Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ametaka viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuandamana na wenzao wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), ili kudumisha muungano.
Alikuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Dimani (CCM), Hafidh Ali Tahiri, aliyedai kuwa TFF inavunja Katiba ya nchi kwa sababu haishirikishi viongozi wa ZFA kwenye ziara zao nje ya nchi.
Pinda alisema sio vibaya viongozi wa TFF kwenye ziara zao nje ya nchi kuandamana na angalau kiongozi mmoja wa ZFA, hali ambayo itaimarisha muungano na kuondoa manung’uniko.
Alisema malalamiko yanayotolewa yana msingi kwa sababu, yanajenga dhana mbaya ya muungano na kuwataka mawaziri kufanya ziara Zanzibar kuangalia maeneo mbalimbali.
Hivi karibuni viongozi wa ZFA walilalamikia kitendo cha viongozi wa TFF kuhudhuria mkutano mkuu wa FIFA katika kisiwa cha Bahamas bila ya kuambatana nao.
Hata hivyo, hivi karibuni maofisa wa TFF walidai kuwa mialiko wanayopata kutoka FIFA huja kwa nyadhifa za viongozi wa TFF, ambao ndio mwanachama wa FIFA.
TFF ndio inayotambuliwa na FIFA wakati ZFA ilikwama maombi yake ya kujiunga na FIFA kutokana na Zanzibar kuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano.
Comments
Loading…