Mgombea urais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Gianni Infantino amesema yupo radhi kujitoa kwenye kinyang’anyiro hicho ili kumuunga mkono Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Michel Platini.
Uchaguzi huo unaofanyika Februari mwakani umevutia wagombea saba, lakini inavyoelekea kuna mipango ya kuachiana fursa hiyo. Hata hivyo haijajulikana iwapo Platini ataruhusiwa kugombea.
Platini na Rais wa Fifa, Sepp Blatter wamefungiwa kwa siku 90 kujishughulisha na masuala ya soka wakati tuhuma za kupeana mlungula baina yao zikichunguzwa. Blatter anadaiwa kumpa fedha Platini ili ajitoe kwenye moja ya uchaguzi zilizopita, lakini Platini anadai yalikuwa malipo halali kwake, kutokana na kufanya kazi kama mshauri wa ufundi wa rais huyo kipindi cha nyuma.
“Ugombea wangu haumaanishi kwamba nampinga Michel (Platini). Ikiwa atasimama kugombea, nitaondoa jina langu, hii ni kanuni rahisi kabisa ya utiifu. Lakini kwa sasa mie ni mgombea kwa asilimia 100 na nasonga mbele, si kwa Ulaya tu lakini katika soka ya dunia,” akasema Mtaliano huyo.
Infantino, 45, amekuwa katibu mkuu wa Uefa tangu 2009 na aliungwa na kamati ya utendaji ya shirikisho hilo kuwania nafasi hiyo, saa chache tu kabla ya muda wa mwisho wa kuchukua fomu uliokuwa umewekwa wa Oktoba 26.
Wakati huo Platini alishatangza kuwania urais huo, lakini inategemea hatima ya uchunguzi wa Fifa juu ya ripoti za kulipwa pauni milioni 1.35 mwaka 2011 kwa kile kinachodiwa kazi aliyofanya muda mrefu kabla. Alilipwa muda mfupi kabla ya uchaguzi wa Fifa, na ni baada ya malipo hayo alitangaza kujitoa.
Mbali ya Platini na Infantino, wengine wanaowania kiti hicho ni Kiongozi wa Shirikisho la soka la Asia, Sheikh Salman bin Ibrahim al-Khalifa wa Bahrain, Mwana wa Mfalme wa Jordan, Ali bin al-Hussein, mwanasiasa wa zamani wa Afrika Kusini, bilionea Tokyo Sexwale, Rais wa Shirikisho la Soka la Liberia, Musa Bility na ofisa wa zamani wa Fifa, Jerome.
Infantino anasema kwamba akichaguliwa kuiongoza Fifa, atatanua ushiriki kwenye timu katika Kombe la Dunia, kutoka 32 zilizopo sasa hadi 40, hatua hiyo ikienda sambamba na ya Uefa kutakakugeza nchi kwenye michuano yake kutoka 16 za sasa hadi 24.