in

Simba walizidiwa lakini watafanya maajabu..

PAMBANO la kwanza la robo fainali kati ya Simba na Kaizer Chiefs lilifanyika hapo jana kwenye uwanja wa First National Bank jijini Johanesburg nchini Afrika kusini. Simba wameanza vibaya kwa kuchapawa mabao 4-0 hivyo kuweka rehani nafasi yao ya kufuzu hatua nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mchezo wa marudiano unatarajiwa kufanyika jijini Dar es salaam katika uwanja wa Benjamin Mkapa. 

TanzaniaSports baada ya mchezo huo imezungumza na makocha mbalimbali ili kupata tathmini zao kuhusu mchezo wa Simba na Kaizer Chiefs. Makocha watatu waliozungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao hadharani wamekubaliana kwa nyakati tofauti kuwa Simba walizidiwa kiakili, kilimwili,kifundi na maarifa mengine, lakini wanakiri kuwa mwenendo huu utawasaidia kufanya maajabu miaka ijayo kwa sababu wanazidi kupata uzoefu wa mashindano

MSIMAMO WA LIGI

Tanzania Sports
Msimamo wa LIGI YA VPL

Msimamo wa Ligi wa timu zote mbili ni tofauti. Kaizer Chiefs wanashika nafasi ya 15 katika Ligi Kuu Afrika kusini ambayo ni maarufu kama PSL (Premier Soccer League). Hii ina maana Simba wakiwa vinara na mabingwa watarajiwa wa Ligi Kuu nchini Tanzania walikutana na timu  ambayo inahaha kuepuka aibu ya kufika kwenye mstari wa kushuka daraja. 

Hata hivyo makocha hao wanakubaliana kuwa ubabe wa Simba na kuyumba kwa Kaizer Chiefs katika ligi zao si kigezo cha kufanya vibaya au vizuri katika mashindano ya kimataifa. Wanatolea mfano klabu za Villareal (Hispania), AS Roma (Italia), na Arsenal (Uingereza) ambazo zte zilifika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Uropa (Europa League) huku zikichechemea katika ligi zao za ndani. 

KUHESHIMU TIMU PINZANI

Tanzania Sports
Matokeo ya michezo mingine

“Simba walitakiwa kuheshimu timu pinzani hasa nchi zinazoendelea na zilizoendelea. Najua hapa Dar es salaam watafungwa, je watakubali kufungwa goli 5 bila na wao kupata goli? Nilichikiona Kaizer Chiefs walifanyia kazi mapungufu ya Simba katika mipira ya krosi na mashambulizi ya kushtukiza. Kwa kuwa ligi yao ni bora kuliko yetu, Kaizer wako bora physically,mentally na tactically,” anasema kocha mwandamizi wa soka nchini.

TanzaniaSports lilimtafuta kocha mwingine kuzungumzia hoja hiyo, ambapo alisema, “Simba hata msimu uliopita walifungwa mabao mengi ya aina ya mipira kama ya jana ipira mirefu na krosi na mashambulizi ya kushtukiza. Kaizer walicheza mpira wa malengo, si kucheza tu. Mkufunzi wangu mmoja kutoka nchi zilizoendelea kisoka aliwahi kuniambia, ukiwa kocha hutakiwi kufundisha kila kitu unachokijua kuhusu mpira wa miguu bali unatakiwa kufundisha kitu kwa malengo. Kupata matokeo katika mashindano. Tumejifunza  mengi kama wadau wa soka kwa faida ya taifa letu. Kwa maoni yangu kwa trend hii ya Simba kama wataendelea hivi miaka miwili ijayo wanaweza wakafanya jambo kubwa sio suala la kucheka,” alisema kocha huyo.

HII NI ‘KNOCKOUT STAGE’

TanzaniaSports imeambiwa na makocha hao kuwa hii ni hatua ya mtoano, timu zote zilizofika hapo zina uwezo mkubwa kwahiyo kila mmoja ana kiwango na ubora fulani uliomwezesha kufika hatua hiyo.

“Yangu ni machache sana, kwenye knock out stage hii, hakuna sherehe, umakini,uzoefu na utayari ni vitu muhimu. Kaizer Chiefs walifanya ujanja kidogo tu, kama unakumbuka FC Platinum nao wakiwa kwao walitumia. Hizi timu zinafahamu ni muhimu kunawaacha Simba wawe na mpira, watambe watakavyo, waje kwenye nusu yao ya kiwanja halagu wao wanaweke watu wengi nyuma ya mpira. Kwahiyo Simba wakipoteza mpira Kaizer Chiefs walicheza mipira mirefu kwenda mbele, hapo mabeki wa Simba wanalazimika kukimbia sana wakiwa wanaliangalia goli lao na wapinzani wanakuwa wanamuangalia golikipa Aishi Manula. Kaizer Chiefs hawajaruhusu hali hiyo ya kukimbizwa. Kila mara Luis Miquissone, Chriss Mugalu, Cleotous Chama wanapokuwa na mpira wanakutana na mabeki zaidi ya wanne wanawasubiri. Kama nilivyosema wachezaji wa Kaizer Chiefs wana nidhamu ya hali ya juu na nguvu za mwili,”

‘POSSESIONS ‘BILA USHINDI 

Tanzania Sports
kipindi cha ushindi

TanzaniaSports ilipenda kuwafahamisha mashabiki wa soka kuhusu uwezo wa Simba kutawala mchezo na kumiliki mpira kwa muda mwingi kuna maana gani. Kocha mmoja amesema

“Nimesikia mara nyingi sana wenye elimu ndogo ya soka wanaangalia possession. Lakini kanuni ya mpira inasema mara zote timu inafungwa baada ya kuwa na mpira halafu ukaupoteza. Jambo la pili ukiwa na mpira halafu unataka ukae nao kwa muda mrefu lazima wachezaji wawe na sifa mbili kuu; moja wawe ufundi wa hali ya juu, pili wawe imara maana wanahitajika kukimbia sana ili wawe karibu karibu, hiyo ndio inaitwa intensity. Ndiyo maana Barcelona wanacheza hivyo na wachezaji wao hakuna wavunja kuni. Kumiliki mpira bila ushindi ni hovyo tu,” amesema kocha huyo.

Je nini kitatokea kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa? Je Simba wataweza kupindua matokeo hayo na kuitupa nje Kaizer Chiefs? Hilo ni jambo la kusubiri na kuona. 

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Baadhi ya wachambuzi wa Michezo

MALIPO :UCHAMBUZI WA MICHEZO NI WAJIBU

ZZ

Makocha watajwa kumrithi Zidane