MABAO manne kutoka kwa Yanga na Simba yametuma ujumbe mzito kote barani Afrika kuwa timu za Tanzania hazitaki tena mambo ya kusindikiza kwenye mashindano ya CAF. Zikiwa katika vwanja viwili tofauti timu hizo ziling’ara na kuacha gumzo kwa maelfu ya mashabiki waliotazama mchezo huo huko Ndola nchini Zambia na Kigali nchini Rwanda.
TANZANIASPORTS ilishuhudia mchezo huo na kuhitimisha kuwa klabu za Yanga na Simba sasa zinatakiwa kulifikiria Kombe si hatua ya makundi, robo fainali,nusu au fainali. Badala yake timu hizi zinapaswa kuweka mikakati ya kutwaa Makombe na hazina sababu za kusingizia. Mathalani Simba walifika robo fainali msimu wa 2018-19, hatua ya awali 2019-20, robo fainali 2020-21, raundi ya pili 2021-22 n robo fainali katika simu wa 2022-23.
Kwahiyo Simba kufika robo fainali,nusu fainali au fainali si habari tena, bali imani ya mashabiki sasa ni kushuhudua Kombe la AFL linakuja Tanzania. Hali kadhalika Yanga waliwahi kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, na fainali ya Kombe la Shirikisho, kwahiyo washabiki wanatalitaka Kombe la Ligi ya Mabingwa au Shirikisho tu, habari zingine hawataki.
Katika mechi zote mbili, kana kwamba zilikuwa zinapeana taarifa za kupata mabao, Yanga waliigeuza El Marreikh ya Sudan kuwa asusa yao kwenye uwanja wa Kigali Pele baada ya kuinyuka mabao 2-0. Watani wao Simba nao walitoka nyuma na kusawazisha hivyo kulazimisha mchezo wake kumalizika kwa mabao 2-2. Ilikuwa siku nzuri kwa klabu za Tanzania, wawakilishi ambao sasa akili na uwezo wao wamehamishia ushindani kwenye mashindano ya kimataifa baada ya miaka mingi kuwa timu za kusindikiza. Wakati Simba ikiwakilisha ukanda wa Afrika Mashariki katika mashindano mapya ya African Football League (AFL) wakiwa robo fainali, watani wao Yanga wapo kwenye hatua ya pili ya kufuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
KIVUMBI CHA KIGALI
Ndani ya Dimba hilo mashabiki wa Yanga walitawala kiasi kikubwa, walishangilia kuanzia dakika ya kwanza hadi mwisho wa mchezo. Hawakuwa na hofu ya kumkosa nahodha wao Bakari Nondo Mwamnyeto, wala hawakujali sana pale mshambuliaji wao Kennedy Musonda alipowekwa benchi. Ulikuwa mchezo mkali na wa kusisimua, ambapo vijana wa Miguel Gamondi walianza kushambulia lango la El Marreikh kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo.
Yanga ya kocha Gamondi ni ya aina yak. Inacheza mpira wa kasi kuanzia dakika ya mwanzo wa mchezo hadi mwisho. Mashambulizi yao hutokea kila upande, kushoto na kulia, katikati na katika ufungaji wachezaji wote wanaweza kucheka na nyavu. Hata Yanga wanapaswa kujilaumu wenyewe kushindwa kumaliza mchezo mapema ili mechi ya marudioano ipoteze umuhimu kutokana na kukosa nafasi za wazi kutoka kwa washambualiaji wao, Aziz Ki, Max Nzengeli na Clement Mzize. Yanga wana silaha kali msimu huu upande wa kulia Yao Kouasi akiwa beki wa kupanda na kushuka.
Gamondi aliweka ukuta mgumu katika eneo la kiungo na kusambaratisha uhodari uliozeoeleka wa El Marreikh katika eneo hilo. Kahlid Aucho, Mudathir Yahya na Pacome Zouzoua waliifanya safu ya ushambuliaji ya Yanga iwe moto wa kuotea mbalai. Clement Mzize aliwekewa wapishi wote Stephane Aziz Ki, Max Nzegeli na Pacome Zouzoua ambao walikuwa wakipika nafasi nyingi za kufunga. Kana kwamba haitoshi,
Yanga walishuhudia umahiri wa kiungo wao mpya Pacome Zouzoua aliyepika bao la kwanza, kabla ya gonga safi kati ya Nzegeli na Aziz Ki kutengeneza bao la pili lililofungwa na mshambuliaji wao chipukizi Clement Mzize. Mchezaji bora wa mchezo huu kwa TANZANIASPORTS ni Pacome Zouzoua, ni kiungo anayejua kazi yake ana rahisisha mpira wa miguu na kuonekana kana kwamba ni kitu rahisi sana.
SIMBA WANAISAKA FAINALI YA AFL
Unaitaka Simba ya Kimataifa? Ndicho ilichokifanya kwenye uwanja wa Levy Mwanawasa huko Ndola nchini Zambia. Kufunga mabao mawili ugenini na kuwalazzimisha wenyeji Powr Dynamos kutoka sare 2-2. Wachezaji kutoka mataifa matano ndiyo walioanza kikosi cha kwanza cha Simba; Morocco,Tanzania,Mali,Zambia na Cameroon.
Iliwachukua dakika 29 wenyeji Power Dynamos kuweza kupachika bao la kuongoza. Simba walitanguliwa kufungwa bao baada ya makosa madogo katika safu ya ulinzi. Licha ya kutanguliwa kufungwa Simba walionesha kwanini wameteuliwa kuingia kwenye mashindano ya AFL. Walionesha wao ni wazoefu wa kutafuta matokeo ugenini.
Power Dynamos wakiwa wanasaka bao la tatu walijikuta wakifungwa bao la pili na kufanya mchezo uwe 2-2. Matokeo ambayo yaliwarudisha Simba kwenye nafasi katika mchezo wa marudiano uliotarajiwa kuchezwa Oktoba 1 jijini Dar Es Salaam. Aidha, katika mchezo huo langoni mwa Simba alianza golikipa mpya Ayoub Lacked raia wa Morocco, huku Abel na Ali Salim wakiwa benchi. Baada ya dakika 90 za mchezo huo, nafasi ya Aishi Manula langoni iko palepale, lakini Ayoub Lacked huenda akarekebisha makosa yake kwa kuwa huo ulikuwa mchezo wa kwanza wa kimashindano akiwa na jezi za Simba. Mchezaji bora wa mechi ya Simba na Power Dynamos wa TANZANIASPORTS ni Cletous Chota Chama, kiungo aliyejaliwa maarifa na anayerahisisha kazi ya Simba kila inaposaka matokeo mazuri.
UJUMBE KWENDA CAF
Kifupi Yanga na Simba zimetuma ujumbe kwa timu zinashiriki mashindano ya CAF kwamba timu za Tanzania zimepania kunyakua makombe yote mawili. Ikiwa makombe hayatawezekana basi timu za kigeni zitarajie shughuli pevu iwe ugenini au viwanja vya nyumbani Tanzania. Mashabiki wanataka kitu kimoja tu, furaha. Ikicheza Simba wawe na furaha. Ikicheza Yanga wawe na furaha. Ushindi wa timu hizo ni faida kwa soka la Tanzania.
Comments
Loading…