SIMBA wamekosa ubingwa wa Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kukubali sare ya 1-1 na wapinzani wao RS Berkane ya Morocco. Watani wao wa jadi Yanga wanawacheka Simba huku mioyoni wakikiri kuwa hii ni mara ya pili watani wao kulileta kombe la CAF nchini. Simba walianza na Kombe la CAF ambalo lilikuwa kwa hisani ya Mashoud Abiola mwaka 1993 na mwaka 2025 wameleta kombe la Shirikisho licha ya kutotwaa taji hilo. Baada ya kufeli mpango wa kutwa kombe la Shirikisho Simba wameingia kwenye vita nyingine mbili mara baada ya kumalzia ya kwanza. TANZANIASPORTS inakuletea uchambuzi yakinifu kuhusiana na vita tatu kali za Simba na Yanga msimu huu.
Fainali ya Kombe la Shirikisho.
Ukweli ni kwamba mashabiki wananogesha sana mchezo wa soka nje ya sheria zinazoongoza. Hakuna ubishi kuwa Simba walikuwa wananyanyasika mno kutokana na tambo za watani wao Yanga hasa linapofika suala la mashindano ya CAF. Simba walikuwa wanataniwa kila kona kuwa wao ni timu ya ‘Mwakarobo’ yaani ile inayoishia kwenye hatua ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na baadaye Kombe la Shirikisho. Kila walipofurukuta walikuwa wanaishia robo fainali.
Kitendo hicho ni kama kiliwapa hasira Simba ambao sasa wanaweza kupunguza uchungu wa kutaniwa. Yanga wao walikuwa wanawatambia watani wao Simba kuwa wametinga fainali ya Kombe la Shirikisho licha ya kushindwa kupachika bao moja ambao lingeweka mchezo huo sare 2-2. Yanga walikubali kipigo cha 2-1 nyumbani kwenye dimba la Benjamin Mkapa, kisha wakaibuka na ushindi wa 1-0 ugenini, nyumbani kwa USM Alger nchini Algeria.
Kitendo cha Yanga kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho kiliwaibua mashabiki wake na wanachama kuwa wameweka kiwango cha mafanikio kwenye soka. Sasa Simba nao wamefanikiwa kufika kiwango hicho licha ya kufungwa na RS Berkane kwa jumla ya mabao 3-1 ya mechi mbili walizokutana. Kwa sasa vita hii imekwisha lakini ndiyo mwanzo wa kuanza nyingine mpya. Vita ya sasa itakuwa nani kuwa wa kwanza kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa au Shirikisho. Hii ndiyo vita wanayoanza kupambana nayo.
Mtanange wa Ligi Kuu
Hadi sasa Simba na Yanga wanapishana pointi 1 tu katika msimamo wa Ligi Kuu. Timu zote zimecheza michezo 27. Yanga wamejikusanyia pointi 72, wakati Simba wamejipatia pointi 71. Katika mazingira hayo mchuano wa ubingwa msimu huu umekuwa mkali huku watani wa jadi wakiongoza mbio za kutwaa ubingwa.

Simba walikuwa na viporo vingi sababu ya kushiriki mashindano ya Kimataifa lakini sasa wamerejea nyunbani kushiriki kikamilifu katika Ligi Kuu. Vita hii ina maana yeyote atakayeteleza hapo itakuwa ni hasara kubwa kwake. Kwa sasa Simba na Yanga ni kama zinaombeana njaa, mmoja afungwe, lakini pia zinaonesha mikakati kila mmoja ashinde mechi zake ili kujikusanyia pointi za kutwaa taji la Ligi Kuu msimu huu. Hii inakuwa vita ya pili kati ya miamba hii ya soka nchini Tanzania.
Kiatu cha dhahabu
Kuna vita ya tatu inayoendelea kati ya Simba na Yanga. Vita hiyo ni kuwania kiatu cha dhahabu msimu huu. Mchuano wa kuibuka mfungaji bora umeshika kasi kwa timu mbili kati ya 16 za Ligi Kuu. Katika mbio za kuwania tuzo ya ufungaji bora Simba imeingzia wachezaji watatu, huku Yanga wenyewe wakiwa na wachezaji wawili, kisha Singida Black Stars ikiwa na ingizo moja. Jean Ahoua amepachika mabao 15, akifuatiwa na mshambuliaji mahiri wa Yanga Clement Mzize mwenye mabao 13 na mwingine Prince Dube mwenye magoli 12 akiwa anashikilia nafasi ya tatu. Stephen Mukwala wa Simba amepachika magoli 12 sawa na Prince Dube wa Yanga, huku akifuatiwa na mshambuliaji mwenzake wa Simba, Lionel Ateba mwenye magoli 12.
Mshambuliaji wa klabu ya Singida Black Stars, Jonathan Sowah anafunga magoli 11 akiwa anashikilia nafasi ya sita kati ya washambuliaji wanaochuana kuwania kiatu cha dhahabu. Katika orodha hiyo, Yanga wamezidiwa na Simba kwani wao wana wachezaji wawili wakati watani wao wana wachezaji watatu.
Vita vya wageni
Wachezaji wa kigeni wamekuwa chachu ya kukua kwa Ligi Kuu Tanzania, kiasi kwamba sasa vita vya wageni katika kuwania tuzo mbalimbali imeshika kasi. Jean Ahoua (Simba), Prince Dube (Yanga), Stephen Mukwala (Simba), Lionel Ateba (Simba) na Jonathan Sowah (Sindiga) wote ni wachezaji wa kigeni ambao wanaing’arisha Ligi Kuu.
Clement Mzize ndiye mshambuliaji pekee anayewakilisha wazawa akiwa anachuana na wageni ili kudhihirisha nao wazawa wana kitu miguuni. Vita ya ufungaji bora imepambana moto huku wazawa wakimtegemea Clement Mzize kuongoza jahazi lao huku wachezaji wa kigeni watano wakiingia kwenye sita bora kati ya wanaochuana kuwania kiatu cha dhahabu. Hii ni vita nzuri katika maendeleo ya soka la Tanzania.