Tangu Machi mwaka huu ulimwengu wa soka umekuwa tofauti, kutokana na kusitishwa kwa mechi za mchezo huo unaopendwa zaidi duniani kwa sababu ya virusi vya corona.
Ligi zote kubwa zilisimama wakati zilikuwa zikielekea ukingoni na katika baadhi ya nchi mabingwa watarajiwa wakiwa wamejulikana – Liverpool wakiongoza kwa mbali katika Ligi Kuu ya England (EPL).
Sasa hivi nchi kadhaa zinafikiria kurejea kwenye soka kwa ajili ya kuhitimisha msimu wa 2019/2020, Ujerumani wakiwa mstari wa mbele, japokuwa pamekuwa na tatizo baada ya majuzi wachezaji kadhaa kupatikana na virusi hivyo vinavyosababisha homa kali ya mapafu.
Soka ndio mchezo maarufu zaidi hata kwenye televisheni, ndio maana kampuni kubwa zinazorusha matangazo hayo na kuweka yale ya biashara hutegemea kwenye soka na hutoa mamilioni ya pauni kwa ligi husika na klabu zake.
EPL ndiyo yenye umaarufu zaidi na kampuni zimerusha ‘nyavu’ zao huku kwa ajili ya kujipatia faida kubwa. Lakini Covid-19 imevuruga mipango – mechi zimesitishwa na matangazo vivyo hivyo, kila mmoja sasa akitazama na kusikiliza lini mpango wa watu kukaa ndani utafutwa ili ligi irudie.
Ukweli ni kwamba hata ikirudia, soka haitakuwa ile ile kwani haitarajiwi kwamba watazamaji wataruhusiwa, bali wachezaji, makocha, waamuzi na wafanyakazi wengine wachache huku washabiki wakitakiwa kufuatilia kwenye televisheni.
Hata hivyo, hakuna huo uhakika kwamba mechi zitarejea msimu huu, kwani tayari klabu zimeanza kulumbana na Bodi ya EPL juu ya mfumo utakaotumika ikiwa serikali itaruhusu mechi kurejewa. Mpango uliokuwa unajadiliwa ni kutumia viwanja vichache huru kumaliza msimu kwa mechi 92 zilizobaki.
Tayari upinzani umeanza; Aston Villa, Brighton na Watford wakipinga mpango huo wakisema si haki kwao na kwamba mpango utaumiza klabu ndogo. Ikiwa klabu zitakazounga mkono mfumo huo hazitafikia 14 miongoni mwa zile 20 za EPL basi si ajabu ligi ikafutwa au anayeongoza ligi akatangazwa bingwa na timu tatu za mkiani zikashushwa daraja.
Haki za matangazo kwa England zilipanda sana kiasi kwamba BT na Sky Sports walikuwa wakijaribu kudhibiti gharama hizo. Kwa maana hiyo, haki husika kwa kipindi kijacho zilitarajiwa kushuka kiasi.
Hata hivyo bado uhitaji upo kwa kiasi kikubwa kutoka kwa wateja na watangazaji. Baada ya kusitishwa kwa soka tangu Machi, wadau wa soka wanasubiri kwa hamu kurejea tena, iwe ni kwenda uwanjani au kutazama kwenye televisheni.
Kwa hali ilivyo, maambukizi yakiwa bado yapo, haitarajiwi kwamba hali ya soka itarejea ya kawaida hivi karibuni. Itachukua muda – si ajabu miezi ili mambo yawe kama zamani na uchangamfu ule uliokuwako hadi Machi ile, wachezaji na kocha kuambukizwa virusi kabla ya kupona.