Manchester United wamepoteza mechi ya tatu mfululizo na kutia shinikizo kubwa kwa kocha David Moyes aliyemrithi Sir Alex Ferguson.
Safari hii Mashetani Wekundu wamefungwa na Sunderland wanaoburura mkia wa Ligi Kuu ya England (EPL), na ilikuwa kwenye mechi ya Kombe la Ligi (Capital One Cup).
Sunderland walifarijika kwa ushindi wa mabao 2-1 kutokana na mkongwe wa Man U Ryan Giggs kujifunga mwenyewe dakika ya 45, Nahodha Nemanja Vidic akasawazisha dakikaya 52 lakini Fabio Borini akapeleka simanzi United kwa bao la penati katika dakika ya 64.
Hii ni mara ya kwanza tangu 2001 kwa United kupoteza mechi tatu mfululizo na Moyes ameendeleza lawama zake kwa waamuzi, akisema penati waliyopewa Sunderland haikuwa halali.
Kadhalika ni mara ya kwanza kwa Sunderland kuwafunga United tangu mwaka 2000 katika mechi 21 baina yao. Borini anacheza Sunderland kwa mkopo kutoka Liverpool.
Timu mbili hizo zitarudiana Januari 22 baada ya United kuwa wameshatolewa kwenye Kombe la FA kwa kufungwa na Swansea na katika EPL wapo pointi 11 nyuma ya vinara Arsenal.
Comments
Loading…