viungo hawa wawili ni kupunguza uwazi kati ya eneo la kiungo cha kuzuia na kiungo cha kushambulia. Pili viungo wa kushambulia walikuwa huru zaidi kwenye eneo la mbele kwa sababu Jonas Mkude na James Kotei walikuwa wanahakikisha ulinzi mzuri eneo la nyuma.
Kwenye mechi ya jana dhidi ya Azam FC hasa kipindi cha pili kulikuwa na uwazi mkubwa sana kati ya Tadeo Lwanga aliyecheza kama kiungo wa kuzuia na Larry Bwalya aliyecheza kama kiungo wa kushambulia. Tadeo Lwanga alitakiwa kupokonya mipira na wakati huo huo kusambaza kwenda mbele.
Hakukuwepo na kiungo ambaye angemuunganisha Tadeo Lwanga na Larry Bwalya. Hapo ndipo wazo langu la James Kotei na Jonas Mkude lilipokuja wakati natazama mechi ile ya Simba SC na Azam FC.
Uwezekano wa Tadeo Lwanga na Jonas Kotei kucheza wote ni mkubwa na una faida kubwa kwa Simba SC. Tadeo Lwanga hana tabia ya kutamani kusogea mbele sana mara kwa mara hivyo ni sahihi kwake yeye kubaki katika eneo la ulinzi kwa ajili ya kupokonya mipira.
Jonas Mkude anaweza akawa anasambaza mipira kutoka eneo la nyuma na kwenda mbele. Pia hii itampa uhuru mkubwa Larry Bwalya ambaye katika eneo la mbele zaidi.
Larry Bwalya ni mchezaji anayependa kuchezea mpira na siyo kukaba sana. Unapompa viungo wawili wa kuzuia unampa uhuru zaidi wa yeye kusogea mbele kwa ajili ya kufanya ubunifu wenye faida kubwa kwa Simba SC.
Comments
Loading…