*Sare ya Chelsea yawaacha Arsenal juu
Wakati njia ikisafishwa kwa Manchester United kuvikwa taji la ubingwa wa England, changamoto inazidi kuwa kubwa kwa nafasi ya tatu na ya nne.
Kipigo cha mabao 3-1 walichokubali Manchester City kimewanyong’onyeza, hivyo kutegemea nafasi ya pili kwa tofauti kubwa ya pointi.
Vijana hao wa Roberto Mancini walikubali kichapo kutoka kwa Tottenham Hotspurs waliotoka mapumziko ya siku 10.
Ushindi huo unatoa matumaini makubwa kwa Spurs kuingia nne bora na kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwani wamefikisha pointi 61 wakiwa nafasi ya tano.
Chelsea waliotoka sare ya mabao 2-2 na Liverpool wapo nafasi ya nne baada ya kufikisha pointi 62, zikiwa ni moja pungufu ya Arsenal walio nafasi ya tatu.
Hata hivyo, Chelsea na Spurs wana mchezo mmoja mkononi, hivyo wakishinda mechi yao moja ya ziada watakuwa juu ya Arsenal, japokuwa bado ushindani utabaki mkali kuelekea mwisho wa EPL.
Man City walijisahau kipindi cha pili, baada ya kumaliza kile cha kwanza wakiongoza na bao moja ugenini, tena likifungwa mapema dakika ya tano kupitia kwa Samir Nasri.
Kipindi cha pili hali ya hewa iliwachafukia mabingwa hao watetezi walioonekana kuchoka, ambapo Andre Villas-Boas alijivunia mabao ya Clint Dempsey aliyesawazisha, Jermain Defoe aliyewafunika na Gareth Bale aliyewaaibisha City. City sasa wameachwa pointi 13 na United.
Katika mechi ya Liverpool na Chelsea, vuta nikuvute haikuwa ya kawaida, Chelsea wakiongoza kufunga kupitia Oscar kabla ya mchezaji wa zamani wa Chelsea, Daniel Sturridge kusawazisha kutokana na pasi ya Luis Suarez.
Hata hivyo, Suarez alisababisha penati iliyofungwa na Eden Hazard. Suarez alishika katika jitihada za kuokoa, lakini ni mchezaji huyo wa kimataifa wa Uruguay aliyeokoa pointi kwa kupachika bao katika dakika za majeruhi.
Sare hiyo inawaweka Liverpool katika nafasi ya saba wakiwa na pointi 51, nyuma ya Everton wenye pointi 56 na mbele ya West Bromwich Albion wenye pointi 45.
Nafasi ya 10 wapo West Ham United kwa pointi zao 42 wakati ya 11 ni Fulham, wakifuatiwa na Southampton, Norwich, Sunderland, Stoke City na Newcastle.
Wanaozibeba timu hizo 16 ni Aston Villa ambao wakijitahidi wataepuka kikombe cha kushuka daraja, wakati walio pabaya ni Wigan, Queen Park Rangers na Reading.
Comments
Loading…