in , , , ,

Suarez marufuku miezi minne

 

*Ametupwa nje ya Kombe la Dunia
*Alimwa faini ya kihistoria £65,680

 

Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) imemtia hatiani Luis Suarez wa Uruguay kwa kumng’ata bega Giorgio Chiellini wa Italia.

Kwa kosa hilo, Suarez (27) amepewa adhabu inayovunja rekodi ya zile zilizopita, ambapo ametupwa nje ya mechi za Kombe la Dunia kwani amezuiwa mechi tisa za kimataifa.

Kadhalika, mshambuliaji huyo wa Liverpool amezuiwa kujishughulisha kwa namna yoyote na masuala ya soka kwa miezi minne, ikimaanisha kwamba atakosa karibu mechi tisa za Ligi Kuu England (EPL) kama atabaki England.

Kana kwamba hiyo haitoshi, Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ya Fifa, Claudio Sulser alitangaza kwamba wanampiga Suarez faini ya pauni 65,680.

Suarez alimng’ata beki Chiellini katika mechi ya makundi baina ya timu zao, ambapo dakika moja baada ya kumng’ata Uruguay walipata bao pekee na kuwatoa nje ya fainali hizo Italia.

Suarez; nahodha wa Uruguay, Diego Lugano aliyepata kucheza England na kocha wao, Oscar Tabarez walikana Suarez kutenda kosa hilo baada ya mechi yao Jumanne iliyopita.

Tabarez alidai vyombo vya habari vya Uingereza vilikuwa vikitia chumvi na kuchochea suala hilo. Uruguay ndio waliwatoa England pia katika mechi ya pili tu ya michuano hii.
Hii ni mara ya tatu kwa Suarez kutiwa hatiani kwa kumng’ata mchezaji.

Alipigwa marufuku kucheza mechi 10 baada ya kumng’ata mkono Branislav Ivanovic mwishoni mwa msimu wa ligi wa 2012/2013 na mwaka 2010 aliadhibiwa kukosa mechi saba kwa kumng’ata Othman Bakkal wa PSV Eindhoven, enzi hizo Suarez akichezea Ajax Amsterdam.

Alikosa mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Uholanzi miaka minne iliyopita baada ya kupewa kadi nyekundu alipodaka mpira uliokuwa unaelekea langoni mwake na kuwanyima Ghana nafasi ya kuingia robo fainali.

Adhabu aliyopewa Suarez ni kubwa kuliko ile ya Mauro Tassotti wa Italia aliyopewa kwa kumpiga kiwiko na kumvunja pua Luis Enrique wa Hispania 1994.

Tassotti aliadhibiwa kukosa mechi nane kwa kumpiga mchezaji ambaye sasa ndiye kocha wa Barcelona.
Suarez amepata pia kuadhibiwa vikali kwa kutoa lugha ya matusi na kibaguzi dhidi ya Patrice Evra wa Manchester United.

Fifa wamesema matukio ya utovu wa nidhamu kama hilo hayawezi kuvumiliwa, hasa katika michuano ya Fifa ambapo mamilioni ya watu wanatazama michuano hii.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Liverpool, Ian Iyre, mara baada ya uamuzi huo alisema kwamba watatoa tamko baada ya kupata nakala ya uamuzi huo na kuupitia.

Liverpool, hata hivyo, hawazuii kumuuza Suarez kwa klabu nyingine ikiwa watapenda kuondokana naye. Akibaki Liverpool, huenda akarudi dimbani kwenye mzunguko wa tatu wa michuano ya Kombe la Capital One wiki inayoanza Oktoba 27 iwapo watakuwa wamefuzu awamu ya pili.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Ghana wawafukuza Boateng, Muntari

Algeria wavuka, Ghana nje