in ,

PSG walikitupa kitabu walichopewa na Barcelona

Pesa za mafuta zimemwagwa sana. Uwekezaji mkubwa umefanyika kwa kiwango cha juu sana kwa kutumia pesa za mafuta.

Na hii ni kwa sababu moja tu, kuifanya PSG kuwa timu kubwa barani ulaya, kuifanya PSG iwe timu ambayo inafanya vizuri katika michuano ya ulaya.

Hili ndilo lengo lao kuu, ndiyo maana hawakusita kumleta yeyote yule mwenye jina ambaye waliwaza kuwa anaweza kuwasaidia.

Unadhani ilikuwa rahisi kwa Carlo Ancelloti kuja PSG bila pesa za mafuta ?. Hapana, pesa za mafuta ndizo zilikuwa na nguvu ya kumleta Carlo Ancelloti pale.

Pesa hizo hizo za mafuta ndizo zilizomleta Zlatn Ibrahimovich katika ardhi ya Paris nchini Ufaransa. Huu ni ushawishi mkubwa sana.

Ushawishi ambao ulimfanya Neymar aikane Barcelona, aiache Barcelona yani aichague PSG mbele ya Barcelona. Haya ndiyo maajabu ya nguvu za pesa.

Nguvu ambazo zilitumika kukusanya wachezaji wengi nyota katika klabu moja, lengo ni moja tu kuifanya timu ifanye vizuri katika michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya.

Ndiyo maana kikosi hiki kina Mbappe, Cavanni, Neymar, Draxler , Di Maria, Verrati, Rabiot , Thiago Silva, Buffon , Dani Alves ndani ya kikosi kimoja.

Hawa ni wachezaji haswaaa, hawa ni wanaume haswaaa na wapo ndani ya kikosi kimoja kwa ajili tu ya kuifanya timu ifanye vizuri kwenye michuano ya ulaya.

Lengo lao ni ligi ya mabingwa barani ulaya tu. Hawawazi kitu kingine kwa sababu vingine wameshashinda vyote.

Unafikiri PSG wanawaza kuhusu Ligue 1? , Hapana, mawazo yao yote yapo kwenye ligi ya mabingwa barani ulaya.

Hapa ndipo tamaa yao ilipo, lakini kuna kitu kimoja tu ambacho wanasahau na kila mwaka huwa wanapewa funzo na cha ajabu huwa hawajifunzi.

Sijui ni ukaidi, sijui ni kujiamini sana?. PSG hawana njaa, hawana njaa ya kufanya vizuri kwenye michuano hii mikubwa barani ulaya.

Kufanya vizuri kwenye michuano hii lazima uwe na njaa. Uwe na moyo wenye tamaa ya kufanya vizuri. Hii michuano kuna timu zimeshaweka kuwa lazima kushinda hili kombe.

Yani wachezaji wamelishwa sumu ya kwanini kushinda hili kombe, ndiyo maana kila wakikanyaga uwanjani kwao wao mpira huwa hauishi mpaka pale refa anapopiga kipenga.

Unaikumbuka mechi ya Barcelona na PSG iliyochezwa katika uwanja wa Nou Camp? Ile mechi ambayo Barcelona walishinda goli 6?

Mechi ya mkondo wa kwanza PSG walishinda goli 4 ikawa mtaji mkubwa sana kwa PSG, na wao waliamini tayari wameshawatoa Barcelona.

Lakini Barcelona walikuwa bado hawajaamini kama wametoka, kwa sababu moja tu kulikuwa na dakika 90 zingine za ziada.

Dakika 90 za wao kuikata njaa yao. Ndicho kitu ambacho walikifanya, waliingia Nou Camp wakiwa wana njaa sana.

Na walifanikiwa sana kushiba baada ya kuifanya PSG na kuitoa kabisa kwenye michuano hii. PSG walikuwa wameshaamini kabisa wao wameshashinda hii mechi.

Kitu ambacho hakitumiki sana kwenye michuano hii, michuano ambayo huwezi kujihakikishia ushindi kabla ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi.

Mara nyingi PSG huingia katika michuano hii wakiwa wanacheza wakiwa hawana njaa kubwa sana ya mafanikio.

Yani wao huamini ni timu bora na wanaweza kushinda kwa njia ile ile ambayo hutumia kushinda katika ligi kuu yao ya Ufaransa.

Hapa ndipo kosa linapoanziaga. Na Jana walifanya kosa hili hili , waliamini tayari wao wameshapita baada ya kuwafunga Manchester United magoli 2-0.

Waliamini kabisa nyumbani kwao mechi itakuwa imeisha, wakacheza wakiwa hawana njaa, tamaa ya ushindi haikuwepo ndani yao hata kidogo.

Hawakuwa na ile njaa ambayo timu nyingi huwa nazo kwenye hii michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Liverpool bado inaishi kwenye matamanio

Tanzania Sports

Mambo matano niliyojifunza kwenye ushindi wa Arsenal