
Anaitwa Ruben Amorim. Ni raia wa Ureno na mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya nchi hiyo na mchambuzi mahiri. Kabla ya kutumbukia kwenye ukocha alikuwa mchambuzi wa soka mara baada ya kustaafu soka. Lakini kocha huyo wa Man United anahangaika kuisuka upya timu ambayo imekuwa dhaifu kupindukia tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson. TANZANIASPORTS inaangazia sababu za timu hiyo kuyumba na kukosa ubingwa wa Ligi Kuu kwa muda mrefu.
Jinamizi la Ferguson
Kufundisha timu kwa miaka 26 ni kipindi kirefu sana kwa kazi ya ukocha. Alex Ferguson anakuwa miongoni mwa makocha waliodumu muda mrefu kwenye klabu moja. Hata hivyo tangu alipoandoka na kustaafu kazi hiyo mwaka 2013 Man United haijawahi kurudi kwenye ubora. Ni kama vile jinamizi la Alex Ferguson linawatafuna. Kukaa muda mrefu kwneye taasisi hiyo kunaweza kuathiri utamaduni na kuwa ule wa mtu badala ya taasisi yenyewe kutengeneza utamaduni wake. Alex Ferguseon alikuwa dude la kutisha katika viti vya ukocha klabuni hapo. Alifanya kila kinachowezekana kuhakikisha klabu hiyo inakuwa bora na inawavutia wachezaji bora. Lakini tangu aondoke timu imeyumba kwa kiasi kikubwa na kusababisha mzimu wake kuendelea kuwatesa mashabiki wa timu hiyo.
Vipaji visivyokidhi mahitaji
Baadhi ya wachezaji wanaosajiliwa Man United hawajaonesha kiwango kilichotarajiwa. Hii maana yake usajili unaofanywa unalenga wachezaji ambao hawakidhi mahitaji. Man united ilikuwa na kundi kubwa la wachezaji ambao mchango wao ni hafifu. Ukosefu wa wachezaji mahiri umechangia timu hiyo kuyumba na kupoteza mwelekeo. Kila man united inapocheza unagundua kuwa inakosa wachezaji wenye ufundi wa hali ya juu. hata wale wanaosajili wakitegemewa kuja kufanya vizuri katika klabu hiyo lakini mambo yanakuwa hovyo. Wachezaji kadhaa wamepitia wakati mgumu lakini mmoja pekee alithubutu kusema matatizo yaliyomo klabuni. Cristiano Ronaldo alilalamika hali ya Man United, na kudai kila kitu kimekuwa cha kizamani, huduma za wachezaji zimebaki zilezile na kwamba hapakuwa na mabadiliko. Maana yake wachezaji walioletwa hawakuwa na wale wenye kiwango na uthubutu wa kupinga mazingira ya kazi.
Lango lao lipo wazi
Edwin van Der Sar ndiye golikipa wa mwisho wa Man United aliyekuwa na kiwango bora ndiye ambao klabu hiyo inaweza kujivunia naye. Tangu wakati wake wamepita makipa wengi lakini hakuna aliyefikia angalau kiwnago chake. Golikipa wa hivi karibuni, Andre Onana alisajiliwa akitokea Inter Milan, lakini baada ya misimu kadhaa hali yake ilikuwa mbaya. Uamuzi wa kocha Ruben Amorim kumtoa kwa mkopo bado haijatatua tatizo lao la golikipa. Katika mchezo wao dhidi ya Chelsea wikiendi hii ulionesha wazi eneo la golikipa bado halijpata tiba.
Safu ya ulinzi dhaifu
Man United inafungwa sana mabao kutokana na aina ya walinzi wake. Harry Manguire alisajiliwa akitokea Leicester City alikokuwa beki hodari. Lakini tangu aliposajiliwa katika kikosi cha Man United hali ya mambo ilibadilika. Kiwango chake hakikuchukuliwa kama bora na huku makosa ya mara mara kujifunga mabao yalikuwa kama kichekesho kwa fedha walizolipa. Safu ya ulinzi imepitia wachezaji wengi, ambapo sasa hakuna mwenye uhakika wa kumaliza dakika 90 kwani wanabadilishwa mara kwa mara. Katika mechi kadhaa beki Harry Manguire amekuwa akibadilishwa na wenzake na kufanya safu hiyo isiwe na mwenyewe.
Upande wa kulia anatumika Mazroui aliyesajiliwa kutoka Byaern Munich na wakati mwingine hutumika Diogo Dalot. Hata hivyo wanaweza kucheza mechi moja kisha inayofuata wakabadilishwa nafasi ay kuwekwa benchi. Hali kadhalika beki wa kushoto hutumika Diogo Dalot na Luke Shaw kabla ya ujio wa Dorgu. Dorgu alisajiliwa Januari mwaka huu angalau alionesha umahiri na kwa kuanza kikosi cha kwanza mara kwa mara. Msimu mpya amekuwa akichezwa kama winga wa kushoto ambako anasaidiwa na beki wake Luke Shaw. Udhaifu wa nafasi ya kushoto ulioneshwa na Man City ambapo vijana wa Ruben Amorim walijikuta wakizabwa mabao 3-0. Katika mchezo huo pia mabadiliko katika safu ya ulinzi yalifanywa na kocha wao.
Ukame wa mabao
Timu kama haifungi mabao ya kutosha inajikweka katika shinikizo. Safu ya ushambuliaji ya Man United imekuwa na ukame mkubwa wa mabao. Ujio wa mshambuliaji mpya Sesko unaonekana kama kuibuka matumaini mapya, lakini nyota huyo anaendelea kukabiliana na hali ya mambo katika klabu ya Old Traford. Safu ya ushambuliaji ya Man United imekuwa katika changamoto ya kupata mabao, na hivyo kusababisha kushambuliwa mara nyingi.
Viungo wasio na dira
Kila ukitazama mchezo wa Man United swali la kwanza unalotakiwa kuuliza, ni ipi dira ya viungo wake? katikatimu yoyote safu ya kiungo wa ulinzi na ushambuliaji ni moyo wa timu. Viungo waliopo Man United hawaonekani kuwa roho ya timu ingawaje katika mchezo wao dhidi ya Chelsea walifunga mabao (Casemiro na Bruno Fernandes). Aidha, katika safu hii pia viungo mbadala nao imekuwa changamoto nyingine, kwani kwenye benchi lao yupo Kobi Mainoo ambaye ni chipukizi anayeendelea kuliweka sawa jina lake. Endapo roho ya timu haina nguvu maana yake Man United itayumba tu.