in , ,

Sepp Blatter: Yametimia

*Aamua kuachana na soka moja kwa moja

*Michel Platini anatafuta njia ya kurudi

Michel Platini, hajakubali yaishe...
Michel Platini, hajakubali yaishe…

Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Joseph ‘Sepp’ Blatter
ametangaza kuachana na soka moja kwa moja, akidai kwamba amekamilisha
kazi yake.

Akionekana kutokuwa nadhifu kama siku nyingine, akiwa hajanyoa ndevu,
baadhi ya vifungo vya shati vikiwa havijafungwa huku akiwa amefungwa
plasta ya khaki chini ya jicho, Blatter ambaye ni raia wa Uswisi,
alitoa kauli iliyosubiriwa na wengi kwa miaka mingi.

“Nimemaliza kazi yangu kwenye soka,” akasema Blatter, siku moja tu
baada ya kuhukumiwa adhabu ya kutojihusisha na soka kwa miaka minane,
adhabu iliyotolewa kwake na Kamati ya Nidhamu ya Fifa baada ya kumtia
hatiani kwa ufisadi.

Blatter (79) amewatupia lawama washirika wake wa miaka mingi kwa mambo
yaliyolifika shirikisho hilo, akisema binafsi hakujua kabisa kama
kulikuwa na chochote ndani ya Fifa kinafanyika kinyume cha sharia,
kanuni au taratibu.

Pamoja na kuamua kuachana na soka, Blatter ana mpango wa kupinga
hukumu na adhabu dhidi yake ili kusafisha jina machoni pa umma.
Amemaliza vibaya urais aliouanza 1998, kwani kabla ya adhabu ya sasa,
alifungiwa kujihusisha na soka kwa siku 90 wakati uchunguzi dhidi yake
ukiendelea.

Sambamba naye, mwingine aliyepigwa adhabu ya kukaa nje ya soka kwa
miaka minane baada ya ile ya awali ya siku 90 wakati akichunguzwa, ni
Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Michel Platini. Mfaransa
huyu alikuwa akiwania kugombea urais wa Fifa kwenye uchaguzi wa
Februari mwakani na alikuwa akipewa nafasi kubwa kushinda lakini jina
lake likakatwa.

Wakati Blatter amedai hukumu na adhabu dhidi yake ni upuuzi, Platini
amesema kamati hiyo ilikuwa imelala usingizi wa pono kwa miaka minne,
kwa ‘kosa’ walilohukumiwa nalo linadaiwa kutendwa 2011, kwa Blatter
kumpa pauni milioni 1.3 wanazosema ni malipo ya kazi ya ushauri wa
ufundi kwa rais huyo.

Kamati ya Nidhamu ya Fifa ilianza uchunguzi wake na kuwafungia wawili
hao baada ya mamlaka za Marekani na Uswisi kuanza uchunguzi tofauti
dhidi ya viongozi mbalimbali wa shirikisho hilo wa sasa na wa zamani
ambapo zaidi ya vigogo 14 wameshanaswa.

“Hiyo Kamati ya Maadili ilikuwa inafanya nini tangu 2011 nilipolipwa
hadi 2015? Ilikuwa imelala? Ghafla inaamka. Ehe, ndio, inaamka mwaka
wa uchaguzi wa Fifa baada ya kuona mie ni mgombea. Ni ajabu,” akasema
Platini.

Platini naye anakata rufaa, ambapo mpango wake ulikuwa kwenda moja kwa
moja katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ili kuwahi
mchakato wa uchaguzi huo wa Februari.

Hata hivyo, Fifa imewaandikia wanasheria wa Platini kuwaeleza hawawezi
kwenda moja kwa moja CAS, bali wanatakiwa kufuata mtiririko wa
taratibu za kisheria na rufaa, hivyo apite kwanza Kamati ya Rufaa ya
Fifa, asioridhika ndio aende CAS.

Platini amekuwa na matumaini kwamba ataepuka mlolongo wa rufaa ndani
ya Fifa ili awahi anayoiita haki yake ya kuwania urais wa shirikisho
hilo, ikizingatiwa kwamba huu ni msimu wa sikukuu na tayari mchujo wa
kwanza wa wagombea umefanywa huku jina lake likiwekwa kando kusubiri
hatima yake kwenye shauri hilo.

Blatter anamalizia vibaya uongozi wake, kwani wakati akiwania uongozi
mwaka huu, Platini alimshauri dakika za mwisho aondoe jina lake maana
mikono yake ilikuwa michafu kutokana na hongo za mamilioni ya pauni
zinazodaiwa kutembezwa shirikani, lakini Blatter akasema ushauri huo
ulichelewa mno.

Hata hivyo, siku nne tu baada ya kushinda tena kiti hicho kwa miaka
mine ijayo, Blatter alitangaza uamuzi wa kuachia ngazi Februari
mwakani, kwa maelezo kwamba hakuwa akiungwa mkono na ulimwengu wote wa
soka.

Pamoja na hayo alisema alikuwa anaendelea na mchakato wa mageuzi
makubwa ndani ya Fifa, japokuwa wengi waliona kwamba haikuwa sahihi
kwa mtu aliyekaa hapo kwa zaidi ya miaka 17 kuanzisha mageuzi huku
shirika likiwa limezongwa na harufu mbaya ya ufisadi.

Blatter ana tuhuma nyingine mbalimbali, ambapo anachunguzwa na Kamati
ya Nidhamu ya Fifa juu ya dili la 2005 kuhusu haki za televisheni
baina ya Fifa na rais wa zamani wa Shirikisho la Soka la Amerika
Kaskazini na Kati (Concacaf), Jack Warner.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Arsenal wawachapa Man City

Tanzania Sports

Van Gaal awekwa mtu kati