MAKOCHA wa Arsenal bila shaka walikuwa wameketi kwenye makochi na kumtazama kijana wao akiwakilisha klabu yao. kijana huyu Myles Lewis-Skelly ni mchezaji halali wa Arsenal. Ni kinda ambaye ameibuka msimu huu na kuonesha umahiri katika usakataji wa kandanda. Myles Lewis-Skelly ameweka rekodi ya kipekee baada ya kuibuka kuwa mchezaji chipukizi kufunga bao katika mechi ya kwanza ya Timu ya Taifa ya Wakubwa.
Nyota huyo toka Arsenal aliitwa katika kikosi cha timu ya Taifa chini ya kocha Thomas Tuchel ambaye alianza mwanzo mpya katika kibarua cha kuinoa timu hiyo mwaka huu. Mchezo wake wa kwanza ulikuwa dhidi ya Albania uliochezwa juzi ijumaa. Kinda huyo amefurahia maisha ya soka baada ya kuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha Arsenal kinachonolewa na Mikel Arteta.
Iliwachukua dakika 20 kwa England kuvunja ukuta wa Albania na kuandika bao la kuongoza. Albania walikuwa wakicheza mchezo wa kujihamia zaidi hivyo safu ya ulinzi ilikuwa na jukumu la kuzuia tu badala ya kusogeza mashambulizi dhidi ya England.
Licha ya nahodha wa England Harry Kane kuwepo katika mchezo huo, lakini nyota ya Lewis-Skelly ilidhihirika na kuonensha mwanzo mpya wa utawala wa Thomas Tuchel. Nyota wengine waliokuwa sambamba na nahodha wao ni Jude Bellingham, Phil Foden na Marcus Rashford ambao walikuwa kwenye kikosi cha kwanza, ilikuwa siku ya Lewis-Skelly aliyetangulia kufumania nyavu. Jude Bellingham alipokea mpira na kukimbia upande wa kushoto kuelekea lango la Albania, huku Lewis-Skelly alikuwa anafuatilia kwa utulivu na kupachika bao la ushindi kufuatia mpira uliombabatiza golikipa wa Albania,Thomas Strakosha.
Akiwa na umri wa miaka 18 na siku 176, Lewis-Skelly anakuwa mchezaji wa kwanza kinda kufunga bao katika mchezo wake wa kwanza. Bao hilo linakuwa la kwanza kwa tangu England ilipocheza mechi rasmi mwaka 1972 dhidi ya Scotland.
“Miasha hayawi mazuri ziadi ya hapa, kwa kuweka rekodi kwenye mechi ya kwanza na kufunga bao zuri namna ile. Ni kinda huyu, anaanza soka lake la kimataifa kwa England dhidi ya Albania. Ni maisha mazuri sana,” alisema kocha mkongwe Stuart Peace akizungumzia bao hilo na uchezaji wa Lewis-Skelly.
Kinda huyu pia amevunja rekodi ya miaka 9 ambayo iliwekwa na Marcus Rashford wa Manchester United ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo katika klabu ya Aston Villa. Marcus Rashford alifunga bao la kwanza la Kimataifa alipoiwakilisha England dhidi ya Australia akiwa na umri wa miaka 18 na siku 209 Mei mwaka 2016.
Wakati huo huo, shambulizi la Lewis-Skelly limemfanya anakuwa mchezaji wa tatu na ambaye anaingia kwenye rekodi ya wachezaji vijana wa England kuifungia nchi yao kwenye mchezo wa kwanza wanaopangwa. Wayne Rooney ndiye kinara wa rekodi hii kwani alifunga bao la kwanza septemba mwaka 2003 akiwa na umri wa miaka 17 na siku 317.Rooney alifunga bao hili wakati wa mchezo kati ya England na Macedonia kaskazini. Michael Owen anakuwa mchezaji wa pili kufunga bao la kwanza akiwa na timu ya taifa katika mchezo kati ya England na Morocco. Owen alifunga bao hilo akiwa na miaka 18 na siku 164 Mei mwaka 1998.
Lewis-Skelly amefurahia soka lake kutoka kikosi cha vijana hadi cha wakubwa katika klabu ya Arsenal. Alianza kucheza kikosi cha kwanza Septemba mwaka 2024 na tangu hapo amekuwa mchezaji mwenye mwendelezo wa ubora na muhimu kwa Mikel Arteta.
Lewis amecheza mechi 26 kwenye mashindano yote. Katika mechi za Ligi Kuu amecheza michezo 14, kati yake mechi 9 ameanza kukosi cha kwanza. Kipaji chake huenda hakijaanza kuonekana vema katika kikosi cha England, lakini amebahatika kuitwa kutokana na kuumia kwa chaguo la kwanza la beki wa kushoto wa England, Lewis Hall wa klabu ya Newcasle United ambaye ameumia.
Lewis-Skelly amecheza kwa kiwango cha juu sana cha soka na kuanza kumiliki nafasi ya beki wa kushoto wa Arsenal na sasa anawinda nafasi hiyo kwa England. Hata hivyo atakabiliana na changamoto kutoka kwa Lewis Hall, beki ambaye anafahamiana vyema na kocha Thomas Tuchel. Lewis Hall ndiye aliibuliwa na kocha Thomas Tuchel alipokuwa kocha wa Chelsea, ambapo alimpa nafasi ya kucheza mwaka 2022 akitokea kikosi cha vijana.
Kana kwamba haitoshi Lewis-Skelly ana faida nyingine kuliko Lewis Hall kwa sababu anaweza kucheza hata kwenye kiungo. Hivyo basi inatarajiwa Thomas Tuchel atampa nafasi ya kutosha Lewis-Skelly kwenye kikosi chake kutokana na umahiri alioonesha kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Albania. Jumatatu England watakuwa uwanjani kupepetana na Latvia na bila shaka Lewis-Skelly atakuwa beki wa kushoto wa England na kujiongezea nafasi nyingine ya kupata uzoefu.