in , , ,

Moyes afukuzwa Sociedad

 

*Vieira bosi mpya New York City

 

Real Sociedad wamemfukuza kazi kocha wao, David Moyes, aliyefanya kazi huko kwa siku 364.

Kocha huyu wa zamani wa Manchester United, Everton na Preston anaondoka baada ya kuanza kwa tabu kazi yake Novemba 10 mwaka jana, timu wakiwa nafasi ya 16 akawapandisha vyema na kumaliza msimu wakiwa nafasi ya 12 msimu uliopita.

Hata hivyo, wakati anakamilisha siku yake ya 364 Jumatatu hii, Moyes alikuwa ameshindwa kuielekeza juu timu, bali ikawa ikiporomoka na kufika kwenye nafasi ile ile aliyoiacha, ambapo kwa msimu huu ni mechi mbili tu walizoshinda.

Moyes (52) ameondolewa kazini baada ya timu yake kufungwa hata na timu ndogo ya Las Palmas 2-0 Ijumaa iliyopita na timu nyingine ndogo siku zilizopita. Ameondoshwa kwenye nafasi hiyo sambamba na msaidizi wake, Billy McKinlay.

Sociedad ambao wana mechi mbili ngumu mbele yao – dhidi ya mabingwa wa Ligi ya Europa, Sevilla na kisha dhidi ya mabingwa wa Ulaya, Barcelona, watakuwa chini ya kocha msaidizi wa zamani wa Barca, Eusebio Sacristan aliyepewa mkataba hadi Juni 2017.

Hii ilikuwa kazi ya kwanza kwa Mskochi huyu tangu alipofukuzwa kazi na Man United, Aprili 2014 baada ya kukaa Old Trafford kwa miezi 10 tu. United msimu huo waliporomoka hadi nafasi ya saba na kukosa fursa ya kushiriki ligi za kimataifa wala kupata kikombe chochote.

Alikaa Everton kwa zaidi ya muongo mmoja, na ilikuwa vigumu kwa bodi ya klabu hiyo kukubali kwamba walikuwa wakimpoteza, baada ya kocha aliyeachia ngazi United, Sir Alex Ferguson kumpendekeza Mskochi mwenzake huyo kurithi mikoba yake.

Moyes mwenyewe alieleza kwamba hangeweza kukataa ofa ya kufanya kazi kwenye klabu kubwa kama United. Alirithi wachezaji waliotwaa ubingwa msimu wa mwisho wa Fergie, lakini hawakuweza kusonga mbele naye vyema.

Kwa sasa anapigiwa chapuo na wengi kurudi kwao Uskochi na kufundisha timu aliyopata kuchezea enzi zake – Celtic. Mkataba wake uliokatishwa Hispania ulikuwa uende hadi Juni mwakani, hivyo atasubiri kulipwa fidia kwa kukatishiwa.

Sociedad walipoteza mechi sita kati ya 11 za ligi, na baada ya kufungwa tena Ijumaa, wamiliki na bodi wakashindwa kuvumilia, bali kumwondosha Moyes ili wajaribu njia nyingine. Majuzi Moyes alikaririwa akisema kwamba angeitiwa kazi ya Aston Villa angeweza kuifikiria, lakini sasa wameshamwajiri kocha mpya, Remi Garde, baada ya kumfukuza Mwingereza Tim Sherwood.

 

VIEIRA APEWA UKOCHA NEW YORK CITY

Patrick Vieira
Patrick Vieira

Nahodha na kiungo wa zamani wa Arsenal, Patrick Vieira amepewa kazi ya ukocha katika klabu ya New York City, ambako wachezaji wake ni pamoja na Frank Lampard na Andrea Pirlo.

Vieira (39) alikuwa kocha mkuu wa timu ya vijana ya Manchester City yenye udugu na New York City. Mfaransa huyo amesaini mkataba wa miaka mitatu. Inadhaniwa kwamba wamiliki wa klabu hizo wanamuandaa ili aje kuwa kocha wa Man City siku zijazo, kwani amekaa hapo kwa muda sasa.

Kazi hiyo mpya, hata hivyo, ataianza Januari mosi mwakani, na licha ya kucheza na kung’ara na Arsenal akiwa na kikosi kile cha ‘Invincibles’, Vieira alitwaa ubingwa wa dunia na Timu ya Taifa ya Ufaransa 1998.

“Nimefurahika sana kuchukua majukumu ya kocha mkuu wa New York City FC. Ni jukumu linaloacha matarajio ya kusisimua kwa kocha yeyote.

Baadhi ya wachambuzi waliona kwamba Arsenal walifanya makosa kutomchukua na kumwaandaa kwa ajili ya kazi ya ukocha Emirates kwa siku zikazo. Ndivyo pia wanavyompigia chapuo Thierry Henry, ili siku Arsene Wenger akiondoka achukue mikoba yake.

Licha ya Arsenal, Vieira amechezea timu za Juventus alikotwaa nao ubingwa wa Italia 2006 kabla ya kujiunga na Inter Milan na kutwaa makombe matatu ya ndani. Alijiunga na Man City Januari 2010 na akatwaa nao ubingwa wa Kombe la Fa 2011 kabla ya kustaafu soka.

Advertisement
Advertisement

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

SIMBA WANAHITAJI FUNZO LINGINE

Tanzania Sports

Platini aandaliwa njia