in , , ,

KUMALIZA MSIMU 2019/2020

Marvin Sordell

Wanasoka waamue hatima

Wanasoka wanatakiwa kuwa huru juu ya hatima ya msimu wa 2019/2020, ikiwa ni pamoja na uamuzi wa kukataa kurudi uwanjani, anasema mchezaji wa zamani, Marvin Sordell.

Sordell anasema kwamba kurejea uwanjani au la uwe ni uamuzi binafsi wa mchezaji na si suala la kuamua kwa makundi, kwani kila mmoja ana utashi na haki ya kujilinda mwenyewe, familia yake na wale anaokutana nao kipindi hiki cha kusambaa kwa virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu.

Bado Uingereza haijaondosha marufuku dhidi ya mikusanyiko, ikiwa ni pamoja na mechi za soka, na Waziri Mkuu Boris Johnson anatarajiwa kutoa mwelekeo wa kulegeza masharti ya kukaa ndani Jumapili hii, baada ya maelfu ya watu kupoteza maisha katika nchi mbalimbali duniani.

“Ikiwa hawataki kucheza, nadhani uamuzi wao unatakiwa kuheshimiwa. Hatuhitaji kuwa na hali ambapo watu wanalazimishwa kurudi uwanjani kucheza,” anasema Sordell, akiongeza kwamba wachezaji wapewe haki zao kwa sababu ndio wadau wakubwa na bila wao hakuna mechi.

Bodi ya EPL imeshaanza mchakato wa kurejesha mechi 92 zilizobaki kumaliza msimu huu – mradi wenyewe ukienda kwa jina la ‘Project Restart’, lakini tayari baadhi ya wachezaji wanaeleza kuogopa kurudi kucheza wakati huu ambapo bado wagonjwa wapo na virusi havijadhibitiwa.

Mshambuliaji huyu wa zamani wa Watford mwenye umri wa miaka 29 alitestaafu soka kiangazi cha mwaka jana ili kuchukua muda zaidi kujielekeza kulinda afya yake ya akili, anaamini kwamba kila mchezaji anatakiwa kutazama hali yake binafsi.

“Kila mtu ana hali tofauti anayoendelea nayo nyumbani kwake. Baadhi ya watu wanaishi wenyewe, wakiwa hawana wajibu wowote kwa wengine, kwa hiyo hofu yao ni ndogo zaidi juu ya kupata na kueneza virusi kwa wapendwa wao,” anasema mstaafu huyu.

Anaongeza kwamba kuna wengine wana wake na watoto au wanaishi pia na wazazi hivyo wamekuwa na hofu juu ya usalama wa afya zao. Anasema wapo ambao ndicho chanzo pekee cha mahitaji, kama chakula, kwa wazazi wao au familia kwa ujumla.

Sordell anasema kwamba wachezaji wengine wana wake ambao huenda wakapata ujauzito, wengine wana watoto wadogo au wachezaji wengine wana matatizo mengine ya afya hivyo kwamba corona ikiwashambulia inakuwa rahisi kwao kudhurika haraka na hata kupoteza maisha, kama ilivyotokea kwa baadhi ya watu.

“Nadhani kutokana na sababu hizo, hatua zinatakiwa kuchukuliwa kwa umakini mkubwa kwa ajili ya afya za wachezaji na si kuwalazimisha kurudi uwanjani au kukataa kufanya baadhi ya mambo,” anasema Sordell.

Klabu za EPL zilisema Ijumaa iliyopita kwamba wamedhamiria kurudi uwanjani kwa ajili ya kumalizia msimu huu, lakini kwamba bado majadiliano yanaendelea kati yake na Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA), LMA, wachezaji na makocha – wadau wa msingi katika mchakato huo.

Sordell ambaye wiki jana alithibitishwa kwua mwanachama mpya wa bodi ya ushauri ya Chama cha Soka (FA) anasema: “Lazima uheshimu maoni ya watu katika hili. Wengi watasema kwambna kwa vile wanapata fedha nyingi wanatakiwa kwenda kucheza.

“Virusi hivi wakati mwingine ni suala la uhai na kifo na mechi yoyote ya soka – bila kujali umaarufu wake, haiwezi kuwa muhimu au kupewa kipaumbele kuliko afya na uhai wa wachezaji.

“Nadhani hali ya mchezaji mmoja mmoja inatakiwa kuheshimiwa pamoja na uamuzi wake. Ikiwa wanataka kucheza na hali ni salama basi waruhusiwe kucheza. Ikiwa hawataki kucheza kwa sababu hawaoni ni salama, basi nadhani hilo linatakiwa kuheshmiwa,” anasema mwanasoka huyu mstaafu.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Man U hawataki mkurugenzi wa soka

Tanzania Sports

Soka itachukua muda kurejea kawaida