Katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji, kocha Robertinho Oliviera alianza na viungo wawili wakabaji, Mzamiru Yassin na Fabrice Ngoma…
NI wekundu wa Msimbazi, wakiwa wamevalia jezi nyekundu ndani ya dimba. Wao si mashetani wekundu kama Manchester United wala wananchi kama Manchester City au Yanga. Simba walikuwa katika dimba la Uhuru jijini Dar Es Salaam kupepetana na watumishi wa umma, yaani klabu ya Dodoma Jiji ya jijini Dodoma. Ulikuwa mtanange wenye kila hamasa, na ulisuhudia mshambuliaji mahiri Moses Phiri akifungua kibubu chake cha mabao kwa msimu mpya wa 2023/2023.
TANZANIASPORTS ilishuhudia mtanange huu kwa ukaribu mtanange huo ambao umewapa Simba pointi tatu muhimu kuelekea kuwania ubingwa wa Ligi Kuu.. Simba walipachika bao la kwanza kupitia kwa Jean Baleke, ambaye bila ajizi alitumbukiza mpira wavuni na kuwapa nafasi Simba kusaka jingine.
VITA YA MAGOLI
Washambuliaji wawili wa Simba Jean baleke na Moses Phiri huenda wakawa wanachuana wenyewe kwenye Ligi Kuu kwani moto wao umeanza kushika kasi. Washambuliaji wanapopachika mabao hali ya timu inakuwa na utulivu na kuondoa presha zozote zinazowakabili. Ni mechi mbili ambazo zimeonesha kuwa safu ya ushambuliaji imedhamiria kuwa tegemeo kama kawaida, huku kila mchezaji akiwa na kiu ya kufunga mabao.
MECHI MBILI MABAO 6
Mchezo kati ya Simba na Dodoma Jiji ulikuwa pili wa Ligi Kuu. Katika mchezo wa kwanza Simba waliwachabanga Mtibwa Sugar kwa mabao 4-2 kwenye uwanja wa Manungu huko Turiani mkoani Dodoma. Mchezo wa pili wa Simba wamepachika mabao 2-0 na hivyo kuwa na mabao 6 katika mechi mbili. Kasi ya mabao ya Simba huenda ikawatisha wapinzani wao kwani ndicho kitu ambacho kinaweza kuamua hatima ya mshindi. Kufunga mabao mengi ni silaha kwa timu yoyote, kwahiyo Simba wanatakiwa kusonga mbele na kupchika mabao mengi kwa mgawanyo kutoka kwa washambuliaji tofauti.
KURUDI KWA PHIRI
Kwa muda mrefu mashabiki wa Simba walikuwa wakimlilia mshambuliaji wao Moses Phiri apewe nafasi ya kucheza. Phiri hakucheza katika mchezo wa kirafiki wa Simba Day, lakini akaibukia kwenye mashindano ya Ngao ya Hisani jijini Tanga ambako walitwaa ubingwa huo mbele ya watani wao jadi Yanga. Tanzaniasports imeambiwa kuwa Moses Phiri amerejea kikosini baada ya kupona majeraha yake. Yeye ni mfungaji aliyeongoza kikosini hapo msimu uliopita mbele ya John Bocco, Jean Baleke na Kibu Dennis. Moses Phiri alifunga bao baada ya kuingia akitokea benchi. Ni mchezaji ambaye habari za malalamiko hazikiki, bali kazi yake inaonekana uwanjani.
KIBU DENNIS MIOYONI MWA MASHABIKI
Ni mchezaji ambaye hakutarajiwa kutikisa katika kikosi cha Simba. Mashabiki wengi huamini wachezaji wazawa wanaotokea timu ndogo huwa hawaweza kufurukuta mbele ya wageni. Na ikiwa wanafanikiwa kufurukuta basi ni watatu kati ya kumi. Kibu Dennis amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Simba. Kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji aliitawala vema nafasi ya upande wa kushoto kwenda eneo la ushambuliaji. Alitengeneza muunganiko mzuri kutoka eneo la kiungo na washambuliaji na kuwafanya mashabiki wa Simba wanyanyuke mara kwa mara vitini kushangilia. Kibu Dennis si mchezaji wa dakika chache, mara nyingi anavyoanza ndivyo anavyomaliza kama kocha hajamtoa. Alikuwa mchezaji machachari mbele ya Dodoma Jiji.
MAKIPA WA KISASA
Kati ya mambo ambayo yana kasi ndogo kufuata mabadiliko ni eno la golikipa. Ali Salim, Hussein Abel ni makipa wa Simba ambao wanatakiwa kujifunza mabadiliko ya nafasi zao. Golikipa Mgore wa Dodoma Jiji alifanya kosa la kushindwa kutuliza mpira mguuni ambao alirudishiwa na beki wake. Mgore alikumbusha makosa kama ya Jens Lehamann wa Arsenal, ambapo mjerumani huyo alikuwa changamoto ya kutuliza mpira mguuni. Makipa wa Ligi Kuu wanatakiwa kujifunza kutoka kwa Djigui Diarra ambaye amekuwa fundi wa mpira miguu mbali ya kudaka. Kama nje ya ncji Makipa wa Ligi Kuu wanapaswa kumtazama Williams wa Kaizer Chiefs au Andre Onana wa Manchester United.
VITA YA KIUNGO
Katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji, kocha Robertinho Oliviera alianza na viungo wawili wakabaji, Mzamiru Yassin na Fabrice Ngoma. Itakumbukwa hivi karibuni TANZANIASPORTS ilimshangaa kocha wa Simba kumfanya Fabrice Ngoma kama mchezaji anayetakiwa kuingia kipindi cha pili kubadili mambo. Kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji, Fabrice Ngoma alikuwa kama kocha mchezaji, alielekeza hiki na kile, alifanya hili na lile. Na zaidi alihakikisha eneo lote la kiungo linakuwa tulivu na mabeki wanalindwa vizuri. Mbele ya Mzamiru yassin Simba inawatuliza wapinzani wake. Hii ni vita nyingine ya namba ambako Saido Kanoute atakuwa na kibarua kigumu mbele ya Ngoma na Yassin
Comments
Loading…