Kuna vingi vinavyoenda na kubaki katika maisha yetu kama kumbukumbu inayodumu. Kumbukumbu ambayo ni ngumu kuisahau kwa sababu ya ubaya au uzuri wa tukio husika.
Mara nyingi watu wazuri hawadumu ila vitu vyao vizuri wanavyovifanya hudumu kizazi baada ya kizazi. Kizazi chetu kinamkumbuka Peter Tinno kwa sababu moja tu alifanikisha sisi tufuzu katika michuano ya Afcon kwa mara ya kwanza na ya mwisho.
Hatujawahi kufuzu tena katika michuano hii ya Afcon, lakini goli lake alilofunga nchini Zambia ndilo linatufanya leo hii tuandike na kuelezea kwa furaha yenye maumivu ndani yake.
Furaha yetu ilikuwa pale tu Peter Tinno alipofunga goli lililotupeleka Afcon mwaka 1980, lakini maumivu yanakuja kipindi ambacho unapogundua kuwa tuna miaka miaka mingi hatujawahi kufuzu Afcon.
Tumekuwa wapekwe sana, upweke ambao unatuongezea huzuni kubwa kwenye maisha yetu ya soka kwa sababu hatuna kitu chochote cha kujivunia. Tutajivunia kwa mafanikio gani tuliyonayo? , tumekuwa na maendeleo yasiyoridhisha katika mpira wetu.
Maendeleo ambayo hayatuoneshi mwanga wowote kule tunapoelekea ndiyo maana hata aliyekuwa raisi wa awamu ya pili, Mzee Alli Hassan Mwinyi alikata tamaa mpaka akasema sisi ni kichwa cha mwendawazimu.
Juu ya kichwa chetu kila kinyozi mchanga atatumia kujifunzia. Tuko kwenye dunia hii, dunia ambao inaumiza sana, dunia ambayo kila uchwao machozi ya huzuni huteremka taratibu katika mashavu ya uso wetu.
Machozi hayajawahi kutuishia, huzuni haijawahi kukaa mbali na sisi , unyonge ndilo vazi ambalo kila siku tumekuwa tukilitumia kuivika ngozi yetu. Hatuna furaha kabisa kwenye mpira kwa muda mrefu.
Tunashauku ya kufanya vizuri lakini tumeshindwa kufanya vizuri, miguu yetu imefungwa kamba ambayo inatuzuia kupiga hatua kwenda mbele kila tunapohitaji kwenda. Tumekosa mtu sahihi wa kutuokoa kwa muda mrefu.
Njia nyingi sana tumezitumia lakini hazijaweza kutufanya kufikia kwenye kilele cha matamanio yetu. Leo hii tuko uwanjani tena, tukisubiri hatima yetu ambayo itatupa mwangaza wa safari yetu tena kama tunaweza kwenda Cameron au la.
Hii siku imekuwa ya mawazo mengi sana kwangu, natamani kuiona timu yangu ya taifa siku moja ikishiriki mashindano makubwa. Nitaumia siku Mungu akinichukua bila kushuhudia timu yetu ya taifa haijashiriki mashindano makubwa.
Niko mnyonge sana, najiuliza sana kipi kifanyike ili tuweze kufuzu kwenda Afcon nchini Cameron. Katikati ya fikra zangu picha ya Peter Tino inanijia kila mara.
Na kibaya zaidi inakuja na maswali mengi sana ambayo yananipa wakati mgumu kupata majibu yake ya sisi. Kipi alikuwa nacho Peter Tino ambacho Mbwana Samatta hana?.
Alijisikiaje Peter Tino kufunga goli lile na anajisikiaje kwa sasa Tanzania inavyomtambua kama mchezaji aliyeweka alama ya sisi kushiriki Afcon kwa mara ya kwanza?.
Kina Mbwana Samatta hawaoni wivu kuivunja rekodi hii?, miguu yao inathamani kubwa sana. Na thamani hii ameshaionesha ulaya msimu huu. Amekuwa mmoja wa wsshambuliaji hatari kwa sababu amekuwa rafiki sana wa nyavu.
Kitu ambacho tunakihitaji sana katika mechi ya Leo, tunamtaka leo atengeneze urafiki wa nyavu. Urafiki ambao hajawahi kuutengeneza tangu aanze mpira. Sawa, Tanzania itamkumbuka Mbwana Samatta kama mchezaji aliyefanikiwa kucheza soka la kulipwa barani ulaya lakini itamwezi kama atafanikiwa kuipeleka timu ya Taifa katika michuano ya Afcon.
Nyakati za yeye kukumbukwa tayari zimeshatimia kwa mengi aliyoyafanya kilichobaki ni yeye kutengeneza nyakati za kuenziwa. Nyakati ambazo atajijengea Ufalme nchini kwetu, nyakati ambazo kina Sunday Manara walishindwa, nyakati ambazo hata Mrisho Ngassa hakufanikiwa kuziweka.
Tuna leo moja tu katika maisha yetu, hatuna leo mbili, leo ni moja tu na tunatakiwa tuitumie ipasavyo leo yetu kwa manufaa ya kesho yetu. Kipi kitakufanya tukukumbuke kesho?, bila shaka leo ndiyo itatufanya tukukumbuke kesho.
Leo inathamani kubwa sana katika maisha ya binadamu, na huwa tunakosea sana kusubiri kesho ili tufanye kitu ambacho ni bora. Kitu bora na kikubwa kinatakiwa kufanyika leo. Na leo hii ndiyo siku ya kina Mbwana Samatta kujijengea kiti cha enzi katika soka letu.