Mcheza tenisi maarufu, Serena Williams ameweka rekodi kwa kufikisha taji la 21 la Grand Slam.
Serena Ametwaa ubingwa wa sita wa Wimbledon na kukamilisha kile kinachoitwa ‘Serena Slam’.
Mmarekani huyu amefikia hatua hiyo baada ya kumshinda Garbine Muguruza wa Hispania na sasa ndiye anashikilia mataji yote manne makubwa duniani.
Serena (33) alishinda kwa seti 6-4 6-4 hivyo kufikisha taji la 21 la Grand Slam, likiwa pia ni taji la tatu kwa mwaka huu pekee.
Alifanikiwa kuzuia makali ya Muguruza (21) aliyejaribu kurejea mchezoni na hatimaye akaibuka kidedea baada ya saa moja na dakika 23.
Baada ya kumaliza kazi hiyo, Serena ataelekea US Open mwezi ujao akidhamiria kukamilisha kalenda ya kwanza ya Grand Slam tangu aanze mchezo huo kiushindani.
Kwa Muguruza ilikuwa mara yake ya kwanza kucheza katika fainali ya Grand Slam na awali aliongoza kwa 4-2 akimtisha vilivyo Serena ambaye alitulia na kuifanya kazi yake sawa sawa.
Serena amekiri kwamba kulikuwa na shinikizo kubwa upande wake, hasa dakika za mwisho, akisema Mhispania huyo alicheza vyema kiasi cha kumfanya afikirie kukwama kutwaa taji hilo.