in , , ,

PESA YA MAFUTA ITALETA WABABE WAPYA ULAYA

Kwenye msimu wa Ligi Kuu ya Ufaransa wa 1993/94 Paris Saint-Germain (PSG) walitwaa ubingwa. Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa klabu hiyo kutoka jijii Paris kunyakua taji la ligi hiyo.

Kabla ya hapo klabu hiyo iliwahi kutwaa taji hilo kwenye msimu wa 1985/86. Kilichofuata tangu ubingwa wao wa pili wa 1993/94 ni ukame wa zaidi ya misimu 15.

Mbaya zaidi klabu hiyo ikawa na misimu kadhaa mibaya iliyoleta rekodi zisizohitajika kukumbukwa na miamba hiyo ya sasa ya soka la Ufaransa. Msimu mbaya zaidi ukiwa wa 2007/08 ambapo klabu hiyo ilimaliza kwenye nafasi ya 16.

Bao la kusawazisha la Jeremy Clement kwenye mchezo wa 37 wa ligi ambao PSG ilicheza dhidi Sait Ettiene ndilo lililoihakikishia timu hiyo kubakia kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa.

Bao hilo liliinusuru klabu hiyo na kushuka daraja kwenye msimu huo wa 2007/08 ambapo ilimaliza kwenye nafasi ya 16 ikiwa na alama tatu zilizoitenganisha na ukanda wa kushuka daraja.

Msimu uliofuata wa 2008/09 klabu hiyo ikamaliza kwenye nafasi ya 6 kisha kushuka mbaka nafasi ya 13 kwenye msimu wa 2009/10.

Kwenye msimu wa 2010/11 klabu hiyo ikamaliza kwenye nafasi ya 4 chini ya mwalimu Antoine Kombouare. Mafanikio hayo yakawavutia wawekezaji kutoka Qatar ‘Qatar Sports Investments’ kuwekeza kwenye klabu hiyo.

Juni 2011 wawekezaji hao wanaotumia mapato ya ziada ya mauzo ya mafuta kwa ajili ya uwekezaji nje ya biashara ya mafuta wakainunua klabu hiyo. Kilichafuata ni usajili wa wachezaji wa daraja la juu na makocha wa aina hiyo hiyo.

Kwenye msimu wa kwanza wa wawekezaji hao zaidi ya euro milioni 100 zilitumika kusajili nyota kadhaa akiwemo Javier Pastore aliyesajiliwa kutoka Palermo ya Italia kwa euro milioni 42 na kuvunja rekodi ya usajili wa pesa nyingi Ufaransa.

Wengine walikuwa Blaise Matudi, Kevin Gameiro na Jeremy Menez. Dau hilo la jumla lililotumika na PSG kusajili nyota hao lilikuwa ni mara tatu ya kiasi kilichotumika na Lille waliokuwa mabingwa watetezi kwenye msimu huo.

Wakafanikiwa kumleta na Leornado Araujo kama Mkurugenzi wa michezo kwenye klabu na baadaye kumsainisha Carlo Ancelotti kuwa meneja wa klabu hiyo Disemba 2011.

Hata hivyo alama 79 zilizokusanywa na timu hiyo kwenye mismu huo wa 2011/12 hazikuweza kuwawezesha kutwaa taji la Ligi Kuu ya Ufaransa. Montpellier waliwapiku na kutwaa ubingwa huo kwa alama 82.

Msimu uliofuata pesa ya mafuta ikatumika kusajili majina kama Thiago Silva, Ezekiel Lavezzi, Zlatan Ibrahimovic na Marco Verratti.

Nyota hao na wengine waliokuwepo wakatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa kwenye msimu huo wa 2012/13 wakiwaacha kwa alama 12 Marseille waliokamata nafasi ya pili.

Huo ulikuwa ni ubingwa wao wa 3 wa Ligi Kuu ya Ufaransa kwa klabu hiyo tangu kuanzishwa kwake. Kilichofuata hapo ni ubabe wa miamba hiyo ndani ya soka la Ufaransa mbaka hii leo.

Pesa ya mafuta ikabadili kabisa upepo wa Ligi hiyo. Wababe hao wakatwaa ubingwa kwenye mismu miwili iliyofuata ya 2013/14 na 2014/15 wakiwaacha washindi wa pili kwa alama 8 au zaidi kwenye misimu yote miwili.

Juzi Jumapili wababe hao kutoka Paris wa litwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa msimu huu baada ya kuwabomoa Troyes 9-0. Wamekuwa timu ya kwanza Ulaya kushinda taji la Ligi baada ya michezo 30.

Pesa ya mafuta imewafanya kuwa wababe wa soka la Ufaransa. Nini kinafuata? Ni dhahiri kuwa miamba hiyo ya Ufaransa inakwenda kuwa wababe wa Ulaya muda si mrefu.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Leicester wazidi kupaa

Tanzania Sports

HAYA YANAWEZA KUWAFANYA ARSENAL WAWASHANGAZE BARCA