- Liverpool wamepoteza michezo mitatu mfululizo kwa mara ya kwanza chini ya Slot.
- Ushirikiano wa Salah na Isak bado unajengwa, lakini mashabiki wanataka matokeo ya haraka.
- Arsenal sasa wanaongoza ligi, huku Chelsea wakipanda hadi nafasi ya 6.
- Estêvão ameibuka kuwa shujaa mpya wa Chelsea.
Kocha wa Liverpool, Arne Slot, amesema anaamini washambuliaji wake wakuu Mohamed Salah na Alexander Isak wataanza kuelewana vizuri kadri wanavyoendelea kucheza pamoja, licha ya timu yake kupata kipigo cha tatu mfululizo baada ya kufungwa na Chelsea.
Liverpool walipoteza nafasi ya kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ya England baada ya kupigwa 2–1 kwenye uwanja wa Stamford Bridge.
Chelsea walipata bao la kuongoza mapema kupitia Moisés Caicedo, kabla ya Cody Gakpo kusawazisha dakika za lala salama. Hata hivyo, kijana chipukizi wa Kibrazil Estêvão Willian alifunga bao la ushindi dakika ya 95 na kuzua shangwe kubwa kwa mashabiki wa Blues.
Akizungumza baada ya mchezo, Slot alisema timu yake bado iko katika kipindi cha kujijenga baada ya mabadiliko makubwa yaliyotokea msimu huu.

“Kadri Salah na Isak watakavyoendelea kucheza pamoja, ndivyo wataanza kuelewana zaidi. Ni suala la muda na mazoezi,” alisema Slot.
“Tatizo letu kubwa kwenye mechi hizi mbili si nafasi — ni umaliziaji. Tumetengeneza nafasi nyingi kuliko wapinzani wetu, lakini tumefunga mara moja tu.”
Slot pia alimkingia kifua Salah, ambaye alikosa nafasi kadhaa za wazi dhidi ya Chelsea, akisema:
“Ni binadamu. Si kila nafasi atakayopata lazima iwe goli. Watu wanasahau hilo kwa sababu ya kiwango kikubwa alichoonyesha msimu uliopita.”
Kwa matokeo hayo, Liverpool wameporomoka hadi nafasi ya pili, wakiachwa na Arsenal kileleni mwa ligi, huku Chelsea wakipanda hadi nafasi ya sita.
Baada ya mapumziko ya kimataifa, Liverpool watakutana na wapinzani wao wa jadi Manchester United katika mechi inayotarajiwa kuwa ya moto.