Mdudu wa nidhamu mbovu na utawala mbaya wa soka Afrika anaendelea Brazil, ambapo wachezaji wa Brazil wamegomea mazoezi.
Wachezaji hao waliofanikiwa kuwavusha Nigeria kutoka hatua ya makundi na watachuana na Ufaransa Jumatatu kwenye mtoano wanadai malipo ya bonasi zao.
Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan anayepambana na magaidi wa Boko Haram nyumbani, ameingilia kati na kuwahakikishia wachezaji hao kuwa watalipwa posho zao.
Super Eagles waligomea mazoezi Alhamisi wakihofia kwamba wakiendelea kucheza hawatalipwa baada ya mashindano hayo.
Hii inaonesha kuna walakini katika utawala wa soka, kwani baada ya Cameroon na Ghana kutumbukia humo humo na kisha kutolewa baada ya mzozo, mabingwa hawa wa Afrika wanaleta aibu mpya.
Wachezaji wanataka walipwe chao sasa lakini Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) linasema kwamba halina fedha hivyo haliwezi kuwalipa hadi Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) litakapowalipa.
Suala la Ghana lilikuwa ni la posho za ushiriki, ambapo Chama cha Soka cha Ghana kilitaka kusubiri hadi Fifa watoe fedha hizo, lakini Rais John Dramani Mahama akaingilia kati na kutoa fedha hizo kutoka serikalini.
Walilipwa fedha hizo na mechi iliyofuata wakapoteza na kufungishwa virago. Cameroon wao walitaka fedha kabla hata ya kupanda ndege kwenda Ubelgiji na walipofika tu wakaanza kucharazwa mechi ya kwanza hadi ya mwisho.
Nigeria wanaingia kwenye mzozo wakati mgumu wanapokaribia kuwakabili Ufaransa ambao ni wazuri msimu huu, huku Nigeria wakivutana pia juu ya kiwango cha malipo.
Wachezaji wanaamini kwamba wanatakiwa walipwe kila mmoja dola 30,000 kwa kufuzu kuingia 16 bora.
Hata hivyo, NFF inasema watalipwa dola 15,000 kila mmoja na mchanganuo wake ni dola 10,000 kila mmoja kutokana na ushindi wa 1-0 dhidi ya Bosnia-Hercegovina na dola 5,000 kwa kwenda sare na Iran. Walifungwa na Argentina hivyo hawadai chchote.
Wakati makundi hayo mawili yakijaribu kufanya kazi ili kupata ufumbuzi, kocha Stephen Keshi anasistiza kwamba sintofahamu hiyo haitawaathiri wachezaji wake katika fainali zinazoendelea.
Kuna habari kwamba wachezaji wamekubali kuendelea na mazoezi wikiendi hii tayari kwa mechi hiyo ya Jumatatu.
Hii si mara ya kwanza Nigeria wanaleta mzozo juu ya posho, kwani mwaka jana walichelewa kufika nchini Brazil kwa ajili ya kushiriki Kombe la Mabara baada ya kushikana mashati na wakubwa.
Comments
Loading…