in , , ,

SIMBA HAIJUI CHA KUFANYA SIMBA DAY, YANGA IKO USINGIZINI

Kuna vitu vizuri lazima viungwe mkono ili viendelee kuwepo kufikia katika ngazi ya ubora.

Uzuri ni hatua moja kuelekea hatua ya ubora, ubora ndiyo kilele cha mafanikio. Mafanikio ni wimbo ambao kila mwaka tumekuwa tukiuimba kila siku kwenye vilabu vyetu.

Tumekuwa tukitamani vilabu vyetu vipate mafanikio makubwa ndani na nje ya uwanja.

Mafanikio ya ndani na nje ya uwanja yanategemeana kwa kiasi kikubwa sana kwa sababu huwezi kuwa na mafanikio ndani ya uwanja bila kuwa na mafanikio nje ya uwanja.

Mafanikio nje ya uwanja yana nguvu sana kutengeneza ubora wa timu ndani ya uwanja. Kwa kifupi timu yenye misuli mikubwa nje ya uwanja ndiyo timu yenye ubavu wa kupambana na kushinda mataji makubwa.

Mataji makubwa huja kipindi ambacho pesa nyingi zinapowekezwa, ndiyo soka la kisasa !. Huwezi kupata mchezaji bora bila kuwa na msuli wa pesa.

Huwezi kuongeza hali ya kupigana kwa wachezaji bila kuwa na msuli wa pesa, ndipo hapo kila siku tumekuwa tukivishauri vilabu vyetu vijiendeshe kibiashara.

Somo la biashara kwenye mpira limekuwa somo gumu sana kwa sababu ya kukosa maono ndiyo maana ni virahisi kukuta timu ikililia mtu fulani mwenye pesa aje aweke pesa zake bila kuwa na makubaliano maalumu ya kibiashara.

Leo hii Yanga iko Morogoro kwa ajili ya maandalizi ya mechi za msimu ujao (pre-season), ilihali Simba wako Uturuki.

Hapa ndipo utakapoona somo la mechi za maandalizi ya msimu mpya (pre-season). Ni ngumu kuelewa mechi hizi zitawanufaije kibiashara.

Simba iko Uturuki, inawezekana itakuwa faida kwao kupata sehemu nzuri ya kupigia mazoezi na kujifunza vitu vingi vipya kwao lakini kibiashara kuna faida kubwa kuzidi faida ya wao kucheza mechi za maandalizi ya msimu mpya wakiwa nchini?

Tumekuwa tukihimiza vilabu vyetu vitumie nembo ya vilabu vyao kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo zitakuwa zinauzwa kwa mashabiki wa timu husika.

Mfano, Yanga imekuwa ikilia kuhusu suala la ukata. Walishindwa nini kutengeneza mkakati wa kuandaa mechi za kujipima uwezo kipindi hiki cha maandalizi ya msimu mpya katika mazingira ya kibiashara?

Mfano, wangeamua kucheza mechi mbili kwenye baadhi ya mikoa ambayo inasemekana Yanga ina mashabiki wengi.

Kungekuwepo na mechi mbili katika mkoa wa Lindi, Mtwara, Songea. Na kwenye hizo mechi Yanga ingetumia nafasi hiyo kuuza baadhi ya bidhaa ambazo zitatumika katika msimu mpya.

Mfano, wangeteneza skafu, kofia, jezi, vikombe, mazulia ya mlangoni yenye nembo ya Yanga afu wakauza siku ya mechi hizo mbili.

Wangenufaika katika kwenye kiingilio na kuuza bidhaa hizo. Baada ya hapo wangechagua mikoa mingine ambayo ina mashabiki wengi. Hii ingetosha kuwapa mechi za kujipima uwezo na kuingiza pesa kwa wakati mmoja.

Simba imekuwa na utaratibu mzuri sana wa Simba Day kila mwaka siku ya tarehe 8 mwezi wa nane.

Utaratibu ambao naona unafanyika katika mazingira yale yale kila siku. Wameshindwa kufikiria njia bora ya kuandaa siku hii iwe bora na wafaidike kiuchumi.

Mfano kungekuwepo na kampeni ambayo ingekuwa ya wiki mbili kabla ya tamasha la Simba Day.

Simba ingecheza mechi kadhaa katika mikoa kadhaa, mechi ambazo zitakuwa na dhima ya Simba day kuelekea kwenye kilele chenyewe cha Simba Day.

Mwanza wangepewa Simba Day yao, Tanga, Mbeya , Shinyanga na sehemu nyingine. Simba ingecheza mechi moja na timu ya mkoa husika, mechi hiyo ingetumika kuuza bidhaa za Simba na kutambulisha wachezaji wapya na hii ikawa kama mechi za kuelekea kilele chenyewe.

Kilele hiki kingekuwa na maandalizi bora kuanzia kwenye uchaguzi wa timu bora inayoalikwa mpaka maandalizi bora ya kuandaa vifaa vyenye nembo ya timu husika.

Tusiishie kufikiria kwenda nje ya nchi wakati soko letu la ndani hatujaliimarisha. Tuna mashabiki wengi sana hapa Tanzania ila bado hatujawajengea mazingira ya kibiashara, mazingira ambayo yatawawezesha wao watoe pesa yao mfukoni kwa ajili ya kujenga timu yao.

Kipindi cha mechi za maandalizi ya msimu mpya ndicho kipindi cha kutengeneza nembo imara ya biashara kwenye hizi timu zetu.

Ni vyema tukafikiria upya jinsi ya kutumia maandalizi ya msimu mpya kibiashara kwa kuanzia hapa, tukijijenga hapa tutakuwa na nguvu ya kwenda nje ya nchi kujitanua kibiashara kwa kutumia mechi za maandalizi ya msimu mpya.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Zlatan Muacheni ajifananishe na mvinyo

Tanzania Sports

Tunawekeza Ubora wa Paa la Taifa Stars na kusahau Msingi