Norwich City wameungana na Bournemouth na Watford kupanda daraja kucheza Ligi Kuu ya England msimu ujao.
Wamefikia hapo baada ya kuwahsinda Middlesbrough 2-0 kwenye mechi ya mtoano ya kufuzu iliyopigwa Uwanja wa Taifa wa Wembley Jumatatu hii.
Walikuwa ni Cameron Jerome na Nathan Redmond waliofunga mabao ya mapema na kuwahakikishia Canaries udhibiti wa mechi hiyo katika nusu ya kwanza.
Boro walikuwa hovyo katika dakika za mwanzo, wakajirekebisha na kupambana kufa na kupona kipindi cha pili lakini maji yalishazidi unga.
Norwich walifuzu kwa mechi ya Jumatatu baada ya kuwafunga Ipswich Town kwenye mechi za nusu fainali zilizolenga kupata timu moja ya kupanda.
Norwich wamecheza msimu mmoja tu kwenye Ligi Daraja la Kwanza kwani walishika 2014 baada ya kuwa juu kwa misimu mitatu mfululizo.
Ilikuwa mechi myhimu ambapo washindi wanapewa zawadi ya pauni milioni 120, na ndani ya dakika 15 za kwanza Norwich walishaanza kuhisi harufu ya ligi kuu.
Washabiki 85,000 walishuhudia mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi mahiri, Mike Dean, ambapo kocha Alex Neil wa Norwich alishangilia kupita kiasi, akiwa ameshinda mechi 18 kati ya 25 Norwich walizocheza chini yake.
Middlesbrough wamekuwa na mkosi na mechi za jinsi hii, kwani hawajaweza kupata ushindi Wembley mara tano walizofika hapo.
Kocha wao, Aitor Karanka anarudi Championships akiwa na matumaini ya kutimiza ndoto ya ligi kuu msimu wa 2016/17, akiwa amefungwa mabao 37 katika mechi 46.
Karanka alikuwa msaidizi wa bosi wa Chelsea, Jose Mourinho enzi hizo wakiwa Real Madrid na amekuwa Boro kwa miezi 18 tu, alipowakuta wakiwa nafasi ya 16 na sasa amewapandisha hadi ya nne.
Timu zilizoshuka daraja hadi la pili ni Millwall, Wigan na Blackpool ambazo zitaenda kujiuliza huko. Wigan wameendelea na mporomoko wakianzia Ligi Kuu, Championships na sasa wanaendelea kushuka – huenda huko wataweka breki.