Siyo vibaya kama utasema klabu ya Simba ina wakati mgumu katika Ligi Kuu NBC Premium League, mashabiki wake hawajaizoea kabisa timu yao ambayo imeonyesha kusua sua kwenye kuusaka Ubingwa wa Ligi. Mpaka sasa klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Msimbazi imejikusanyia jumla ya alama 23 ikishika nafasi ya tatu nyuma ya watani zao Yanga SC ambao wao wanakata nafasi ya pili wakiwa na alama 30 huku Azam FC wakiongoza msimamo wa Ligi hiyo na jumla ya alama 31 ingawaje Simba inazidiwa michezo mitatu mbele.
KELELE ZA MASHABIKI
Mashabiki wengi wa Klabu ya Simba wanaamini timu yao kufanya vibaya ni kutokana na umri wa wachezaji wao kuwa ni mkubwa. Mfano mchezaji kama Saido Ntibanzonkiza, John Bocco, Mohamed Hussein Zimbwe, Shomari Kapombe, Clatous Chota Chama, hao ni baadhi ya wachezaji ambao inapelekea timu kuelemewa kama watakutana na timu yenye Kasi zaidi yao. Kipigo walichokipata kutoka kwa Yanga SC cha mabao 5-1, pia kilichagizwa na kasi ya wachezaji wa Yanga ambao kwa kiasi kikubwa wanaongozwa na vijana wenye umri mdogo. Waangalie wachezaji kama Maxi Nzengeli, Clement Mzize, Stephanie Aziz Ki, hiyo ni sababu ya Simba SC kupoteza mchezo ule kwa idadi hiyo ya mabao.
KUCHAGUA VIWANJA
Hii ya kuanza kuchagua ni uwanja upi wautumie pia inachagiza ile ya kufanya vibaya kwenye Ligi. Kwasasa viongozi wanaumiza vichwa ni uwanja upi utafaa kwao kwa matumizi ya michezo yao ya Ligi, tayari wameshatuma barua kwenda ZFF kuomba kama wataweza kuutumia uwanja wa Amaan Stadium Zanzibar kama uwanja wao wa nyumbani. Wengi walijiuliza kwanini Simba wanavikimbia viwanja vya hapa nyumbani na stori kubwa ikielezwa kuwa klabu hii haiko tayari kuuchezea uwanja wa Azam Complex, Chamazi huku wakiamini siyo uwanja wa bahati kwa upande wao.
KUACHWA KWA WACHEZAJI
Eneo ambalo liliawaacha wadau wa soka vinywa wazi ni hili. Hakuna aliyetarajia kama Simba SC ingeachana na washambuliaji wake Moses Phiri pamoja na Jean Baleke na kufanya usajili mwingine. Baada ya kumalizika Katika michuano ya Mapinduzi Cup pale Visiwani Zanzibar, klabu hiyo ilitangaza kuachana na wachezaji hao na kufanya usajili wa wachezaji Freddy Michael Kouablan, Pa Omar Jobe. Inatafsiriwa mabadiliko hayo yamekuwa ni ghafla sana.
KUHUSU UKUTA WA YERIKO
Hapa napo ni pa kukuna kichwa kwa viongozi wa Simba SC baada ya kuwepo taarifa kutakiwa mlinzi wao wa kati Inonga Baca ‘Varane’. Kumezuka taarifa hizo baada ya mlinzi huyo kuonyesha kiwango bora Katika michuano ya AFCON inayoendelea pale nchini Ivory Coast. Baka ambaye anatengeneza ukuta mzuri na beki raia wa Cameroon, Chemalon Fondo na kupelekea kupachikwa jina la utani la ukuta wa Yeriko kutonana na aina yao ya ukabaji, hata hivyo Mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amewaondoa wasiwasi mashabiki na wanachama wa klabu hiyo na kusema hakuna atakayemchukua mlinzi huyo raia wa DR Congo.
IMANI IMEBAKI KWA KOCHA
Pamoja na yote hayo imani kubwa imebaki kwa kocha Mkuu Abdelhak Benchikha ambaye alilithi mikoba ya kocha Roberthino Oliveira aliyefurumishwa kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo. Benchikha aliyetamba na kikosi cha USM Alger ya Algeria amekuwa tumaini jipya kwa Wanamsimbazi baada ya kukosa Ubingwa ndani ya misimu miwili huku watani zao Yanga SC wakipeta ndani ya NBC Premier League.
Comments
Loading…