Nyota wa Arsenal, Mesut Ozil amegoma kukatwa asilimia 12.5 ya mshahara wake, tofauti na ilivyokubaliwa na wachezaji pamoja na kocha wao, Mikel Arteta.
Kima hicho kilikubaliwa kwa ajili ya kupunguza makali ya kifedha wakati huu ambapo dunia imeathiriwa na virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu – ugonjwa ambao tayari umeua maelfu ya watu.
Ozil anayepata pauni 350,000 kwa wiki, akiwa ndiye analipwa zaidi ya wachezaji wote na bado hajatafsiri thamani hiyo uwanjani katika miezi ya karibuni, hataki kuwa sehemu ya mpango huo.
Arsenal walitangaza Jumatatu ya wiki hii kwamba kukatwa mshahara ni kitendo cha hiari kilichokubaliwa na wachezaji wa kikosi cha kwanza, kocha mkuu na jopo lake la karibu, na kwamba watakatwa kwa muda wa miezi 12. Ni klabu ya kwanza hapa kutangaza hayo.
Hata hivyo, Ozil ambaye anatakiwa kuwa kiongozi kutokana na uandamizi wake hapo Emirates, inaelezwa hajashawishika kukubaliana na hilo, na kwamba ana wenzake wawili ambao hawajatajwa, wanaoshinikiza uamuzi huo ubadilike na iwe kwamba kima hicho kisogezwe mbele – walipwe baadaye na si kukatwa moja kwa moja.
Mazungumzo yalifanyika binafsi kati ya mchezaji mmoja mmoja na uongozi. Chama cha Wachezaji wa Kulipwa (PFA) kiliwashauri wachezaji dhidi ya kukubali kukatwa mishahara, kikisema kwamba kodi inayopelekwa kwenye Idara ya Huduma za Afya (NHS) nayo itapungua hivyo hakuna kitakachokuwa kimesaidia.
Katika mazungumzo na wachezaji wake Jumatano ya wiki iliyopita, inaelezwa alishiriki kwa kiasi kikubwa kujenga umoja klabuni na hata kutia cheche iliyosababisha wengi wao kubadili mioyo yao kwa ajili ya kushiriki kusaidia kupunguza makali ya kifedha yaliyotokana na janga hili kubwa.
“Tunapenda kuwatangazia kwamba tumefikia makubaliano ya hiari na wachezaji wetu wa kikosi cha kwanza, kocha mkuu na jopo lake, kwa ajili ya kuiunga klabu katika wakati huu mgumu. Hatua hii inafuatia mjadala chanya na wenye kujenga.
“Katika mjadala huo, wengi walionesha kuguswa na ukubwa wa tatizo hili linalosababishwa na Covid-19. Kwa hakika wameonesha ile hamu ya kushikamana na kuungana mkono kama familia ya Arsenal,” taarifa ya klabu ikasema.
Wachambuzi wa soka kwenye televisheni, Gary Neville na Jamie Carragher wamejitokeza na kumpinga Ozil (31), wakisema alitakiwa kuwa mfano kwa wenzake, hasa wale wadogo na wanaopata mshahara mdogo kuliko yeye.
Wanaonya kwamba nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani anajiweka katika hatari ya kutengwa. Carragher anasema kwamba hilo linaweza kuwa tatizo. Akasema kwamba kuna makundi mawili ya wachezaji wanaoweza kukataa kukatwa mishahara – wale wadogo wasiokuwa na kipato kifaacho na wale ambao mikataba yao inamalizika.
“Sasa kama mchezaji anayelipwa kiasi kikubwa zaidi cha fedha anakataa kukatwa asilimia hiyo ndogo, inakuwaje kwa hao wengine wanaolipwa kidogo. Kwa kweli hii ni sawa na kujifunga bao mwenyewe. Simlaumu kwa kiasi kikubwa cha fedha anacholipwa, labda walaumiwe wanaolipwa, lakini anayelipwa kima kikubwa zaidi anatakiwa kuonesha mfano kwa wengine,” akasema mchezaji huyo wa zamani.
Neville alisonga mbele zaidi na kusema kwamba vitendo vya Ozil haviwezi kutetewa hata kidogo. “Kanuni ya kutokuwa pamoja kama familia na kundi haifai na kamwe haiwezi kutetewa. Mnakuwa timu moja ndani na nje ya uwanja,” akasema Mwingereza huyo.
“Nisingependa kabisa kuwa mmoja kati ya hao watatu wanaokataa. Itawafanya watengwe kutoka kwa wengine. Wakati kundi la wachezaji wanapigia kura kitu fulani, unatakiwa kwenda nao na kuwa sehemu yao.
“Hii inaonesha tu magumu yalipomo kwenye klabu za Ligi Kuu ya England (EPL). Soka inajila yenyewe kutoka ndani kwa ndani. Klabu nyingi na wachezaji hawapo kwenye vita bali katika mapambano makubwa. Kuna wachezaji hawana imani na klabu na huu ni mfano mmoja tu,” akasema Neville