Menu
in , , ,

Okwi amegeuka kisiki cha mpingo

KAMA  kuna jambo linatoa somo kwa viongozi wa soka la Bongo, basi ni
usajili wa Emmanuel Okwi. Tukirudi nyuma tunakumbuka usajili wa
Ramadhan Wasso, Victor Costa na mastaa wengine waliowahi kuzichanganya
klabu za Simba na Yanga.

Kwa namna moja au nyingine utaona kuwa viongozi wetu bado hawajagundua
nini maana ya usajili wa wachezaji.

Kwa kuwa klabu zetu hazina mpango
wa kuwekeza kwa vijana, kilichobaki ni kuhangaishana kila kukicha na
wanampigania staa huyo wa Uganda kana kwamba ana uwezo mkubwa kuliko
wazawa.

Katika ulimwengu wa soka mchezaji anapiganiwa kwa bei yake sokoni na si
kwa usumbufu au vinginevyo. Leo viongozi wa timu wanawafanya wachezaji
kama vyuma ambavyo haviwezi kuwa na mioyo au akili.

Mchezaji kama Okwi hakupaswa kuwa wa kogembewa. Kwa sasa ametengenezwa
kuwa kama kisiki cha mpingo kutokana na kushindwa kudhibitiwa.
Viongozi wa soka la Bongo wamefanya jamaa huyo wa Uganda kama mchezaji
wa kipekee wakati wapo wachezaji kama Mbwana Samata au Thomas
Ulimwengu ambao wanafanya vema TP Mazembe.

Katika hali ya kawaida ilibidi kujiuliza swali jepesi tu; ni kweli
Okwi amekuwa na kiwango cha kutisha kuliko nyota wetu akina Hassan
Dilunga?
Ni kwa namna gani Okwi anaweza kuwa bora zaidi ya akina Juma Luizio?
Kutokana na ubabaishaji tumemwona staa wa zamani wa Mtibwa Sugar, Juma
Luizio akitimkia Zesco ya Zambia badala ya kuzihangaikia klabu za Simba na
Yanga.

Kwa namna yoyote ile Yanga walifanya kosa kumsajili mchezaji na
kumpa masharti ya mkataba ambayo hawawezi kutekeleza.
Okwi alichota takribani shilingi milioni 90 za Yanga za usajili tu
achilia mbali mshahara wake wa shilingi milioni sita kila mwezi. Sababu kubwa
ilikuwa kukwezwa na viongozi wa Yanga, ambapo sasa Simba nao wamemtwaa
na kumgeuza kuwa kisiki cha mpingo.

Bila hata uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya TFF
kukata mzizi wa fitna kwa kuweka wazi kuwa Yanga walishavunja mkataba
na Okwi kwa kushindwa kumlipa sehemu ya fedha za usajili na mshahara
kama walivyokubaliana katika mkataba, bado mchezaji huyo hajafikia
hadhi ya kugombewa kiasi hiki.

Lakini sifa kubwa ambayo anaweza kuichukua Okwi ni kwamba ametoa
fundisho kwa viongozi wa klabu zetu kuwa mikataba inapoingiwa inabidi
wawe makini na utekelezaji wa masuala yanayokubaliwa.

Suala hili linaweza kuwa fundisho kwa wanasoka wengine, wakiwamo
wazawa kwamba ni vema wakawa na misimamo katika suala zima la
kupigania haki zao.

Pia viongozi wa klabu za soka na hata kampuni mbalimbali, ni vema
wakajifunza kuheshimu mikataba na wafanyakazi wao kwani mara nyingi
imetokea waajiriwa kujikuta wakihaha bila mafanikio kupigania haki zao
za msingi kutokana na ubabaishaji wa wakubwa wao.

Katikati ya wiki hii nilipata taarifa kuwa Yanga wanataka kwenda FIFA
kumshitaki Okwi na Simba kwa ‘umafia’ waliowafanyia. Binafsi, bado
nimebaki pale pale katika pointi ya msingi waliyoitumia TFF kumweka
huru Okwi kuwa kati ya Yanga na Mganda huyo, ni nani aliyeanza kuvunja
mkataba?

Je, ni Okwi aliyeanza kususa kucheza mechi za mwisho za mzunguko wa
pili au Yanga walioshindwa kumlipa chake pamoja na kumpa nyumba kama
walivyokubaliana?
Tunaweza kukaa chini na kujaribu kufikiri kwa kila njia kwamba FIFA
itaamua nini, lakini kwa taratibu za kazi kati ya Yanga na Okwi
zinaonesha wazi kuwa upande usiotekeleza makubaliano ya mkataba lazima
hatua stahiki ichukuliwe.

Kwa maana hiyo Yanga na Simba wamemfanya mchezaji huyo kuwa kisiki cha
Mpingo, hali ambayo haikutakiwa hata kufikiriwa.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version