in

Samba inatawala kila Ligi duniani

samba

SAMBA ni inajulikana kama aina ya soka la Kibrazil. Vilevile pili la utani la Brazil baada ya Selecao yaani wacheza Samba. Lakini Samba pia ni utamaduni ambao unagusa maisha ya watu wa Brazil kwa karne nyingi zilizopita. Ni muziki (ala), ngoma na burudani. Sherehe za Samba hufanyika kila mwaka ifikapo Desemba 2.

Kihistoria watu weusi kutoka bara la Afrika ndio walioanza kucheza ngoma za Samba nchini Brazil kunako karne 16. Ngoma (ala) hizo zilichezwa kama sehemu ya utamaduni. Watu waliburudika. Walijisahaulisha shubiri za kila namna za ukoloni wakati huo. Walijumuika watoto na Vijana. Watu wa makamo na wazee. Wote walicheza Samba mitaani.

Samba ilitoka Angola. Wabantu hawa ndio waliopeleka Samba huko Brazil. Angola  ni nchi iliyopo kusini kwa jangwa la Sahara na mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Ni nchi ambayo imewakuwa na raia mmoja mtata aitwaye Jonas Savimbi.

Tanzania Sports
Everton, Leo Messi, Erick Pulgar na Edison Cavani

Baadhi ya mapigo (ala) yalitoka Congo. Kwahiyo waafrika kutoka Angola (95%) na wachache kutoka Congo waliingiza ala hizo kwneye jimbo la Bahia huko Brazil, ambako watumwa wengi waliwekwa hapo kama kambi na kuanza maisha.

Angola ndiyo iliyoandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010. Ni nchi ambayo inalo jimbo moja liitwalo Cabinda. Kwenye jimbo la Cabinda kuna kikosi cha waasisi ambao wanataka kujitoa katika taifa la Angola, kisa utajiri wa mafuta. Wanatamani wawe taifa, yaani nchi ya Cabinda.

Naam. Samba ni ngoma au muziki ambao umeongezwa vionjo kutoka jamii za Amerika kusini pia, lakini mwanzo na asili yake ni Angola. Watu waliotoka Angola ndio walilipeleka Samba nchini Brazil.

Katika karne ya 20 kuna ala zilizoongezwa kwenye Samba. Samba huchezwa katika kundi, wala haitegemei mchezaji mmoja. Uchezaji wa Samba unahusisha watu wote yaani kundi.

Naomba nitoe mfano kwa mazingira niliyokulia na kushuhudia uchezaji wa ngoma unaofanana na Samba kwa mbali.  Katika wilaya yetu ya Nyasa mkoani Ruvuma tunacheza ngoma za Madogori (Lindeku), Makanya ama Ligambusa. Ni ngoma za wote, kila mmoja anajiachia msimu wake unapofika, hasa kiangazi. Ni matamasha kama ilivyokuwa kwa Samba.

Naongelea Samba la mtaani sio ‘sherehe’ ya pili ya Samba inayoandaliwa kumbi za starehe. Samba linachezwa mtaa kwa mtaa nchi nzima ya Brazil.  

Kwenye ngoma za kwetu za Ligambusa au Lindeku pana staili zake za kucheza. Unafuata stepu kwa stepu, lakini si kundi maalumu bali wote tunacheza. Mpigaji wa ngoma anakuwa katikati huku kundi la watu wanaocheza wanatengeneza duara kucheza stepu kwa stepu.

Ni kama vile Afrika magharibi hasa nchi za Togo, Ghana, Nigeria, Benin wanavyocheza ngoma zao za Azonto. Ni ngoma au muziki wa utamaduni ambao sasa umetangazzipo aina takribani nne za Samba.

Lakini ‘Samba de roda’ ndiyo chimbuko la aina zingine kutoka makoloni yote ya Ureno (Lusophone). Wabantu hao walicheza mtindo uitwao Lundu (tamka ‘Landu au Landum”) huko Brazil. Wabantu hao walitumika katika biashara ya utumwa (Atlantic Slave Trade) kati ya Ureno, Brazil na Afrika.

Katika karne ya 15 Wareno ndio walikuwa wanafanya biashara ya utumwa. Kufika karne ya 17 na 18 kulikuwa na watumwa wengi nchini Brazil waliotoka Angola.

Katika karne ya 18 watu wa Ulaya walihusisha mtindo wa kucheza Lundu ni sawa na uchawi. Wazungu hawakuwa na elimu wala ufahamu wa uchezaji wa ngoma hizo hivyo wakaudhika na kuubatiza utamaduni huo kuwa ‘uchawi’.

Waliamini kucheza wakiwa nusu utupu (kujisitiri sehemu za siri tu kama wafanyavyo wacheza Samba) ni uchawi. Lakini watumwa hao waliendelea kucheza na kupiga ngoma za Lundu kama sehemu ya utamaduni wao. Baada ya hapo ndipo mtindo huo ukapata umaarufu nchini Brazil.

Mwaka 1749, mwanamuziki wa Kibrazil, Manuel de Almeida Botelho alihamia jijini Lisbon (Ureno) akitumia muziki wa Modinha pamoja na kuimba na kucheza mtindo wa Lundu.

Hadi karne ya 19 mtindo wa Lundu ulikuwa muziki rasmi ulipendwa na watumwa na wale waliozaliwa baadaye Brazil kutokana mchanganyiko wa kijamii.

Mtindo wa Lundu hutegemea upigaji wa gitaa, filimbi, kinanda na ngoma. Pia hufanana na mitindo ya Zamba (Argentina), Zamacueca (Peru), Bolero (Cuba) ambazo zote zilichezwa katika kipindi cha ukoloni na watu weusi.

Kwahiyo basi mtindo wa Lundu ndiyo chanzo cha ngoma za muziki wa Choro, Maxixe na baadaye Samba ya Brazil ya sasa kama inavyopendwa na wenyewe.

Nataka kukuambia tu, wachezaji wenye asili ya Brazil wametawala kila kona ya dunia hii. Ligi Kuu Tanzania Bara nayo imepokea wacheza Samba watatu wakiwa katika kikosi cha Mabingwa wa soka nchini Simba. Gerson Fraga Vieira, Tairone Santos da Silva, Wilker Da Silva. Na hiyo ndiyo historia ya Samba.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Jhai Dhillon

Kulikoni Waasia wachache EPL?

kikosi cha yanga

Yanga Kusajili Wachezaji Tisa