*Man United wamwendea Sergio Ramos
Real Madrid wapo tayari kutoa pauni milioni 21 ili kumnasa mlinzi wa kati waArsenal, Laurent Koscielny.
Hatua hiyo inakuja baada ya Manchester United kutinga Madrid na ofa ya pauni milioni 35 kwa ajili ya kumsajili beki wao wa kati, Sergio Ramos.
Mwenyewe Ramos anaelezwa kupendezwa kucheza Ligi Kuu ya England na amewataka Madrid waifikirie ofa hiyo ili akakipige Old Trafford.
Madrid wameonesha nia ya kumchukua Koscielny kwa sababu mazungumzo ya mkataba mpya baina yao na Ramos yamevunjika, huku mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania akiwa amebakisha miaka miwili ya kucheza Santiago Bernabeu.
Mtendaji Mkuu wa real Madrid, Jose Angel Sanchez alikaa na mchezaji huyo pamoja na kaka yake, Rene Ramos ambaye pia ni wakala wake katika viwanha vya mazoezi vya klabu hiyo vya Valdebebas, lakini badala ya kufikia mwafaka wa Ramos kubaki Bernabeu, mchezaji huyo aliomba klabu ianze majadiliano na United.
Hata hivyo, Arsenal watapambana kuhakikisha kwamba Koscielny, mmoja wa wachezaji wao muhimu, anabaki Emirates, akiwa pia amesaini mkataba wa muda mrefu na Arsenal mwaka jana tu. Huu ni wakati ambapo Washika Bunduki wa London wangependa kujiimarisha badala ya kuuza wachezaji.
Ndiyo maana wamefika hatua ya kubisha hodi kwa mahasimu wao wa London, Chelsea kwa ajili ya kumsajili kipa aliyedumu Old Trafford kwa miaka 11, Petr Cech ambaye sasa anasubiri kufanyiwa vipimo Emirates wakati wowote.
United walianza kuonesha nia ya kuchukua wachezaji wa Real baada ya kuwapo kila dalili kwamba kipa wao namba moja, David De Gea angeondoka Old Trafford na kuhamia kwao Hispania.
Pamekuwapo pia kutoelewana baina ya Ramos na Rais Florentino Perez, rais akisisitiza kwamba Ramos hawezi kuondoka hadi pale klabu itakapofikia dau la pauni milioni 180 zilizo kwenye kifungu cha mkataba wake, kama bei ya awali ya kumuuza.
Iwapo Madrid watampoteza Ramos na kumkosa Koscielny, wanatarajiwa kuwaendea mlinzi wa Athletic Bilbao, Aymeric Laporte au yule wa Valencia, Nicolas Otamendi ambao wamepata kutakiwa na Real Madrid.
Katika tukio jingine, Manchester United wamewatumia salamu Barcelona wakiwaambia kwamba hawana nia ya kumuuza kiungo wao, Angel Di Maria. Barca wameulizia juu upatikanaji wa raia huyo wa Argentina majira haya ya kiangazi.
Dimitri Payet anatarajiwa kujiunga na West Ham United, ambapo amefikia hatua ya kufanyiwa vipimo Alhamisi hii au mapema Ijumaa, baada ya ofa ya pauni milioni 10.7 kwa Marseille kukubaliwa.
Manchester United wameingia kwenye vita na Liverpool wakimtaka mshambuliaji wa Sevilla, Carlos Bacca anayekadiriwa kugharimu pauni milioni 21 zilizowekwa kwenye kifungu cha mkataba wake.
Manchester City wanafikiria kutoa ofa ya tatu na ya mwisho kwa mshambuliaji wa Liverpool, Raheem Sterling. Liverpool wanaweza kukubali ofa ya pauni milioni 50, hasa baada ya kumnunua mshambuliaji mwenye sifa za Sterling, Roberto Firmino wa Brazil kwa pauni milioni 28.
Aston Villa wanasisitiza kwamba mshambuliaji wao Mbelgiji, Christian Benteke hatauzwa kwa bei pungufu ya pauni milioni 32.5 iliyoelezwa bayana kwenye kifungu cha mkataba wake.
Everton wanatarajia kutangaza usajili wa kiungo wa Barcelona, Gerard Deulofeu waliyekuwa naye kwa mkopo Goodison Park msimu wa 2013/14. Klabu mbili hizi zinaelezwa kukubaliana tayari juu ya mchezaji huyo.
Katika hatua nyingine, mchezaji wa Arsenal, Lukas Podolski anaamini kwamba alifanya makosa kujiunga na Inter Milan kwa mkopo msimu uliopita na sasa anasema anaamini atafanya makubwa Arsenal msimu ujao.
Mabingwa wa Uturuki, Galatasaray wanataka kumsajili Podolski lakini Mjerumani huyo amekaririwa akisema kwamba soka ya England ndiyo inalandana na mtindo wa mchezo wake japokuwa anaona mambo yanabadilika na ingekuwa vyema hangeenda hata Milan.