in

Refa ameiba matokeo ya Simba na Geita Gold FC

Mechi ya Simba dhidi ya Geita Gold Fc ilikuwa ya kupendekeza mno tangu mwanzo ambayo ilimalizika kwa ushindi wa mabao 2-1 na kuwaongezea pointi mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Simba. Baada ya mchezo huo wamejikusanyia pointi 17, wakiwa nyuma ya Yanga. Huu unakuwa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu kwa mwezi Desemba. 

Ni mchezo ambao ulizkutanisha timu kongwe na ngeni katika Ligi Kuu. Vijana wa kocha Fred Minziro walionesha kandanda safi na kuwasisimua mashabiki wengi. Ninaamini soka safi lililooneshwa na Geita litawapa nafasi mashabiki wengine kukubali uwezo wa kocha Minziro na vijana wake licha ya ugeni wao kwenye mchezo huo. 

Nimeona mechi nzuri yenye ufundi kwa wachezaji binafsi na mbinu za makocha kwa ujumla wake. Geita Gold namna wnaavyocheza,wanavyojenga mashambulizi yao,wanavyopiga pasi fupi fupi,wanavyonana na kuwatetemesha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Simba lilikuwa jambo la kipekee mchezoni. 

Geita wanastahili pongezi kwa kile walichokifanya uwanjani, ufundi na uhodari wao katika kusaka mabao ulikuwa wa kiwango kizuri, na hakika inapendeza kuona mechi nzuri kama hii ikichezwa kwenye Ligi Kuu Tanzania.

Aibu

Simba wanaamsha amsha nyingi lakini wanaonekana wazi kutafuta namna ya kutengeneza kombinenga. Tunaweza kusema kuwa kocha Pablo Franco Martin alikuwa na mpango maalumu kuwapa nafasi wachezaji wa akiba ili  wawe na utimamu wa mchezo, lakini bado ilikuwa haioneshi ujuzi wa hali ya juu. Ni kama vile kocha anataka kila mchezaji acheze, lakini namna ya kucheza haijapatikana. Kazi ni kazi na kasi ya wachezaji bila mipango thabiti itakuwa na madhara wakikutana na timu kali. 

Kitu kimoja kizuri Simba wanaweza kutafuta matokeo vizuri sana, na wanahitaji nidhamu ya Efua Morrison ili afuzu kubeba timu zaidi, pia wanahitaji wepesi wa kupokea na kutoa pasi kwa haraka wa Larry Bwalya kwa sababu kuna muda mipira iliishia kwake wakati mpango ulianza kutengenezwa. Kingine Bwalya haoneshi kasi ya mchezo ili kuipa uhai safu ya kiungo mshambuliaji.

UTATA WA MWAMUZI

Jambo moja ambalo limetia dosari mchezo wa Simba na Geita ni  uamuzi wa refa Martin Saanya. Mwamuzi huyo alikataa bao la kusawazisha la Geita kwa madai mfungaji alimchezea madhambi beki wa Simba kabla ya kupiga kichwa mpira kwenda wavuni hivyo kuamua ni golikiki. 

Picha video zilionesha wazi kuwa mfungaji hakumgusa beki wa Simba Shomari Kapombe, yaani hapakuwa na mgusano wowote kati ya mshambuliaji na beki, lakini mwamuzi Martin Saanya akaashiria sio bao. Kwa namna moja tukio hilo linaeza kutafsiriwa kuwa ni wizi wa mwaka, kwa sababu mwamuzi alitoa uamuzi wa uongo kwa sababu za uongo na kuinyima Geita pointi. 

Matukio ya waamuzi kuboronga mechi yamekuwa yakishamiri mno kiasi kwamba TFF na Bodi ya Ligi zimekuwa zikitoa adhabu mara kwa mara kwa waamuzi kutokana na kushindwa kumudu mchezo.

Mathalani mwamuzi wa mchezo kati ya Namungo dhidi ya Yanga aliadhibiwa kwa makosa ya kushindwa kumudu mchezo na kutoa tafsiri potofu ya sheria 17 za FIFA. 

Matukio ya namna hii yanaharibu sifa za waamuzi na mchezo wenyewe. Waamuzi wanajikuta hawapati nafasi ya kuchezesha mechi za kimataifa kwa sababu ya kufanya maamuzi yaliyojaa utatanishi na yasiyohusishwa na sheria za soka. 

RATIBA NGUMU SIMBA

Katika mchezo huo kocha Pablo Franco Martin alipangua kwa kiasi kikubwa kikosi chake. Uamuzi huo unatokana na ratiba ngumu wanayokabiliana nayo hivyo aliwapumzisha ili kuwapa nafasi ya kuepuka uchovu wa mechi. Simba watapambana na Yanga Desemba 11, pia wana michezo mingine ya Kombe na Shirikisho la soka Afrika dhidi ya Red Arrows na Kombe la ASFC kwahiyo alihitaji kuwapumzisha nyota wengi kikosini. 

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
SIMBA SC

Mambo  ya kuchungwa na Simba jijini Lusaka

Yanga Vs Simba

Simba,Yanga mwenye kisu kikali atakula nyama