Kwa muda mrefu pamekuwapo hoja ya kujumuisha watu wa aina tofauti, kwa maana ya asili, rangi na jinsi nyingine kwenye uongozi wa soka, lakini wahafidhina waliokaa madarakani muda mrefu wamekuwa wazito kubadilika.
Ipo fursa sasa ya kuchukua hatua hiyo wakati huu ambapo mambo kadhaa yamejiweka wazi. Kwanza kuna nafasi wazi za waandamizi zinatakiwa kujazwa kwenye Chama cha Soka (FA), Bodi ya Ligi Kuu ya England (EPL) na Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA).
Tunaona kwamba Greg Clarke ameondoka kwenye uongozi wa soka, lakini suala la kina kwenye uongozi wa soka kwa muda mrefu kuwa na utata na kukosa usawa, hasa kwa wasio Wazungu halisi linabakisha hali ya uongozi kwenye mamlaka nyingi kuwa si nzuri.
Clarke alijiuzulu nafasi yake ya Uenyekiti wa FA, baada ya kuwa ametoa kauli kandamizi na za kibaguzi kuhusiana na watu wanaotoka kwenye makundi madogo na ambayo kwa muda mrefu hayajapewa haki yao kwenye uongozi wa soka.
Amekiri kwamba amefanya makosa kwa kutoa kauli husika, tena mbele ya wawakilishi wa wananchi na kwamba aliwakosea wanawake, watu weusi, Waasia na wale wenye mapenzi ya jinsia moja na jamii zao.
Hayo yakijiri, ni wakati huu kuwa wakweli kila mmoja katika nafasi yake na kujiuliza na kufikia hitimisho ni kwa jinsi gani tunavyotambua watu kuwa viongozi. Changamoto ni kubwa ya kupata viongozi ambao kwa hakika watapeleka mchezo huu pendwa wa soka kwenye mwelekeo sahihi.
Ni kwa vipi mchezo wenye mchanganyiko wa watu wengi hivi walio na vipaji na uwezo mkubwa, ushindwe kuhakikisha kwamba kila mmoja anapewa nafasi? Si sahihi kwa afya ya mchezo huo kitaifa na mabadiliko yanatakiwa sasa.
Theluthi moja ya wachezaji wanaume wa soka ni weusi na ni vipaji hivyo vinavyosaidia kwa kiasi kikubwa kuingiza mapato ya pauni bilioni moja kila msimu, ikiwa ni theluthi moja ya mapato ya jumla kutokana na matangazo ya TV na EPL.
Lakini ajabu ni kwamba, miongoni mwa klabu zote 92, ushawishi na utawala wa weusi hawa ni mdogo sana. Yupo Ben Robinson pale Burton Albion – Mwenyekiti pekee katika historia kuwa mweusi klabuni.
Kwingineko, FA hivi karibuni ilimteua Edleen John kwenye uongozi wa timu na Bobby Barnes amekuwa Naibu Mtendaji Mkuu kwenye PFA. Paul Elliot ni mwangalizi pale kwenye Bodi ya FA lakini hakupewa sifa ya kupiga kura. Paul Cleal ni mwakilishi wa kwenye Bodi ya EPL. Lakini unaweza kuona kwamba ndio weusi wanahesabika kabisa, wengine wote wakiwa ni Wazungu weupe.
Tangu Taarifa ya McKinsey ichapishwe 2014, ikisisitiza haja ya kuwa na mjumuisho wa watu kutoka matabaka mengine hasa hayo madogo, hakuna hatua za dhati zilizochukuliwa, watu wale wale wakikaa kupanga hayo lakini wanajirudisha hao hao – weupe.
Ni wakati wa dhamira halisi kuonekana wazi ambapo FA inahitaji mwenyekiti mpya huku EPL na PFA nao wakihitaji kuweka viongozi wapya waandamizi. Kama wana nia kweli, basi tutaona wakati huu. Je, mfumo gani utatumika kuwapata au ni ujanja ule ule wa kurejesha wa ain ana asili hiyo hiyo?
Gemu inatakiwa kuondoka kwenye mfumo unaowatambua weupe tu kuwa na vipaji vya uongozi kwa hiyo hata weusi na Waasia wana sifa hizo, wapewe nafasi na si kuweka weupe tena wanaume tu karibu kila mahali.
Kampuni za aina nyingi sasa zipewa zabuni ya kuandaa mpango wa kuchagua viongozi mchanganyiko na watakaokuja kweli kuleta mapinduzi kwenye utawala wa soka. Mchanganyiko wa watu hawa wa aina mbalimbali inamaanisha biashara nzuri Zaidi. Je, soka itaendelea kusubiri hadi lini?
Comments
Loading…