Soka inapita katika uvuli wa mauti, wakati huu wa maambukizi na vifo vinavyotokana na virusi vya corona.
Waliokuwa wamezoea kuwa nyuma ya seti za televisheni kuwasikilisha wachambuzi wakati mechi zikiendelea au baada ya kumalizika sasa hawawezi tena; waliokuwa wakijiingiza kwenye kamari kama moja ya njia za kukuza kipato sasa wameliwa. Watu hawapo mitaani nje – imekuwa kama mahame.
Ile raha ya kutazama soka uwanjani kwa waliokata tiketi za msimu na waliokata za mechi mahsusi kwa klabu zao imetoweka; watu wamejifungia ndani wakiwa na tabu kubwa, wasjiue lini janga liamalizika na serikali za nchi zao kuwaruhusu tena kuwa mitaani.
Walio bize kwa sasa ni watoa huduma za afya ambao wanazidisha muda wa kazi kwa ajili ya kuokoa maisha ya maelfu ya watu walioathirika pande mbalimbali za dunia. Ligi Kuu ya England (EPL) iliyokuwa inaelekea ukingoni kwa Liverpool kutabiriwa ubingwa nayo imekwama, maswali yakiwa mengi kuliko majibu.
Mapolisi nao pamoja na wanajeshi katika nchi mbalimbali wanahangaika kuhakikisha kwamba watu wanafuata maelekezo ya kujitenga au kuwa ndani kama familia isipokuwa kwa sababu muhimu na maalumu tu.
Imetokea kwamba katika nchi kama Uganda, Rwanda na India watu wameadhibiwa vikali hata kwa kutumia silaha kutokana na ukaidi. Lakini hayo yakiendelea, maisha yanaonekana kwamba ni kama kawaida nchini Tanzania.
Watu wanaendelea kwenda kazini na kwenye biashara kama kawaida na hata tumeona wachezaji wakiendelea na mazoezi. Kweli zipo sehemu ambako pamewekwa vitasaka mikono, maji na sabuni, lakini watu wapo mitaani kama kawaida, na jioni wanapita baa na kwenye grosari kupata moja moto moja baridi kama ambavyo ilikuwa kabla ya janga la COVID-19.
Tanzania, kama Kenya, wamepata kifo kimoja kutokana na maambukizi na Italia, Hispania na Marekani zinaendelea kuwa katika wakati mgumu – vifo vikizidi na maambukizi kadhalika, japokuwa walau ile kasi imepungua tangu Baba Mtakatifu Francisco aendeshe sala maalumu kwa ajili ya kuomba maepusho ya janga hilo.
Tuliona pia picha za polisi wakipambana na Oumnar Niasse wa Everton kutokana na kukaidi amri ya kukaa nyumbani na kutosogeleana na watu. Imekuwa sasa ikiwa una kitu unachukua kwa mtu kinawekwa chini, unafika unamsalimu kwa mbali unakichukua na kuondoka.
Ni watu wachache katika Tanzania niliowasiliana nao ambao wanafanya kazi kutoka nyumbani na kuchukua hatua za hadhari. Wengi wao ni wale wanaofanya kwenye mashirika ya kimataifa, lakini hawa wengine wanaendelea kupanda mabasi na kwenda kazini au kwenye biashara kama kawaida – yakiwa ni maisha ya kubangaiza. Hakuna akiba ndani, hakuna fedha za kutosha benki au mifukoni kwa hiyo watu wanaendelea kuhangaika.
Ni wiki tatu zimekatika tangu kukatika kwa mawasiliano ya kisoka, baada ya zile raundi za mechi za EPL kuahirishwa na hivyo kukosa utamu wa ligi yenye mvuto mkubwa zaidi duniani. Wanasoka hawawezi tena kutufanya kucheka, kulia, kuropoka au kushangilia kwa sababu hawako ten ana mpira. Wamejifungia makwao.
Zilitoka meseji zilizokuwa zikilaani wamiliki wa klabu kwa kuwalipa wanasoka mamilioni ya pauni huku manesi na madaktari wakipata kiduchu, na sasa wanasema wawaite wanasoka hao wawaponyeshe wagonjwa wa COVID-19.
Wakati Cristiano Ronaldo ametoa hoteli kwa ajili ya matabibu huko Ureno, golikipa namba moja wa Manchester United, David De Gea alitoa kima cha £275,000 kwa ajili yam ji wake wa Madrid kutokana na athari za ugonjwa huo mbaya. Kadhalika, Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola ametoa euro milioni moja kwa ajili ya jimbo la kwao la Katalunya.
Watu wengi wamekwama na kukwazwa na ugonjwa huu, huku mapato ya klabu yakianguka hivyo kwamba klabu zinafikiria jinsi ya kukata watu wao mishahara ili kuweza kujiendesha kwa sababu hawajui hali hii itaendelea kwa muda gani.
Huduma za utalii ni kana kwamba zimesimama, lakini uzuri kwa Afrika ni kwamba haukuwa msimu wa utalii (peak season). Itakuwa kilio na kusaga meno iwapo hali hii itaendelea kwa miezi kadhaa ijayo, kwani Juni ni msimu wao na wengi walishaahidi kuingia Tanzania, baadhi wakiwa ni kutoka Italia, Israel, China nan chi nyingine zilizoathirika ambapo mashirika ya ndege yameweka chini madege yao kwa muda.