Mwenyekiti wa klabu ya soka ya Simba, Ismail Rage amewaomba radhi wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kufuatia taarifa za kukanganya kuhusu hatma ya kocha Patrick Phiri.
Kocha Phiri anatarajia kurejea kesho kutoka nchini Zambia alikokwenda kwa mapumziko baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodacom, Mei mwaka huu.
Akizungumza na Nipashe jana kwa njia ya simu toka Tabora, Rage amesema yeye na uongozi mzima wa klabu hiyo wanaomba radhi kwa taarifa hizo za kukanganya.
“Napenda kuwaomba radhi watanzania na wapenzi wa soka kwa ujumla juu ya mkanganyiko uliojitokeza kuhusiana na kocha wetu Patrick Phiri, tulitangaza kumuacha kabla ya kukubali kuendelea naye kufuatia yeye mwenyewe kuomba radhi na kuahidi kuja Jumatatu,” alisema.
Kabla ya Phiri kuthibitishwa kwamba atarejea kwenye klabu hiyo ya mtaa wa Msimbazi, uongozi wa klabu hiyo ulitoa kauli ya kumtimua kazi kutokana na kocha huyo kushindwa kurejea nchini kwa wakati.
Mbali na kutangaza kumtimua Phiri, pia uongozi wa klabu hiyo ulisema kwamba uliamua kuwasiliana na aliyekuwa kocha wao wa zamani Milovan Cirkovic ili kuchukua nafasi yake.
Akifafanua, bosi huyo mpya wa Simba alisema mkanganyiko huo kwa kiasi kikubwa ilichangiwa na Phiri kutokana na kushindwa kutoa taarifa za wazi na zinazoeleweka kuhusu kibarua chake.
Rage alisema kama kiongozi muadilifu, amekubaliana na Phiri kurejea nchini kwa ajili ya kuifundisha msimu unaokuja wa ligi kuu, baada ya kuiwezesha kutwaa ubingwa wa kihistoria bila kupoteza mechi hata moja msimu uliopita.
“Kumtimua Phiri kwa hakika ingeivuruga Simba kiuchezaji na ndio maana tumeamua kumpa nafasi aendelee ili hata atakapoondoka basi tuachane kwa amani na heshima kama alivyoingia,” alisema mwenyekiti huyo.
Kwa mujibu wa Rage, Phiri atatua kesho mchana na moja kwa moja ataelekea Zanzibar kwenye kambi ya timu yao inayojiandaa na mechi yao ya Ngao ya Hisani dhidi ya watani zao Yanga, Agosti 14.
Comments
Loading…