Kwa mara nyingine Timu ya Taifa ya Tanzania – Taifa Stars wamepoteza mechi muhimu na kuwatia simanzi wapenda soka nchini Tanzania.
Baada ya mfululizo wa kufungwa mechi kadhaa, ikiwa ni pamoja na zote kwenye michuano ya COSAFA nchini Afrika Kusini, wamepokea kichapo cha 3-0 kutoka kwa Misri.
Visingizio havikosekani kwa sababu ni kiasi cha kuviandaa, hasa hii ya Misri wale wanaozungumzia upande wa kuwatetea wachezaji na kocha Mart Nooij watasema Misri ni wagumu.
Nilimsikia Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi akisikitika jinsi wachezaji (anawaita vijana wake) walivyopata adha baada ya kuwasili Dar es Salaam.
Kabla ya hao wa Misri kuwasili, wengine waliobaki nyumbani walishambuliwa na basi lao kupasuliwa kioo. Hawa wa Misri naambiwa kuna waliokunjana na washabiki.
Malinzi anasema anasikitishwa na kebehi na masimango dhidi ya kikosi hicho. Sidhani kama ni sahihi kusema ni kebehi na masimango, naona kwamba ni mwitikio wa hali halisi iliyojitokeza.
Anataka kuwapo uvumilivu lakini ukweli ni kwamba kuna kitu kinatakiwa kufanywa kwa ajili ya kuhakikisha soka inarejea. Kuanguka kwa kiwango cha soka na nafasi ya Stars kunaenda kama shilingi inavyoanguka.
Kuna wadau wanaosema vijana walijitahidi Misri kwa vile hadi mapumziko mabao yalikuwa 0-0, lakini waelewe kwamba soka ni dakika 90 na nyongeza zake inapobidi.
Wasisahau kwamba Yanga katika mechi moja walishawafunga Simba mabao 3-0 mapema lakini kocha Abdallah Kibaden akazungumza na vijana wake wakati wa mapumziko na wakaja kurejesha mabao yote yale.
Yawezekana vijana hawana stamina au wanashindwa kujituma katika muda wote wa mchezo. Lakini pia labda tujiulize juu ya namna ya upangaji wa timu.
Je, bado kocha anaelekezwa na viongozi (watawala) wa soka juu ya nani apangwe na yupi asipangwe? Kuna sababu gani ya mfungaji bora na mchezaji bora wa Ligi Kuu 2014/15, Simon Msuva kuwekwa benchi hadi baadaye?
Mechi ile ilitanguliwa na za kirafiki na nyingine za COSAFA ambazo wachezaji walifanya vibaya. Kule Alexandria mabao yalifungwa kuanzia dakika ya 61 hadi ya 70. Stars walijilinda hadi saa nzima na wakapoteana nusu saa iliyobaki.
Kabla ya mechi kocha alisema vijana walikuwa wameiva na wenye ari kubwa ya ushindi walipokwenda Ethiopia kwa ajili ya mazoezi pale uwanja wa benki.
Hatukutarajia makubwa sana dhidi ya Misri, ikizingatiwa walitangulia kuchabangwa na Swaziland, Madagascar na na Lesotho.
Hata hivyo, ikumbukwe kwamba kikosi kiliimarishwa kwa kuongezwa wachezaji lakini muda ulikuwa muda mfupi hivyo huenda haingewezekana kuzoeana na kucheza vyema.
Nakumbuka kwenye mechi baada ya Yanga kutwaa ubingwa walipanga mabeki ambao hawakuwa wamecheza pamoja na walipoteza mechi zile.
Nooij aliyerithi mikoba ya Kim Poulsen mwaka jana ameshinda mechi tatu tu kati ya 17. Kama hali na mwelekeo ndio huu tusubiri kichapo hata kutoka kwa Chad na kibano zaidi kwa Nigeria.
Kwa nini hatua za haraka zisichukuliwe kurekebisha mambo haya? Pengine ni wakati wa kocha mzawa na benchi zima la ufundi la wazawa?
Wachezaji kwenye klabu zao wamefanya vyema, tatizo ni lipi wanapokuwa Taifa Stars? Nakumbuka Yanga walivyopambana kiume dhidi ya Etoile Du Sahel wa Tunisia lakini wakiingia Taifa hovyo.
Nadir Haroub na Amri Kiemba ndio walioweza kuzungumza na waandishi wa habari wakati wachezaji wengine walikuwa wakilia na timu kusambaratika uwanja wa ndege waliporejea.
Ni wakati wa TFF na wadau wa soka kuangalia hatua za kuchukua, maana tukikosa tena AFCON 2017 itakuwa pigo kwa washabiki wa soka ambao wangependa kuona timu ikisonga mbele.
Tunakumbuka sana enzi za Marcio Maximo alipopandisha soka yetu sana.