* Atabaki nje kwa dhamana, akisubiri hukumu yake
Mwanariadha maarufu mwenye ulemavu wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius ametiwa hatiani kwa kosa la mauaji, lakini si kwa kukusudia.
Jaji Thokozile Masipa wa Mahakama Kuu ya Afrika Kusini alifikia uamuzi huo Ijumaa hii, akisema kwamba mwanamichezo huyo alitumia vibaya silaha yake kwa kufyatua risasi kupitia mlango ambayo kwa bahati mbaya ilimuua mpenzi wake, Reeva Steenkamp.
Jaji Masipa alisema kwamba Pistorius alifanya uzembe hata kama aliamini kwamba kulikuwa na mtu amemvamia kwenye nyumba yake, ambapo Alhamisi katika uamuzi wake wa awali alisema Jamhuri ilishindwa kuthibitisha kwamba Pistorius alimuua mpenzi wake huyo kwa kukusudia.
Pistorius pia ametiwa hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya silaha, ambapo alifyatua risasi ilikwenda hadi katika mgahawa mmoja. Baada ya kutiwa hatiani huko, Pistorius alifuta uso wake, akainama kidogo kisha akatulia.
Kwa mwenendo wa usomaji wa jaji, wengi mahakamani hapo walishajua angetiwa hatiani kwa kuua bila kukusudia, ambapo katika adhabu itakayotolewa ndani ya wiki chache zijazo, itajulikana kipindi atakachokaa jela.
Kwa kosa la kuua bila kukusudia, Pistorius anaweza kutupwa jela kwa miaka kati ya 10 hadi 15 japokuwa wataalamu wengine wa sheria wanadai kwamba si ajabu akafungwa hata miaka saba.
Jaji Masipa alisema kwamba Pistorius (27) alibubujikwa alichukua hatua haraka mno kufyatua risasi. Akimsafisha dhidi ya mashitaka ya kuua kwa kukusudia juzi, Jaji Masipa alisema hangeweza kufikiria kuua mtu yeyote aliyekuwa nyuma ya mlango wa choo.
Comments
Loading…