in , , ,

SERIKALI IZUIE USHIRIKI WA MASHINDANO YA DARFUL

 

HAKUNA ubishi miongoni mwa sehemu za hatari za dunia yetu kwa sasa, Darfur Sudan ni mojawapo. Hali ya huko kwa sasa ni kama ilivyo ya DR Congo Mashariki, Somalia, Syria na sehemu nyingine zinazorindima vita vya wenyewe kwa wenyewe. Sehemu hizo si salama kabisa kufanyika kwa mambo ya furaha na ya raha ya kimataifa kama michezo. CECAFA wamepeleka mashindano ya kombe la Kagame ya mwaka huu huko Darfur kwenye hatari! Kwa maana hiyo wanaweza kupeleka mashindano hayo Somalia kwani naona kwao ufanikishaji wa malengo yao ndilo jambo la msingi kuliko usalama wa wafanikishaji jambo hilo.

 

Kwa kuitambua hatari hiyo, timu mbili kubwa na maarufu za Sudan zimekataa kushiriki mashindano hayo. Hizo ni El Merreikh na El Hilal. Kenya nao hawapeleki timu. Kwa maana hiyo mashindano ya mwaka huu yatakuwa zaidi ya bonanza ikizingatiwa kuwa zile za Sudan zitakazoshiriki mashindano hayo, kwa Tanzania, zinaweza kuwa kama Polisi Morogoro na African Lyon!

United Nations Security Council Resolution 1672
United Nations Security Council Resolution 1672 (Photo credit: Wikipedia)

 

Jambo moja la kusisimua ni kwamba Mtanzania mmoja aliyebobea katika masuala ya uhusiano wa kimataifa na mjuzi wa masuala ya kunusa nusa akiwa shushushu mwandamizi, katumia ujuzi wake usiotiliwa shaka kwenye taaluma hizo mbili na kueleza wazi kwamba si salama vijana wetu wa Yanga, Simba na Falcon kwenda kushiriki mashindano ya kombe la Kagame mwaka huu huko Darfur. Kwa bahati mbaya sana, mtaalam huyu, Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, ameishia kutahadharisha tu; hakuelekeza kwamba timu zetu zisiende huko.

 

Mwanya huo wa kutotolewa katazo la serikali la ushiriki wa mashindano hayo unachukuliwa sivyo kabisa na TFF, Yanga na Simba. Kwa kusema tu kwamba Darfur si salama, serikali ilipaswa itafsiriwe kwamba imeshazuia ushiriki wa watu wake kwenye mashindano huko. Kama sivyo, kauli ya uhatari wa Darfur imetolewa kwa malengo yapi? Kama hawakuilewa serikali, Yanga na Simba kila siku wanatoa kauli kueleza kuhusu ushiriki wao wa mashindano hayo wakimaanisha kwamba lazima watashiriki! Mdhamini wao naye amewapa vifaa katikati ya sintofahamu hii!

 

Huu ni utovu wa nidhamu kwa upande mmoja kutokana na kuiona kauli ya serikali kama upuuzi fulani. Kwa upande mwingine huku kunaonesha jinsi baadhi yetu tusivyojitambua; Nani hajui kwamba Darfur si salama? Kwa nini usalama wako unautekeleza kwa kutegemea kauli za watu wengine? Eti klabu zetu zinasubiri mpaka serikali ikitamka moja kwa moja; hakuna kwenda Darfur ndipo zitaacha kwenda kwenye hatari hiyo.

 

Usishangae hapo wakaibuka wapambe fulani na kuishitaki serikali yao wenyewe FIFA kwamba serikali yao imeingilia masuala ya soka. Naamini Mheshimiwa Membe aliuhisi upuuzi huo na ndiyo maana amewapa changamoto TFF waweke sawa jambo hili wenyewe lakini wao wanasema wanasubiri tamko la serikali la kuzuia timu zetu kwenda Darfur. Kwa nini wanataka wafanyiwe kazi yao na serikali? Au wanataka wanawe mikono kama watu fulani watalalamikia hatua hiyo kwamba si wao walioamua?

 

Usalama wa mtu ni jukumu lake mwenyewe; si vizuri watu wetu wa mpira wakasubiri serikali iwalazimishe kulinda maisha yao badala ya wao wenyewe kuanzisha mchakato huo. Kwa sababu kuna kutegeana miongoni mwa serikali, TFF na vilabu kuhusu kushiriki kwetu mashindano kwenye eneo hatari kama Darfur, serikali yenyewe izuie ushiriki huo na huko wala si kuingilia masuala ya soka.

 

Jamani, usalama ndiyo msingi wa kila tufanyalo la kimaendeleo. Tukitafakari hilo, ni vizuri tukikumbushana kwamba waasi na magaidi wa sehemu yoyote ya dunia hulenga sana kundi la wageni wanaofika eneo lao la mashambulizi kwa mkakati kwamba wakiwadhuru, wataichonganisha serikali yao na za nchi walikotoka wageni hao. Kwa nini tuivamie hatari kubwa namna hiyo? Sababu ya kombe tu!

 

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

FA yalilia wazawa Ligi Kuu England

Ushiriki Darfur mikononi mwa serikali- Tenga