in , , ,

SIMBA WANAHITAJI FUNZO LINGINE

 

 

Unakumbuka wakati fulani mwezi Aprili mwaka huu mlinzi mahiri wa kulia wa Simba SC aligoma kusafiri na klabu hiyo kwenda mkoani Shinyanga kucheza mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar?

Alikuwa anapigania maslahi yake. Alikuwa akiushinikiza uongozi wa Simba umpatie milioni 5 zilizokuwa zimesalia kwenye ada yake ya uhamisho na pia fedha za kupangia nyumba ambazo zilikuwa sehemu ya mkataba wakati anasajiliwa akitokea Mtibwa Sugar.

Huyo ni Hassan Kessy. Mlinzi ambaye amekuwa akifanya vizuri sana upande wa kulia tangu alipohamia Simba. Shinikizo lake lilifanikiwa na siku chache baadaye akapewa haki yake na akarejea kwenye ratiba za timu hiyo kama kawaida.

Nafikiri wakongwe hao wa Ligi Kuu Bara waliteleza kidogo kwenye swala hilo. Labda nisiwalaumu sana kwa kuwa pengine kipindi kile hawakuwa wamepata funzo na ndio maana walifanya mzaha kwenye swala hilo la Hassan Ramadhani Kessy.

Lakini nakumbuka kuna jambo lingine lilikuja kuwatingisha mno wakongwe hawa miezi miwili baadaye. Hilo lilikuwa swala la Ramadhani Singano. Nae pia alikuwa akipigani maslahi yake dhidi ya Wekundu hawa wa Msimbazi.

Simba walikuwa wanadai kuwa mkataba wa Singano ulitakiwa kumalizika Julai 2016 wakati Singano alikuwa anadai kuwa mkataba wake halali ulikuwa unaishia Julai mwaka huu. Uamuzi wa kamati ya maadaili ya TFF ukaangukia upande wa Singano na akatangazwa kuwa mchezaji huru.

Advertisement
Advertisement

Simba walifanya jitihada za dhati kujaribu kumshawishi Singano asaini mkataba mpya. Walijua wazi kuwa kijana huyo ni mmoja kati ya wachezaji wa viwango vya juu hapa nyumbani. Lakini juhudi zao zligonga mwamba mchezaji huyo aliposajiliwa na Azam FC mapema mwezi Julai na kutia mfukoni milioni 50.

Hili lilikuwa funzo kwa Simba SC. Niliwahi kuzungumzia kwenye makala zangu za nyuma kuwa kuwa uzembe na ujanja ujanja ndio uliowafanya kushindwa kurefusha mkataba wa mchezaji huyo mapema.

Jana nilikutana na habari nyingine iliyonifanya niyakumbuke hayo. Habari hii inamhusisha Hassan Kessy kwa mara nyingine. Mkataba wa miezi 18 ambao mchezaji huyo alisaini mwezi Disemba mwaka jana utabakiza miezi sita mwezi ujao ambapo kwa mujibu wa sheria za usajili atakuwa huru kufanya mazungumzo na timu nyingine.

Kocha mkuu wa Simba SC Dylan Kerr amezungumza akiusisitiza uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha mlinzi huyo mahiri wa upande wa kulia anaongezewa mkataba mpya haraka iwezekanavyo ili asalie kwenye timu hiyo.

Nafikiri Simba wameendelea kuwa wazembe kwa mara nyingine. Hivi unawezaje kuacha kurefusha mapema mkataba wa mchezaji kama Hassan Kessy kabla ya hata mkataba huo haujakaribia kubakisha miezi sita?

Kuna taarifa kuwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wamejipanga vyema kumuwania mlinzi huyo wa kulia ambaye mwalimu Charles Boniface Mkwasa amemjumuisha kwenye kikosi cha timu ya Taifa hivi karibuni.

Tunawajua Yanga walivyo vizuri kwenye swala la kutumia pesa kusajili wachezaji wazuri na kuwalipa vizuri. Kuna hatari kuwa mchezaji huyo anaweza kushawishika na akagoma kusaini mkataba mpya na timu yake anayoitumikia sasa kwa kuwa amebakiza mwezi mmoja tu kuwa huru kufanya mazungumzo na timu nyingine.

Kiwango cha Kessy kimekuwa kikiongezeka siku hadi siku. Sijui Simba walikuwa wanasubiri nini kurefusha mkataba wake siku zote hizi. Nafikiri bado wanasumbuliwa na uzembe. Pengine wanahitaji funzo lingine kwa kuwa funzo walilopata kupitia swala la Singano halikuwatosha.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

TP Mazembe wafalme

Tanzania Sports

Moyes afukuzwa Sociedad